ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 16, 2012

Zamalek yaficha nyota wake

Licha ya kwamba timu ya soka ya Zamalek inatarajiwa kuwasili nchini kesho alfajiri, uongozi wa mabingwa hao mara tano wa Afrika umeficha majina ya nyota wake watakaoivaa Yanga Jumamosi kwenye mechi yao ya kwanza wa ligi ya klabu bingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mpaka kufikia jana, Zamalek ilikuwa imetuma taarifa za ujio wake lakini hawakutuma majina ya nyota wake kwa shirikisho la soka nchini (TFF).
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, kikosi cha timu hiyo kitawasili nchini kesho alfajiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri (Egypt Airways).
"Bado hatujajua majina ya wachezaji watakaokuja lakini ila wametutumia taarifa ya safari yao ambapo watawasili nchini Ijumaa (kesho) alfajiri kwa ajili ya mchezo huo," alisema Wambura.
Naye katibu mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa alisema kuwa hawana taarifa ya majina ya wachezaji wa Zamalek watakaokuja nchini Ijumaa.

Katika hatua nyingine uongozi wa Yanga pamoja na kampuni iliyopewa jukumu la kuutangaza mchezo huo wa Zamalek na Yanga, jana ulitangaza viingilio vya mechi hiyo itakayochezwa keshokutwa kwenye uwanja wa taifa ambapo kiingilio cha chini kimepangwa kuwa Sh. 3,000.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwesigwa alisema kuwa viingilio hivyo vimewekwa kwa ajili ya kuwawezesha mashabiki wengi wa klabu hiyo ambao wengependa kuingia uwanjani kuishangilia timu yao.
Mwesigwa alisema kuwa kiingilio cha chini kitakuwa Sh. 3,000 kwa ajili ya jukwaa la viti vya rangi ya kijani huku viingilio vingine vikipangwa kuwa Sh. 7,000 kwa jukwaa lenye viti vya rangi ya bluu wakati jukwaa la viti vya rangi ya machungwa kiingilio chake kikipangwa kuwa Sh. 10,000.
"Mbali na viingilio hivyo pia, kwa upande wa jukwaa la VIP viingilio vimegawanywa kwenye makundi matatu na hii yote ni kwa ajili ya kuwezesha mashabiki wengi kujitokeza kenye mchezo huu," alisema Mwesigwa.
Alivitaja viingilio vya VIP kuwa ni Sh 15,000, VIP B (Sh. 30,000) wakati jukwaa la VIP A kiingilio chake kitakuwa Sh. 50,000 ambacho ndicho kiingilio cha juu zaidi kwenye mchezo huo.
Aidha, ilivitaja vituo viitakavyotumika kuuzia tiketi kuanzia kesho kwa ajili ya mchezo huo wa Jumamosi kuwa ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Benjamini Mkapa, Mgahawa wa Steers (Posta), vituo vya mafuta vya Big Bon vya Kariakoo, Mbagala, ubungo na Tandika Mwembe Yanga pamoja na maduka ya Zizou Fashion.
Mwakilishi wa kampuni iliyopewa jukumu la kuitangaza na kuusimamia mchezo huo, Balozi Kindamba alisema tiketi hizo zitakazoanzwa kuuzwa leo zitatumika mara moja tu na zitakaguliwa kwa kutumia mtambo maalum wa kompyuta kabla ya shabiki kuingia uwanjani siku ya mchezo.
Alisema kuwa mashabiki wanunue tiketi mapema kuepusha usumbufu siku ya mchezo na kwamba watakaonunua tiketi watapewa stika maalum za kuvaa mkononi.
"Kwa kutumia teknolojia hii, hakutakuwa na tatizo la kughushi tiketi, na pia tiketi itatumika mara moja tu na teknolojia hii itabaini tiketi ambayo imeshatumika... pia wakati mchezo ukiendelea tutajua idadi ya mashabiki walioingia uwanjani mpaka muda huo," alisema Kindamba.
Alisema mashabiki watakaojitokeza mapema uwanjani watapata burudani kutoka kwa wanamuziki nyota nchini ambao watatoa burudani kwa mashabiki kabla ya kuanza kwa mchezo huo.
Katika hatua nyingine, Mwesigwa alisema kuwa timu hiyo ipo kwenye maandalizi ya mwisho kwa ajili ya mchezo huo ambapo wachezaji wapo katika ari nzuri isipokuwa wachezaji Salum Telela na Nurdin Bakari wataukosa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.
Hata hivyo, taarifa hiyo ya Mwesigwa inatofautiana na taarifa aliyoitoa kocha wa timu hiyo Kostadian Papic ambaye alisema kuwa wachezaji watano akiwemo kipa Mghana Yaw Berko wanaweza wakaukosa mchezo huo wa Jumamosi kutokana na kuwa majeruhi.
Wachezaji aliowataja Papic mbali na Berko, Nurdin na Telela pia wamo Shadrack Nsajigwa na kiungo Rashid Gumbo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: