ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 13, 2012

Bingwa Ligi Kuu patamu

 
Azam FC

MBIO za ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara mpaka kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita, zimeonekana kupamba moto kwa timu za Simba, Azam na Yanga. 

Vinara wa ligi hiyo kwa kipindi kirefu Simba ilishindwa kuongeza pengo la pointi na kujiweka katika mazingira mazuri zaidi ya kutwaa taji hilo ililolichukua msimu wa mwaka 2009/10, baada ya juzi kutoka 0-0 na Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Taifa , Dar es Salaam. 


Kabla ya mchezo huo Simba ilikuwa ina pointi 40 kwenye michezo 18 iliyocheza baada ya kuifunga Kagera Sugar mabao 3-1 katikati ya wiki iliyopita, hivyo kama ingeshinda dhidi ya Toto Africans ingefikisha pointi 43 katika michezo 19 iliyocheza pointi mbili zaidi ya timu inayoshika nafasi ya pili ya Azam yenye pointi 41. 

Lakini Simba ingekuwa na faida kubwa zaidi kwani yenyewe imezidiwa mchezo mmoja na Azam, hivyo kama Simba ingeshinda michezo yake yote ingekuwa inaipita Azam pointi tano. 

Hata hivyo kutokana na matokeo yake na Toto Africans kwa namna moja au nyingine ni faraja kwa Yanga inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 37 katika michezo 18 iliyocheza baada ya kufungwa mabao 3-1 na Azam, ikiwa nyuma kwa mchezo mmoja dhidi ya Simba inayoongoza ligi na michezo miwili nyuma ya Azam yenye pointi 41 sawa na Simba. 

Kama Yanga itashinda kiporo chake kimoja, itakuwa na pointi 40 ikifungana michezo na Simba iliyocheza michezo 19, lakini ikizidiwa pointi moja na kama ikishinda mchezo wake mwingine itafikisha pointi 43, hivyo kuipita Azam pointi mbili na wote watakuwa michezo sawa. 

Kwa hesabu rahisi mbio za ubingwa bado ziko kwa miamba ya soka nchini yaani Simba na Yanga ikiwa timu hizo zitashinda mechi zake zote zilizobakia, huku mechi ya mwisho kati ya miamba hiyo ndiyo itaamua nani bingwa wa Ligi Kuu soka ya Tanzania Bara kwa msimu wa mwaka 2011/12, kwani mpaka mchezo huo utakapofikia Simba itakuwa imeizidi Yanga pointi moja kama zitakuwa zikishinda michezo yao. 

Azam yenyewe itakachokifanya sasa ili kutwaa ubingwa ni kuombea kuteleza kwa miamba hiyo, kinyume chake hata nafasi ya pili inaweza kuwa ngumu kwa timu hiyo, ambayo mbali na kuwania ubingwa itakuwa ikiwania kuiwakilisha nchi kwa mara ya kwanza kwenye moja ya michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka la Afrika (Caf). 

Kama Yanga na Simba zitashinda mechi zake zitakazozifanya timu hizo kufikisha idadi sawa ya michezo na Azam, itakuwa ikizidiwa pointi tatu na Simba na pointi mbili na Yanga. 

Yanga na Simba zimebakiza mechi zao na timu zilizo kwenye hatari ya kushuka daraja kulingana na ligi inavyokwenda, ambapo Yanga bado haijacheza na Villa Squad, haijacheza na Polisi Dodoma haijacheza na African Lyon, lakini pia haijacheza na Coastal Union ya Tanga. 

Huku Simba nayo ikiwa haijacheza na Polisi Dodoma, African Lyon na Moro United ambazo kimsingi kwa jinsi ligi inavyokwenda timu hizo zote ziko kwenye hatari ya kushuka daraja hivyo hakutakuwa na mechi rahisi kwa Simba na Yanga. 

Zikiteleza Azam itaweza kuchukua ubingwa. Simba ilifungwa bao 1-0 na Villa Squad na ikatoka suluhu na Toto African, pamoja na timu hizo kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja, kiasi cha wengi kuziona chovu.. 

Pia Yanga inaweza kufungwa na Villa Squad au timu nyingine ambayo iko kwenye hatari ya kushuka daraja kwa vile soka si mchezo unaoweza kuutabiri. 

Pia Azam nayo inaweza kujikuta ikipoteza mchezo na timu hizo zilizo kwenye hatari ya kushuka daraja. Hivyo mbio za ubingwa bado kali kwa Simba, Yanga na Azam.


Habari Leo

No comments: