ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 22, 2012

Mbunge, makada mbaroni

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa 
Jeshi la Polisi limemkamata na kumhoji kwa muda Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, kwa tuhuma kwamba alihusika kwenye tukio la kuzuia msafara wa mgombea ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sioi Sumari, lililotokea Machi 18, ambapo pia gari moja lilivunjwa vioo.

Kadhalika, jeshi hilo limewashikilia na kuwahoji vigogo wawili wa CCM ambao ni Allan Kingazi ambaye ni Katibu wa chama hicho wilaya ya Moshi Vijijini pamoja na Ndengaso Ndekubali wa Manyara, kwa tuhuma za kumteka, kumpiga na kumjeruhi Mwenyekiti wa Chadema tawi la Magadrisho, Nuru Maeda.


Akizungumzia kukamatwa kwake, Mchungaji Msigwa, alisema ameshangaa kuhojiwa na polisi na kutakiwa kuandika maelezo ya awali kwa kosa ambalo hakulifanya.
“Mimi sikuwa eneo la tukio, lakini baada ya kusikia kuna jambo ambalo si zuri linaendelea Maji ya Chai nilikwenda na nikawatuliza watu wangu,” alisema.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Isaya Mngulu, alithibitisha kukamatwa na kuhojiwa kwa watu hao na kueleza kwamba wote wapo nje kwa dhamana huku uchunguzi wa matukio hayo ukiendelea.
Alisema jeshi hilo halitamvumilia mtu yeyote atakayekiuka sheria au kanuni bila kujali cheo chake au nafasi yake katika jamii.
POLISI: WANASIASA WASITUSHINIKIZE
Kamishna Mngulu alimwonya Dk. Willibrod Slaa pamoja na Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM), Martin Shigela, akieleza kwamba Jeshi la Polisi halitafanya kazi kwa maelekezo ya wanasiasa.
“Hatufanyi kazi kilelemama, Polisi tunafanya kazi kitaaluma, kama wameona hatufanyi hivyo waache siasa waende chuo wakasome ili wawe mapolisi, hatutafanya kazi kwa kuelekezwa na wanasiasa,” alisema.
Mngulu alitoa onyo hilo baada ya Dk. Slaa kutahadharisha kwamba kama vyombo vya dola pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) vitaibeba CCM, atahamasisha maandamano makubwa kutoka Arumeru kuelekea Ikulu Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine, Mngulu, amemwonya Shigela baada ya kueleza kwamba vijana wa CCM hawatavumilia wafuasi wa Chadema kuzuia msafara wa mgombea wao na kwamba atawahamasisha wangie msituni kama tukio hilo litatokea tena.
Alisema jeshi hilo limejipanga kikamilifu kukabiliana na wanasiasa wowote watakaotoa lugha za kichochezi na kuonya kwamba halitasita kumchukulia hatua mwanasiasa yeyote.
Alisema inashangaza kusikia Dk. Slaa akiwaeleza wananchi kuwa jeshi la polisi limekuwa likiwabambikizia wananchi kesi hali aliyosema inapandikiza chuki kwa wananchi ili walichukie jeshi hilo.
Hata hivyo, akihutubia mkutano wa hadhara katika eneo la Kiwawa, Dk. Slaa, alisema jeshi la polisi limekuwa likiwabambikia wananchi kesi hususan wafuasi wa Chadema akieleza kwamba mambo hayo yamefanyika katika chaguzi ndogo za Biharamlo, Igunga, Kiteto, Busanda na sasa Arumeru Mashariki.
Alisema jeshi hilo limekuwa likiwakamata wafuasi wa Chadema ambao wanakwenda vituo vya polisi kuripoti matukio ya kupigwa na kunyanyaswa na wafuasi wa CCM, lakini wameishia kubambikiwa kesi ambazo baada ya uchaguzi humalizika kinyemela.
“Na sisi hatuwezi kuendelea kuvumilia ukiukaji na manyanyaso haya, uvumilivu sasa ni mwisho nawaambia kabisa polisi Arumeru patachimbika na kama ni kupiga mabomu au kukamata watu wa Chadema anzeni kunikamata mimi,” alisema.




VITUO VYA KUPIGIA KURA UTATA




Yameibuka madai ya mbinu chafu za kutengeneza vituo hewa 55 vya kupigia kura katika Jimbo la Arumeru Mashariki, zinazodaiwa kufanywa na CCM kwa kushirikiana na Nec.
Dk. Slaa alitoa madai hayo kwenye mkutano wa hadhara jana uliofanyika katika Kata ya Maji ya Chai, kijiji cha Kiwawa akiituhumu Nec kwamba inashirikiana na CCM kutengeneza vituo hivyo.
Alisema vituo halali vya kupigia kura ni 327, lakini taarifa walizopata zinaonyesha kwamba idadi hiyo imeongezwa kinyemela hadi kufikia vituo 382, jambo linalokitia wasiwasi chama hicho kwamba NEC inataka kupanga matokeo kwenye uchaguzi huo.
“Kama ni kweli vituo vimeongezwa kinyemela hatutakubali, tumechoka kuchakachuliwa safari hii patachimbika mpaka kieleweke,” alisema.
Dk. Slaa alisema kitendo hicho kinaweza kuhatarisha amani kwa kuwa wafuasi wa chama hicho hawatavumilia wizi wa kura kupitia vituo hivyo huku ukisimamiwa na Nec na vyombo vya dola.
Hata hivyo, alisema chama hicho kinaendelea kufuatilia taarifa hizo na watakapojiridhisha watatoa taarifa kamili na mikakati ya kuhakikisha hawanyang'anywi ushindi kupitia vituo hewa.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Trasias Kagenzi, alisema suala la kugawanya vituo litaweza kufanyika baadaye kulingana na mahitaji kwa kulinganisha idadi ya wapigakura iliyoandikishwa.
“Vituo vinapokuwa na idadi kubwa ya wapigakura huwa tuna sub-divide (gawanya) yaani kwa vile vyenye wapigakura zaidi ya 500 ili kupunguza msongamano wa watu, ni jambo la kawaida kugawanya vituo, lakini hatutafanya hivyo bila kushirikisha vyama vya siasa,” alisema.
Kagenzi alipoulizwa ikiwa hadi sasa kuna vituo vyenye idadi ya wapigakura zaidi ya 500 ambavyo vitagawanywa alisema: “Ni vigumu kwa idadi ya watu kuwa kubwa kwa sababu wapo wapigakura waliohama au kufariki, lakini kama nilivyosema kama kutakuwa na ulazima wa kugawanya vituo tutafanya hivyo baadaye na tutashirikisha vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huu.”
WAZIRI MWANRI: AMNADI SIOI
Mbunge wa Jimbo Siha na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa, Aggrey Mwanri, amewataka wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki kumchagua Sioi ili asaidiane naye kutatua kero mbalimbali za maendeleo katika jimbo hilo.
Aliwaambia wananchi waliojitokeza kusikiliza mkutano katika kata ya Kiongori kuwa, ikiwa watamchagua mgombea huyo, atamsaidia kusukuma mikakati yake ya kuboresha barabara, upatikanaji wa maji na nishati ya umeme.
“Ndugu zangu mimi ni Naibu Waziri wa wizara inayoshughuilika na halmashauri zote, mipango yote ya maendeleo lazima ipitie katika ofisi yangu nipeni Sioi tusaidiane naye katika harakati za maendeleo,” alisema. 
 “Mchagueni Sioi msifanye masihara ndugu zangu, ndiye anayeweza kusikilizwa na serikali na si chama kingine,” alisema Mwanri.
Aliwataka wananchi hao kujifunza kwa yanayotokea katika Jimbo la Arusha Mjini ambapo alisema kuwa hakuna kinachofanyika zaidi ya maandamano kila kukicha.
Naye Sioi aliahidi kutatua kero ya umeme inayowakabili wakazi wa kata ya Ngarenanyuki kwa kuwapatia huduma hiyo pindi watakapompa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao bungeni.
Alisema tatizo la kero ya umeme ndani katika kata yao analitambua na tayari ameshafahamu njia mbadala za kuwapatia huduma hiyo, ambapo atajitahidi kuishauri serikali iunganishe njia ya umeme utokao KIA na kuulekeza katika kata ya Ngarenanyuki.
Sioi aliyekuwa amefuatana na mkewe, Pamela, aliwaambia wakazi wa kata hiyo kwamba huduma ya umeme katika kata yao ni muhimu kwa maendeleo yao, hivyo atahakikisha anashirikiana na serikali kutatua kero hiyo.
NASSARI AJINADI
Mgombea wa Chadema, Joshua Nassari, amesema hatakwenda bungeni kulala wala kuzomea wabunge wenzake, bali kuwasilisha kero na maoni ya wananchi wa Arumeru Mashariki.
Nassari aliyasema hayo kwenye mikutano yake ya kampeni jana kwenye maeneo ya Kiwawa, Manyata, Maji ya Chai na Nkuarisango, akieleza kwamba wananchi wa Arumeru Mashariki wanapaswa kumchagua ili akapiganie haki zao ikiwemo ardhi yao iliyomilikishwa kwa walowezi na kuwaacha wananchi wakikosa mashamba.
Alisema zaidi ya hekta 16,000 za ardhi ya Arumeru imemilikishwa kwa wawekezaji ambao hawachangii vilivyo maendeleo ya Arumeru kwa kuwa wanalipa Sh. 600 ya kodi kwa hekta moja kila mwaka, fedha aliyosema ni kidogo
MDEE AMVAA LOWASSA
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, amemvaa Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, akimtaka kuacha kutumia matamanio yake ya kuwania urais mwaka 2015 kuwadanganya wananchi,  hususan kuwa anaumizwa na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini.
Akihutubia mamia ya wananchi katika mikutano ya kampeni jana, Mdee alisema Lowassa anataka kuwaghilibu Watanzania kuwa anaumizwa na tatizo la ukosefu wa ajira wakati akijua kuwa serikali ya chama chake ndio iliyotengeneza tatizo hilo.
Akiwa katika Kijiji cha Ndatu katika Kata ya Poli, Mdee aliwaambia wananchi kuwa kama Lowassa ana uchungu na vijana na nchi kwa ujumla alipaswa kushauri anayoshauri hivi sasa alipokuwa madarakani, si wakati huu anapoandamwa na tuhuma za ufisadi.
Mdee aliongeza kuwa kama kweli Lowassa ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu Februari 2008 kwa kashfa ya ufisadi wa kampuni tata ya Richmond, anaumizwa na tatizo la ajira kwa vijana na kuwa hataki nchi ilipuke, basi akishauri chama chake na serikali yake kuziba mianya yote ya ufisadi na kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wote wa ufisadi nchini ambao wametumia nafasi zao kuwaibia Watanzania na kuifilisi nchi.
“Jamani Lowassa anaanza kuwadanganya wananchi kuwa ana uchungu na tatizo la ajira kwa vijana, nataka kumwambia hivi, asitumie matamanio yake ya urais kuwadanganya watu, alikuwa serikalini muda wote huo, amekuwa ndani ya chama chake hicho kwa muda wote huo, tatizo hili
halikuanza leo, halikuchipuka kama uyoga ni mlundikano wa matatizo mengi, ikiwemo kushindwa kwa mfumo, sera na mipango ya chama kilichokomadarakani...ufisadi na mafisadi wamesababisha vijana kukosa ajira, hivyo ufisadi ndiyo tishio kubwa kabisa kwa nchi hivi sasa,” alisema.

Aliongeza kuwa “Namwambia Lowassa kabla tatizo la ajira kwa vijana halijafikia kilele cha kulipua nchi ufisadi unaofanywa na viongozi wa CCM na serikali utakuwa umeshailipua nchi hii, hivyo azungumzieufisadi kwanza,” alisema Mdee.
AFC, SAU VYALILIA MUUNGANO
Wakati huo huo, Chama cha Wakulima (AFP), ambacho hakijazindua kampeni zake rasmi, kimesema kwamba hali ya kampeni inaenda vizuri na chenyewe kinafanya kampeni za nyumba kwa nyumba.
Katibu Mkuu wa AFP, Rashid Rai, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa kwamba pamoja na maendeleo mazuri, vyama vya upinzani vinavyoshiriki kinyang'anyiro hicho vinapaswa kuungana ili kuhakikisha vinanyakua jimbo hilo.
“Sisi tupo tayari kushirikiana na wenzetu na kumpa sapoti mgombea mmoja, nasema hivi nikiwashauri wenzetu tuone haja ya kuungana ili tumsapoti mgombea mmoja mwenye nguvu...hatuna maslahi na mgombea yeyote kwa hiyo tutamuunga mkono yeyote kama ikitokea tukaungana,” alisema.
Kwa upande wake, mgombea wa chama hicho, Abdallah Mazengo, alisema ana matumaini ya kushinda kwenye uchaguzi huo kwa kuwa wananchi wameonyesha kumkubali na kuelewa sera za AFP.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kupitia wa Chama cha Sauti ya Uma (Sau), Shabani Kirita, amedai kuwa Chadema, kina uchu wa madaraka.
Alitoa madai hayo wakati wa mkutano wa kata ya Maji ya Chai wilayani Arumeru na kuongeza kuwa chama chochote kikitaka mapinduzi ni lazima kiungane na vyama vingine kupambana na kupata ushindi, lakini chama chochote kikiwa kinataka ushindi bila kushirikisha vyama vingine itakuwa vigumu kwa chama hicho kuingia bungeni. 
“Chadema ina uchu wa madaraka na ndio maana inajidai inaweza yenyewe, ingekuwa siyo uchu kwa nini isingeungana na vyama vingine vya upinzani halafu tujipange kuing’oa CCM madarakani,” akidai.
Imeandikwa na Restuta James, Cynthia Mwilolezi, Charles Ole Ngereza na Woinde Shizza, Arusha.
CHANZO: NIPASHE


No comments: