ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 27, 2012

Arumeru Mashariki ilivyobadili mfumo wa kampeni za ubunge

Image
Wanachama na wafuasi wa CCM wa Kijiji cha Mulala Jimbo la Arumeru Mashariki, wakimkaribisha kwa kumbeba mgombea ubunge wa CCM, Sioi Sumari.
WAKATI zikiwa zimebaki siku nne kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge katika 
Jimbo la Arumeru Mashariki, mbwembwe, vioja na vijembe vimeendelea kutawala kampeni hizo, mvutano mkali ukiwa baina ya mgombea wa CCM, Sioi Sumari na mgombea wa 
Chadema, Joshua Nassari. 

Vyama vingine vya UPDP, DP, SAU, AFP, TLP pia vitashiriki uchaguzi huo utakaofanyika Aprili 1, mwaka huu kwa kuhusisha kata 17 na vijiji 74 vya jimbo hilo, ambalo linapakana na Jimbo la Siha kwa upande mmoja na Jimbo la Arusha Mjini kwa upande mwingine. 

Siku nne kabla ya uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi ili kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kumchagua mwakilishi 
wao ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge, marehemu Jeremiah Sumari kufariki dunia mwanzoni mwa mwaka huu kwa ugonjwa. 


Baada ya uzinduzi, vyama vinavyopewa nafasi kubwa ya kulinyakua jimbo hilo vya CCM na 
Chadema vilianza kampeni kwa nguvu kubwa, CCM wakibadili mtindo walioutumia Igunga, kwa kutumia magari badala ya helikopta, lakini Chadema wakitumia helikopta siku ya uzinduzi, wakasitisha kabla ya kurejea tena kwenye kampeni za helikopta siku nane kabla ya uchaguzi. 

Tofauti na chaguzi nyingi, siku nne kabla ya uchaguzi, wananchi wa Arumeru Mashariki na Watanzania kwa ujumla wameshuhudia kampeni zisizo za kistaarabu kutoka pande zote mbili kwa kuwepo kwa lugha ya matusi, vitendo vya kudhalilisha, wizi wa bendera na picha za wagombea, kutekana nyara, kutishiana maisha na matukio mengine kama hayo ambayo 
yametia doa uchaguzi wenyewe. 

Pamoja na kasoro hizo lakini yapo matukio ambayo yametia chachu katika kampeni na kuzifanya kuonekana kuwa na msisimko wa aina yake na hivyo kuongeza joto kwa pande zote 
mbili. 

Mke wa Sioi, Pamela, yeye amekuwa akiwapigia magoti akinamama na vijana wa Jimbo la Arumeru Mashariki akiwaomba kumchagua mumewe, Sioi. Pamela ambaye ni mtoto wa 
aliyekuwa Waziri Mkuu , Edward Lowassa, anasema atatumia nafasi yake kama mama kumshauri ipasavyo mumewe, endapo atachuguliwa ili kuharakisha maendeleo ya Jimbo la Arumeru Mashariki. 

Kwa siku zote za kampeni, CCM imekuwa ikiwasisitiza wananchi kumchagua Sioi, kwa vile Mbunge aliyemtangulia alikuwa wa CCM na anapaswa kuchaguliwa ili kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010. 

CCM inasema Chadema kutaka mgombea wake kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, ni sawa na Padri kuombwa kwenda kuendesha swala msikitini baada ya Shehe kufariki dunia. 

Meneja wa Kampeni wa CCM kwa Jimbo la Arumeru Mashariki, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, wamekuwa wakiongoza kikosi cha kampeni za Sioi, kwa kumnadi katika kata mbalimbali. 

Wabunge hao wanawaomba wana Arumeru kumchagua Sioi, kutokana na kuwa na uwezo 
mkubwa wa kuwaletea maendeleo na pia kutoka katika chama kinachoendesha Serikali iliyopo 
madarakani. 

Wanasema pamoja na kwamba Chadema wamekuwa wakitoa maneno ya kejeli dhidi ya CCM na 
Serikali yake, lakini chama hicho kinafahamu fika kwamba ni vigumu kwa wabunge wake kuwaletea wananchi maendeleo bila msaada wa Serikali ya CCM. 

Akinadi sera za CCM, Sioi anasema kama atachaguliwa ataharakisha ujenzi wa barabara, atajenga madaraja yanayosumbua katika barabara hizo, ujenzi wa zahanati na kushughulikia 
matatizo ya ardhi. 

Katika hatua nyingine, CCM wanatoa tuhuma nzito dhidi ya Chadema, kwamba kimeanza kucheza rafu kwa kukodisha mamluki ili kufanya fujo kwenye mikutano ya CCM na pia kuwatumia vijana kuiba shahada za baba na mama zao ambao ni wanachama wa CCM ili kuwahujumu wasipige kura. 

Vyama vyote viwili vinadai kwamba chama pinzani, kimeanza kukodisha vijana, ambao wamekuwa wakifika katika mikutano yao ya kampeni na kufanya vitendo mbalimbali kama kuzomea, kutoa ishara mbaya na hata kujibizana na viongozi wanapokuwa wakielezea sera majukwaani. 

Hatua hiyo ndiyo iliyolifanya Jeshi la Polisi, kuvionya vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo na kuvitaka kuepukana na vurugu. Tamko la Jeshi la Polisi lilikuja baada ya CCM kupitia kwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Martin Shigela, kusema kuwa CCM 
ilikuwa imechoka kuvumilia vitendo vya vurugu na fujo, vinavyofanywa na wanachama wa Chadema. 

Jeshi la Polisi lilitoa onyo kwa vyama vyote vya siasa, vinavyoshiriki kwenye uchaguzi huo, kuepukana na fujo na vurugu zinazoweza kuhatarisha hali ya amani na utulivu na kutia kasoro 
mwenendo wa uchaguzi huo. 

Naibu Kamishna Msaidizi wa Polisi, Isaya Mngulu, ambaye ndiye mkuu wa operesheni za uchaguzi kwa Jeshi la Polisi katika Jimbo la Arumeru Mashariki, anasema tayari Jeshi hilo limepokea mashitaka ya vurugu na fujo katika mikutano ya kampeni. 

Anayataja matukio hayo kuwa yanahusiana na uchanaji wa bendera za vyama vya siasa, kuchana picha za wagombea, wizi wa bendera na picha za wagombea, na lugha za matusi zinazowadhalilisha wagombea na viongozi wa vyama hivyo. 

“Wanaacha kunadi sera wanaingilia mambo ya ajabu mara huyu ukoo wao hivi mara huyu si raia. Haya mambo hayana manufaa kwa wananchi ambao lengo lao ni kutaka kusikia sera zitakazowaletea maendeleo,” anasema Mngulu. 

Polisi wanasema matamshi yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa, ya kuwataka wananchi wa Arumeru Mashariki, kujichukulia hatua mikononi kama hawaridhishwi na hatua zinazochukuliwa na Polisi ni kauli ya uchochezi inayoweza kuhatarisha amani na utulivu. 

Anasema tayari mashitaka hayo yamewasilishwa kwa Kamati ya Maadili iliyo chini ya Msimamizi wa Uchaguzi ili kuyafanyia kazi. 

Nassari anasema anafaa zaidi kuwa Mbunge, kwa vile anao uwezo mkubwa wa kutatua kero za wananchi, hasa upatikanaji wa maji safi na salama, uboreshaji wa huduma za afya, upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya mashamba, na pia kuboresha barabara zinazounganisha vijiji vya jimbo hilo. 

Anawataka wananchi kutupilia mbali vijembe vinavyoelekezwa kwake, kwamba hafai kuwa Mbunge kwa vile hana mke. Anasema hoja hiyo haina msingi, kwa vile wapo wabunge wengi wa Chadema ambao hawajaoa, lakini wamekuwa wakiyaongoza majimbo yao kwa mafanikio makubwa kuliko wabunge wenye wake.


Habari Leo

No comments: