ZIMEBAKI siku tatu tu ili ifike ile siku maalumu zaidi ulimwenguni kwa ajili ya wenzi kuoneshana namna wanavyopendana. Ni Sikukuu ya Wapendanao. Shamshamra kila kona.
Marafiki jambo kubwa ambalo nalizungumzia hapa ni namna ya kuifanya siku hiyo kuwa ya tofauti kabisa na siku nyingine au sherehe ya namna hiyo uliyowahi kuadhimisha.
Marafiki jambo kubwa ambalo nalizungumzia hapa ni namna ya kuifanya siku hiyo kuwa ya tofauti kabisa na siku nyingine au sherehe ya namna hiyo uliyowahi kuadhimisha.
Katika ubunifu, kama mtakumbuka wiki iliyopita nilisema, ni vyema kama utapata nafasi ya kuandaa hafla maalum. Katika kipengele cha kwanza wiki jana nilisema, unaanza na kuandaa hafla hiyo kichwani mwako.
Sasa twende katika vipengele vingine vilivyosalia.
FANYA MAANDALIZI YA KUTOSHA
Itakuchukua muda kidogo kufanya matayarisho ya hafla hii nzuri ya kupendeza. Usifanye mambo kwa kukurupuka.
Kwa kawaida, si hafla kubwa sana yenye gharama ya kutisha, kwa hiyo unaweza kujiandaa mapema kwa fedha na mambo mengine ambayo nitayaeleza hapa chini, halafu usubiri wiki moja kabla ndipo ukamilishe mambo muhimu kwa ajili ya siku hiyo.
AINA YA HAFLA/WAALIKWA
Wakati ukiwa katika maandalizi yako, ni vizuri ukijua unataka kufanya hafla ya namna gani, nikiwa na maana ya gharama na hadhi ambayo utaimudu.
Aidha, lazima upange utakuwa na akina nani katika sherehe yako hiyo. Andaa majina ya rafiki zako (wenye wenzi tu) kwa kuzingatia bajeti.
Sherehe yenye idadi ndogo kabisa inaweza kuwa watu kumi kwa maana ya pea tano (five couples).
TUMA MIALIKO
Baada ya kuwa na idadi na majina ya watu ambao unapenda kuwa nao katika siku hiyo, watumie kadi.
Waalike mapema ili kuwapa nafasi ya kujiandaa. Wakati mwingine unaweza kutuma mwaliko wako kumbe wenzako wameshapanga kwenda mbuga za wanyama kumalizia siku yao.
Katika kadi ya mualiko, ambatanisha na motisha wa zawadi kwa wenzi (couple) watakaopendeza zaidi. Hii itawafanya wote kujiandaa na kuja nadhifu kwa kila mmoja kutamani kuibuka na ushindi kwa kuvaa vizuri.
CHAGUA CHAKULA/LIPA
Chagua aina ya chakula unachoona kinafaa, kisha weka oda na lipa sehemu ya fedha au yote ili kuepuka usumbufu.
Katika upande huu wa chakula, suala la kugawa majukumu kwa watu wako wa karibu kushughulikia ni zuri, kwani litaifanya sherehe yako kuwa nzuri na isiyolalamikiwa.
Huduma zitakwenda haraka na wageni watajisikia sehemu ya familia yako. Epuka kabisa kuwafanya wajisikie vibaya na kuanza kujilaumu kuwa bora wangeendelea na sherehe wakiwa peke yao kuliko mjumuiko huo ambao umepunguza matarajio yao.
BURUDANI
Kumbuka hafla yako ni ya kimahaba, hivyo basi ni vyema ukaandaa burudani zinazofanana na sherehe yako. Andaa muziki laini wenye mashairi ya mahaba.
Zipo nyingi, za lugha mbalimbali, changanya au zingatia matakwa au uelewa wa wageni wako, maana wewe ndiye unayewajua vizuri zaidi.
Unaweza kuandaa pia Chemsha Bongo ya kuuliza maswali ya kimapenzi. Aina ya muziki iliyopendekezwa zaidi ni pamoja na Soul, Bluase, RnB, Jazz, Rock, Country na nyingine nyingi.
MAPAMBO
Ukumbi au eneo lako la hafla lazima liwe la kimahaba. Pamba kwa kutumia vitu vilivyotengenezwa kwa alama ya kopa inayoashiria mapenzi.
Tumia rangi za aina mbalimbali, rangi maalumu kwa siku hiyo ni pamoja na nyekundu, pinki na nyeupe. Rangi za nyongeza ni pamoja na damu ya mzee, maziwa, hudhurungi na udongo.
SASA FURAHIA
Baada ya matayarisho yote hayo, unaweza kuifurahia siku yako vyema. Fika ukumbini kukiwa tayari kumeandaliwa vyote hivyo, halafu muoneshe mwenzi wako jinsi unavyompenda.
Kila mmoja ndani ya ukumbi au eneo ulilochagua, apewe nafasi ya kuzungumzia historia ya uhusiano wao, changamoto na namna wanavyomaliza migogoro yao.
Kwa kiasi kikubwa, wewe na mwenzako mtajifunza vitu vipya, lakini pia hata rafiki zako, watakuona mtu muhimu kwao kwa kuwaalika kwenye hafla nzuri ambayo haitasahaulika katika maisha yao.
Jambo kubwa zaidi, ni kwamba utakuwa umeingiza uhusiano wenu kwenye historia za uhusiano mwingine, lakini kubwa huimarisha na kuondoa mawazo ya kuachana, kwani kila mhusika anapofikiria juu ya jambo hilo, nafsi yake humsuta mara baada ya kukumbuka hafla ilivyokuwa.
Happy Valentine’s Day!
Joseph Shaluwa ni Mtalaam wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Lets Talk About Love na Who is your Valentine? ambacho ni maalum kwa siku ya wapendanao.
No comments:
Post a Comment