ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 16, 2012

Chenji ya Rada yarejeshwa rasmi

 
ILE chenji ya rada, zaidi ya Sh bilioni 75 sasa imeiva na wakati wowote itakuwa mikononi mwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) baada ya Hati Maalumu ya Makubaliano (MoU) baina ya pande zinazohusika kusainiwa. 

Hati hiyo ilisainiwa jana kati ya Serikali ya Tanzania, Kampuni ya Uuzaji wa Silaha ya Uingereza (BAE System), Ofisi ya Uingereza ya Kupambana na Ufisadi (SFO) na Idara ya Kimataifa ya Misaada ya Maendeleo (DFID). 


Taarifa iliyolifikia gazeti hili jana ilieleza kuwa fedha hizo na riba yake, zitatumika kwenye elimu kwa mujibu wa makubaliano baina ya Serikali za Tanzania na Uingereza, na matumizi hayo yatafuatiliwa kwa makini ili zitumike kama ilivyokusudiwa. 

Aidha, ilielezwa kuwa hati hiyo ilisainiwa ili kutekeleza makubaliano baina ya BAE Systems na SFO. 

Matumizi ya fedha hizo yatahusisha ununuzi wa vitabu kwa shule za msingi zote 16,000 nchini ambapo watoto takriban milioni 8.3 watanufaika na vitabu hivyo vitakavyokuwa vya masomo yote 11 ya kuanzia darasa la kwanza hadi la saba. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kipaumbele cha vitabu hivyo kitawekwa katika masomo ya Kiswahili, Kiingereza, Hisabati na Sayansi kwa uwiano wa kitabu kimoja wanafunzi wawili. 

Taarifa hiyo ilieleza kuwa idadi ya vitabu vingine inafanyiwa kazi kwa misingi ya utaratibu wa ununuzi. Hata hivyo hati hiyo haitawekwa wazi mpaka kukamilika kwa ununuzi Mei. 

“Kuwa na vitabu pekee hakutainua kiwango cha elimu, hivyo fedha hizi pia zitatumika kugharamia vifaa vya kufundishia kwa walimu 175,000 wa shule za msingi, kuandaa mitaala na miongozo ya kufundishia na kusaidia kuongeza uwezo wa walimu katika kufundisha,” ilieleza taarifa hiyo. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, takriban Sh bilioni 13 zitatumika kununulia madawati kwa wanafunzi wa shule za msingi katika wilaya tisa ambazo zina mahitaji makubwa. 

Uwepo wa vifaa hivyo utasaidia juhudi za Serikali ya Tanzania kwenye kipaumbele cha kuinua kiwango cha elimu kwa shule za msingi. 

Pia ilielezwa kuwa ufuatiliaji na uhakiki wa matumizi ya fedha hizo utakuwa huru na utafanywa kwa niaba ya pande zote nne zilizoingia makubaliano hayo ili kuhakikisha fedha hizo zinawafikia na kuwanufaisha Watanzania. 

Fedha za rada zilizorudishwa nchini zilitokana na ufisadi uliofanyika katika mchakato wa ununuzi wa rada wakati wa Utawala wa Awamu ya Tatu ambapo Serikali ilinunua rada iliyotumika kwa fedha zaidi ya bei ya kawaida.


Habari Leo

No comments: