
Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi wa CUF kumvua uanachama Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, na wenzake, yalikuwa ni mepesi kwa sababu chama hicho kimekwishafanya maamuzi magumu zaidi kuliko hilo.
Alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akifungua kikao cha siku mbili cha kawaida cha Baraza Kuu la Uongozi la CUF Taifa, jijini Dar es Salaam.
“Hili lilikuwa jepesi kulinganisha na maamuzi magumu ambayo tuliyafanya mwaka 2001 wakati Katibu Mkuu alipokuwa nje ya nchi. Maamuzi ya kufanya maandamano ya kudai katiba mpya, kudai tume huru ya uchaguzi, kudai utawala bora na uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2000 urejewe,” alisema na kuongeza: “Yalifanywa chini ya uongozi wangu wakati Katibu Mkuu hakuwapo.”
Alisema maandamano hayo ya mwaka 2001, pamoja na kuwapoteza wahanga wa demokrasia, ndiyo yaliyoanza kujenga misingi mpaka hatimaye wakaweza kufikia maridhiano ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamisi, alisema CUF imejipanga kuhakikisha inawashinda maadui wa chama hicho.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alimhakikishia Profesa Lipumba kuwa CUF iko imara na kwamba bado iko ngangari kinoma kama alivyoiacha kabla ya kuondoka nchini au zaidi ya hapo.
Hata hivyo, Maalim Seif alisema changamoto inayoikabili CUF hivi sasa, ni kuendeleza moto uliowashwa ili wafike mwaka 2015 katika joto lile lile ambalo hivi karibuni lilianzishwa na ujio wa Profesa Lipumba kutoka nje ya nchi.
Mapema, Profesa Lipumba alisema CUF inazingatia na kutetea maslahi ya wanyonge, na kwamba itaendelea kufanya hivyo bila kujali maslahi ya mtu binafsi.
Profesa Lipumba alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi, ikiwamo ardhi yenye rutuba, madini, gesi asilia, bandari na jiografia yake kwa ujumla ambavyo alisema iwapo vitatumika vizuri, wananchi wanaweza kunufaika na kupunguza tatizo la umaskini linalowakabili.
Alikemea siasa za udini ambazo alisema hazina mustakbali mwema katika kuwaunganisha Watanzania na kuwaletea maendeleo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake