ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 17, 2012

Umejifunza nini baada ya Valentine kupita?

JUZI, Jumanne, Februari 14, mwaka huu, dunia nzima ilikuwa inaadhimisha Sikukuu ya Wapendanao. Wenye lugha yao, wanaiita Valentine’s Day. Yes! Ni siku ya kuonesha namna unavyomjali, kumpenda na kumthamini mtu wako wa karibu.
Nguo nyekundu zilivaliwa, maua yakanunuliwa na kila aina ya viashiria kwamba ni siku ya wapendanao vilifanyika. Ilikuwa furaha sana kwa wale waliooneshwa kupendwa na ndugu zao, wazazi, marafiki au wapenzi.
Kwa wanandoa ilikuwa siku muhimu zaidi kwao, maana chimbuko halisi la maana ya siku hiyo ni muasisi wake, Padre Valetino, kutetea vijana wafunge ndoa na siyo kufanya uzinifu.
Wapo ambao hawana ndoa, lakini siku yao iliisha vizuri na wapenzi au wachumba wao kwa kuoneshwa thamani kubwa zaidi namna wanavyopendwa.
Hayo yote ni furaha, lakini marafiki zangu, siku zote hakuna tamu isiyo na chungu, pia hakuna chungu isiyo na tamu. Naamini wapo ambao wamebaki na maumivu makubwa baada ya siku hiyo kupita.
Wapo wanaoilaani siku hiyo, kwamba huenda kama isingekuwepo wasingepata matatizo makubwa ambayo wameyapata. Kuna mengi ambayo yametokea.
Inawezekana wewe unayesoma hapa ulipata matatizo. Uliteswa. Ulinyanyaswa. Ulisalitiwa, ulionewa na kushushwa thamani yako. Pole sana, lakini usijali maana unasoma safu yenye dawa ya maumivu yako.
Yes! Let’s Talk About Love, kwa kutumia lugha ya kirafiki, siku zote ndiyo jibu la matatizo yako yote yanayohusu mambo ya mapenzi.
Acha kulia, futa machozi yako, halafu sasa weka ubongo wako tayari kupokea kitu kipya. Nakuhakikishia utakuwa na mtazamo mpya ambao utakuwa mwongozo wa maisha yako yajayo katika sayari ya wapendanao.
Twende tukajifunze.

MAPITIO MUHIMU
Nilishazungumza juu ya hili katika makala yangu yangu ya utangulizi ya Sikukuu ya Wapendanao. Nilieleza kwa mapana juu ya asili ya siku hii.
Kimsingi ni siku ya kumkumbuka Mtakatifu Valentino ambaye alikamatwa enzi za Utawala wa Dola ya Warumi, huko Roma, akakaa gerezani kwa muda kabla ya kuhukumiwa kifo.
Kosa alilopatikana nalo Mtakatifu Valentino ambaye alikuwa ni Padre ni kufungisha ndoa za siri.
Kihistoria, Dola ya Warumi ilitamani sana kutawala sehemu kubwa ya dunia, hivyo waliwataka vijana wengi waachane na mambo ya kuoana na badala yake waingie vitani!
Mtakatifu Valentino kwa kuona hivyo, aliamini vijana wengi waliangukia katika dhambi ya uzinifu. Ni kweli walifanya hivyo. Kwa kuwaepusha vijana na dhambi hiyo, aliamua kuwafungisha ndoa kwenye mahandaki yaliyokuwa chini ya kanisa.
Kabla ya kifo chake, Mtakatifu Valentino aliwataka watu wapendane, akiwa gerezani alisambaza ujumbe kwa watu waliomtembelea kwa kupitia makaratasi. Ndiyo hasa maana ya uadhimishwaji wa siku hiyo.

TAZAMA TOFAUTI
Mtakatifu Valentino ambaye kwangu mimi ni Baba wa Upendo, alikuwa na maana kubwa aliposaidia vijana wengi kuingia kwenye ndoa. Hata ilipopokelewa na kuonekana siku muhimu ya upendo, watu walisisitizwa kuoneshana upendo wa ndani.
Ilikuwa vigumu sana kupokelewa, lakini baada ya mafundisho ya kutosha, jamii ilielewa maana ya siku hiyo na kuipokea kama ilivyo.
Tatizo limekuja katika miaka ya hivi karibuni, siku hiyo kugeuzwa ni ya ‘ngono’. Kwa maneno mengine kwa watu wengi zaidi au pengine nusu ya wanaoadhimisha, huamini kuwa ni ‘siku ya ngono’.
Kuna ambao wanafuata mkumbo, kwa maana kwamba hawana elimu juu ya asili ya siku hiyo. Anakutana na mtu Februari 02, halafu tarehe 14 ya mwezi huo, appointment yao inakuwa gesti.
Siyo Valentine!
Si Mtakatifu Valentino huyo mtetezi wa wanandoa. Mfia imani ambaye alitaka watu wafunge ndoa na kuacha uzinifu. Hiyo ni sikukuu yao wenyewe. Tena ingekuwa vyema kama wangeitafutia jina.

ULITOKA NA NANI?
Kwa kuwa leo nazungumza na wenzi zaidi, acha tujadili juu ya hili. Siku hiyo ulitoka na nani? Marafiki zangu, upendo wa kweli huonekana zaidi katika siku muhimu na maalum kama hiyo.
Unakuta mtu ana mkewe, lakini ana vimada watatu na wote wanataka kutoka naye. Kinachotokea hapo ni kumchenga mkewe kisha anapanga ratiba.
Asubuhi na mapema anakwenda Kimara, mchana anahamia Kijitonyama, halafu jioni kabisa anawahi Ubungo, kutafuta basi la Morogoro. Hapo anakwenda kwa hawara yake mwingine anayeishi Kihonda!
Mkewe kamdanganya ana kazi muhimu Chalinze. Eti naye anaadhimisha Valentine’s Day! Siyo kweli.
Rafiki zangu, bado kuna mengi ya kuelekezana kwa ajili ya kuwekana sawa baada ya kipindi hiki kupita. Valentine ipo kila mwaka, hivyo ni vyema kupata kinga kabla ya kuugua. Nafasi yangu haitoshi, wiki ijayo uje darasani tuendelee. Nani atakubali kupitwa?

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About na Who is your Valentine?, vilivyopo mitaani.

No comments: