ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 19, 2012

Mwanajeshi aua wananchi watano kwa risasi

WATU watano wa kijiji cha Maguba, wilayani Ulanga mkoani Morogoro, wameuawa na wengine watatu wamejeruhiwa kwa risasi na mwanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), katika mapambano ya kujihami baada ya wananchi hao kuvamia wanajeshi. 

Kati ya waliokufa, wanne walifia eneo la tukio katika kijiji hicho katika kata ya Igawa, Malinyi na mmoja katika Hospitali ya Mahenge alikokimbizwa kwa matibabu. 

Aidha, majeruhi watatu wamelazwa hospitalini hapo kutokana na majeraha ya risasi, huku mwanajeshi huyo Koplo Paulo Laurent, aliyekuwa na bunduki aina ya SMG akilazwa pia hapo kwa majeraha yaliyotokana na mashambulizi ya wananchi. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo, alisema jana ofisini kwake mjini hapa na kuongeza kuwa mauaji hayo yalifanyika Jumamosi saa nane mchana kijijini hapo. 

Kwa mujibu wa Kamanda Chialo, kabla ya mauaji hayo wanajeshi hao wa Kitengo cha Ushauri wa Mgambo wilayani Ulanga, walikwenda katika kijiji hicho kuendesha operesheni katika eneo la Hifadhi ya Wizara ya Maliasili na Utalii. 


Alifafanua kuwa pamoja na eneo hilo kutengwa kuwa hifadhi ya wanyamapori, wananchi wamekuwa wakiingia kulima na kusababisha uharibifu wa mazingira uliochangia wanyama kukimbia na wananchi kuharibu mbuga hiyo. 

“Eneo hilo limehifadhiwa na Serikali lisifanyiwe shughuli nyingine za kibinadamu ikiwamo kilimo na ufugaji,” alisema Kamanda Chialo. Kwa mujibu wa Kamanda, siku hiyo Ofisa Mteule wa Daraja wa Pili wa JWTZ na Kiongozi wa Mgambo wa Wilaya hiyo, Job Edward (54), alikwenda eneo hilo akifuatana na Koplo Laurent akiwa na SMG tayari kuendesha operesheni hiyo. 

Alidai walipofika mbugani humo, walikuta wananchi wakiendelea na shughuli za kilimo na ufugaji ambazo haziruhusiwi na ghafla waliwavamia wanajeshi hao wakiwa na silaha za jadi. 

Kwa mujibu wa Kamanda Chialo, uvamizi huo ulisababisha Koplo Laurent kujihami baada ya kuhofia kuporwa silaha kutokana na hasira walizokuwanazo wananchi. 

Kamanda Chialo aliendelea kudai kuwa, ya kufyatua risasi angani, wananchi walimvamia na kumjeruhi kwa silaha walizokuwanazo. 

“Alipoona kundi la wananchi likileta vurugu zilizoashiria kutishiwa kunyang’anywa silaha, alifyatua risasi za moto angani kwa bahati mbaya zikajeruhi watu wanane,” alidai. Alisema kati ya watu hao, wanne walifia eneo la tukio na wa tano alifariki baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Mahenge. 

Aliwataja waliokufa kuwa ni Sanyiwa Ndaya (34), Lutaya Ndala (48), Mchambi Bujiku (28), Kulwa Luhande (48) huku aliyefia hospitalini akiitwa Shija Mshishiwa (35) wote wakazi wa kijiji hicho. 

Maiti wanne walizikwa kijijini hapo isipokuwa mmoja ambaye anasubiri ridhaa ya ndugu zake wanaoishi Tabora. 

“Kijiji hicho asilimia kubwa ya wakazi wake ni wahamiaji kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa … hivyo mwili uliobaki ni wa mhamiaji, tunasubiri idhini ya wanandugu wa Tabora,” alisema Kamanda bila kumtaja jina. 

Aliwataja waliojeruhiwa na kulazwa Mahenge kuwa ni Mkama Isonge (35), Vina Msheshiwa (30), Msheshiwa Taiya (60) wote wa kijiji cha Mabuga na Koplo Laurent. Hata hivyo, alisema hali ni shwari na Polisi inaendelea na uchunguzi baada ya kukamilisha itatoa taarifa rasmi kuhusu sakata hilo. 

Mwishoni mwa mwaka jana, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Morogoro chini ya Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera, ilitembelea eneo hilo ambalo ni la Hifadhi ya Bonde la Kilombero na Pori Tengefu lililokuwa limevamiwa na wananchi wakilima na kufuga. Baada ya kubaini uvamizi huo, Bendera aliwataka wananchi kuondoka eneo hilo mara moja na kwenda kulima maeneo ya nje ya hifadhi.


Habari Leo

1 comment:

Anonymous said...

Hii ni moto.Manslaughtering by self defence is applicable!