ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 29, 2012

Zitto, Makamba wautaka urais

  Waanza kampeni ya kupunguza umri wa urais
  Wataka sasa upunguzwe hadi miaka kufikia 35
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (kushoto), akisisitiza jambo wakati akichangia mada katika kongamano la kuelimisha vijana kuhusu Katiba lililoandaliwa na Femina Hip. Kulia ni Mbunge wa Bumbuli, January Mmakamba. (Picha na Omar Fungo)
Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba, ameshauri katiba mpya inayotarajiwa kuundwa nchini iwe na mabadiliko yatakayoupunguza sifa ya umri wa mgombea kiti cha urais toka miaka 40 ya sasa hadi kufikia miaka 35 ili kutoa nafasi kwa vijana kugombea.
Msimamo wa Makamba uliungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ambaye alikwisha kusema kwamba mwaka 2015 hatagombea tena ubunge ila atajitosa katika urais.
Makamba alisema kwa kufanya hivyo kutawawezesha vijana ambao ni zaidi ya asilimia 65 ya idadi ya Watanzania kuwa na fursa ya kugombea nafasi hiyo ya juu nchini na hatimaye kushiriki moja kwa moja kwenye maamuzi yanayohusu mustakabali wa nchi yao.


Aidha, Makamba, aliyezaliwa Januari 28, 1974 alipendekeza katiba mpya iwe na mabadiliko yatakayoruhusu sifa ya umri wa raia kupiga kura upunguzwe kutoka miaka 18 ya sasa hadi miaka 16 kwa lengo la kupanua wigo wa vijana kushiriki katika maamuzi ya kumchagua rais na wakilishi wanaowataka.
Makamba aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akishiriki kwenye warsha ya Vijana na Katiba iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Femina na kuwashirikisha vijana wa kada mbalimbali pamoja na mabalozi, wabunge, wanaharakati, maofisa wa serikali na wanafunzi.
“Pamoja na mambo mengine ya msingi, tutakayokubaliana kama taifa, ningependelea zaidi katiba ijayo iwe na mabadiliko hayo niliyoyataja hapo juu, na hili ninawaasa tulipiganie,” alisema na kuongeza:
“Wakati umefika kwa vijana kushiriki kwenye ngazi zote za maamuzi kwa ajili ya kuhakikisha mambo yanayotuhusu yanaingia kwenye mipango ya utekelezaji na si wakati wa kukaa pembeni na watu wengine kutufanyia maamuzi.”
Ingawa Makamba na Zitto hawakutaka kusema wazi wazi kwamba wanataka marekebisho hayo ya sheria yafanyike ili wajitose kwenye urais, walisema kuwa warsha ya jana haikuwa kwa ajili ya kutangaza nia ya kuwania urais, ingawa walijenga hoja ya marekebisho ya sheria ili vijana wapate fursa hiyo.
Ingawa Makamba hajatangaza kokote kuwa atawania urais mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu, kauli yake inakuwa kama mwangwi wa habari ambazo zimekuwa zikielezwa kwamba ni miongoni mwa vijana wanaotamani urais ili kuwakilisha maslahi na hisia za vijana.
Naye Zitto  akijenga hoja ya vijana kuruhusiwa kuwania urais kwa kushusha umri unaoruhusiwa kisheria kutoka miaka 40 hadi 35, alisema kuwa nchi zote za maziwa makuu, kama Uganda, Kenya, Burundi na Rwanda umri wa kuwani urais ni miaka 35 na kuhoji ni kwa nini Tanzania ni tofauti.
Kauli ya jana ya Zitto inazidi kuthibitisha nia yake ya kuwania urais ambayo alianza kuitoa mwaka 2010 wakati wa kuwania ubunge.
Akihutubia moja ya mikutano ya kampeni za uchaguzi wa ubunge wa mwaka 2010 katika jimbo lake, aliwaambia mamia ya wananchi waliokuwa wamekusanyika kumsikiliza kwamba mwaka 2015 atakaporejea tena kuwaomba kura hazitakuwa za ubunge ila ni za urais.
Zitto aliingia bungeni mara ya kwanza mwaka 2005 akiwa ni mbunge kijana kuliko wote walioingia katika chombo cha wawakilishi mwaka huo akiwa na umri wa miaka 29. Alizaliwa Septemba 24, 1976.
Kadhalika, Zitto, aliwaasa vijana kuachana na siasa za kulalamika bila ya kutoa majawabu ya matatizo wanayoyalalamikia na kwamba enzi hizo zimepitwa na wakati.
“Siasa za vijana wa sasa ni za kutoa masuluhisho ya kukabiliana na changamoto zilizopo bila ya kuangalia itikadi za kivyama, kama ambavyo tumekuwa tukifanya mimi na Makamba katika mambo ya msingi yenye maslahi kwa nchi. Ni lazima palipo na maslahi ya nchi, tusimame pamoja kwa kuwa bila ya kufanya hivyo, watu wengine watatusemea,” alisema.
Aidha aliwaasa vijana kutowaachia wanasiasa suala la katiba mpya kwa kuwa wao wanaangalia maslahi yao, badala yake wahakikishe kwamba wanashiriki kikamilifu kwenye mchakato huo kwa kutoa mawazo na mapendekezo yao ili yawe sehemu ya katiba mpya.
CHANZO: NIPASHE

No comments: