Patricia Kimelemeta
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) imebaini utata wa matumizi ya zaidi ya Sh25 bilioni katika Wizara ya Maliasili na Utalii, huku watendaji wa wizara hiyo wakikosa takwimu za idadi ya wanyamapori na vitalu vya uwindaji.
Kashfa hiyo imezidi kuitikisa wizara hiyo kwani hivi karibuni ilikumbwa na kashfa nyingine ya utoroshaji nje twiga wakiwa hai, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Jana, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo alisema fedha hizo zinatokana na mapato kutoka vyanzo mbalimbali vya wizara hiyo.
PAC kwa muda wa wiki nzima imekuwa ikipokea taarifa za wizara mbalimbali za Serikali, ikiwamo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambako iliibua ukata katika balozi za Tanzania nje na juzi, ilikutana na watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu na kubaini utata wa matumizi ya Sh1.5 bilioni za mafuriko ya Kilosa.
Cheyo alisema kamati yake katika Wizara ya Maliasili na Utalii pia ilibaini watendaji wa wizara hiyo kutokuwa na takwimu za wanyama, vitalu vya uwindaji, takwimu za watalii wanaoingia na kutoka pamoja na rasilimali mbalimbali zinazoweza kuiingizia nchi mapato, jambo ambalo limesababisha kupata hati chafu kwa miaka mitatu mfululizo.
“Nashindwa kujua mnafanyaje kazi wakati hamna hata takwimu za wanyama wala watalii wanaoingia nchini, jambo hili linaisababishia Serikali kushindwa kuingiza mapato na kuweka mianya ya wizi, kutokana na hali hiyo mnapaswa kubadilika na kufanya kazi zenu kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na nchi,”alisema na kuongeza.
“Kutokana na ripoti iliyowasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imebaini kuwa zaidi ya Sh25 bilioni zimetumika kinyume na taratibu katika kipindi cha mwaka jana, na kwamba matumizi hayo hayako kwenye vitabu vya Serikali wala hazina,” alisema Cheyo.
Alisema hilo ni kosa kwani watendaji walipaswa kuwasilisha fedha hizo hazina ikiwa ni pamoja na kuandika mchanganuo wa matumizi ili taarifa zake ziwekwe kwenye vitabu vya Serikali.
Lakini, Cheyo alisema kilichofanyika ni kuchukua uamuzi mkononi wakati wakijua kuwa wanachokifanya ni kinyume na sheria.
“Huwezi kuchukua fedha za Serikali bila ya kutoa maelezo, fedha zinazoingia kwenye wizara zinapaswa kuwasilishwa hazina ili ziweze kuhakikiwa ndipo ziweze kurudishwa kwenye wizara husika kwa ajili ya matumizi husika. Lakini, kilichofanyika wizara hii ni kuchukua mgawo wao mapema huku wakijua wanachokifanya ni kosa,”alibainisha.
Alisema kutokana na hali hiyo, mapato ya wizara hiyo yamekuwa yakishuka kila mwaka kutokana na watendaji wake kutokuwa makini, hali ambayo inaonyesha wazi kuwa, wanashindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Kwa mujibu wa Cheyo, makadirio ya ukusanyaji wa mapato ya wizara hiyo kwa mwaka 2010 yalikuwa ni Sh1.7trilioni, lakini walikusanya Sh79bilioni, mwaka 2011 mapato yalishuka na kufikia 52bilioni na sasa hawana hata shilingi.
Alisema idadi ya watalii wanaoingia nchini ni kubwa, lakini fedha zinazowasilishwa serikalini ni ndogo ambazo hazilingani na idadi hiyo, hali ambayo inaonyesha wazi fedha hizo zinapotea kinyume na taratibu.
Alisema idadi ya watalii wanaolala kwenye hoteli za hapa nchini ni kubwa, lakini fedha zinazowasilishwa serikalini ni ndogo na hazilingani na idadi hiyo ya watalii, jambo ambalo linaonyesha wazi kuna wajanja wanatumia nafasi hiyo kuiba mapato ya Serikali.
Cheyo aliongeza kwamba wizara hiyo ni nyeti kwa ajili ya kuongeza mapato ya Serikali, lakini watendaji wake wanashindwa kuwajibika ipasavyo jambo ambalo limesabababisha fedha nyingi kutumika kinyume na utaratibu.
Alifafanua kwamba kutokana na hali hiyo, watendaji hao wa wizara wanapaswa kuweka mifumo ya uwazi ya ukusanyaji wa mapato ili kila mtu aweze kubaini kiasi kilichoingia, kilichotoka na matumizi yake na si kuweka usiri ambao unasababisha mianya ya wizi.
Kamati hiyo imewaagiza watendaji hao kukaa na hazina ili waweze kuhakiki mapato na kuwasilisha taarifa hizo kwenye vitabu ya Serikali.
Mbali na hilo, pia PAC imewataka watendaji wa wizara hiyo kuweka utaratibu wa kuwataka watalii wanaoingia nchini kulipa fedha za Kitanzania na si kutumia fedha za kigeni kama ilivyo sasa.
Kauli ya Katibu Mkuu
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maimuna Tarishi alikiri kuwepo kwa wafanyabiashara wajanja wa hoteli wanaokwepa kulipa kodi na kusababisha wizara hiyo kukusanya kiasi kidogo cha fedha kila mwaka.
“Ni kweli, kuna baadhi ya wafanyabiashara wa hoteli kuwa wajanja na kushindwa kodi stahiki, lakini sasa hivi tunabadili mfumo na kuwepo mfumo wa kielectronic ili tuweze kujua idadi ya watalii walioingia nchini,”alisema Tarishi.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment