ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 27, 2012

Waziri Chami: Sijuzulu ng'o

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami amesema wizara yake haiwezi kuzuia uchunguzi wowote wa kashfa ya ufisadi ndani ya wizara hiyo, lakini, akaweka msimamo wake kwamba kamwe hataachia ngazi kutokana na kashfa inayokabili Shirika la Viwango Tanzania (TBS).Shinikizo la kumtaka Dk Chami asimamishwe kazi au ajiuzulu kupisha uchunguzi wa kashfa hiyo ya TBS limezidi kuongezeka katika siku za karibuni baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika la ya Umma (POAC), kulipeleka suala hilo mikononi mwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Akizungumzia shinikizo hilo la kumtaka aachie ngazi au  asimamishwe, Dk Chami alisema madai hayo yanayotokana kashfa TBS kutoa taarifa tata za ukaguzi wa magari kwa makampuni hewa mwaka 2007, hayana msingi kwani wakati huo hakuwa kwenye wizara hiyo.

Dk Chami alisema wakati zabuni hiyo ikitolewa alikuwa hajateuliwa kushika wadhifa huo na alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa.

Alijitetea pia kwamba kazi ya utoaji zabuni iko ndani ya mamlaka ya utendaji wa TBS na haiko chini ya wizara hiyo moja kwa moja, ingawa jambo hilo halizuii wizara yake kumchukulia hatua Mkurugenzi wa TBS, Charles Ekelege, lakini itafanya hivyo kwa kuzingatia sheria na taratibu. 

“Wizara ya Viwanda na Biashara haimlindi na haitamlinda mtu yeyote asichunguzwe pale tuhuma zinapotolewa dhidi yake. Hata hivyo, ninachoomba ni kwamba lazima kuwe na utaratibu wa kumchunguza au kumsimamisha kiongozi,” alisema Dk Chami na kuongeza:

“Utaratibu ukifuatwa na akatokea mtu akazuia uchunguzi huo, hapo ndipo mhusika anapaswa kuchukuliwa hatua.”

Dk Chami alisema shinikizo la kumtaka aachie ngazi kutokana na kampuni zisizo na uwezo kupewa zabuni hiyo na TBS mwaka 2007 ni kumwonea na kutomtendea haki.

Dk Chami alisema hivi sasa wizara yake inasubiri mawasiliano kutoka Ofisi ya Spika juu ya tuhuma zilizoibuliwa kuhusu Mkurugenzi Mtendaji wa TBS na kuahidi kwamba hawatachelewa kuchukua hatua stahiki, watakapopewa tuhuma hizo kwa maandishi.

“Sasa leo ukiniambia Waziri niitishe bodi kwa ajili ya Ekelege, nitaionyesha kitu gani? Sina maandishi yoyote yanayonipa nguvu ya kuiita bodi na kuiambia kuna hili na hili kumhusu Mkurugenzi huyu!” alisema Dk Chami.

Waziri huyo alisema pamoja na uchunguzi utakaofanyika kutokana na taarifa watakazopokea kutoka Ofisi ya Spika, wizara yake nayo inaendelea kuchunguza tuhuma hizo kupitia vyombo vya uchunguzi vya dola kwa lengo la kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mhusika. 

Sakata la TBS
Agosti 16 mwaka jana, wajumbe wanne wa POAC, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Deo Filikunjombe walitembelea Hong Kong na Singapore kuthibitisha uwezo wa wakala walioshinda zabuni ya TBS kuhusu ukaguzi wa magari kama wanakidhi vigezo ikiwemo kuwa na ofisi, wafanyakazi na vifaa kwa kazi hiyo.

Ziara hiyo ya wajumbe wa POAC ililenga kuangalia uwezo wa wakala hao walioteuliwa na TBS ambayo iko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.  

Kampuni sita zilishinda zabuni hiyo ambazo zote zilipewa leseni ya kufanya kazi tangu mwaka 2007, lakini tangu kipindi hicho kampuni hizo (majina tunayo) zimekuwa hazina ofisi licha ya kuingia mkataba wa TBS ambayo hutoza fedha za gharama za ukaguzi wa viwango kwa waagizaji magari nje.

Hata hivyo, wabunge hao walipofika huko, walipokewa na Ekelege na ofisa mwingine wa shirika hilo na katika mazingira ya kutatanisha, hawakukuta vifaa wala ofisi.

Baada ya ujumbe huo wa POAC kurejea nchini, ulimuweka kiti moto Ekelege na wenzake huku ukimtaka achukuliwe hatua.


Mwananchi

No comments: