ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 29, 2012

Mwanajeshi kizimbani kwa mauaji raia watano

skari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ), MT 70328 Koplo Paulo Laurent (38), amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za mauaji ya watu watano, ambao ni wakazi wa kijiji cha Maguba, tarafa ya Malinyi, wilayani Ulanga, mkoa wa Morogoro.

Koplo Laurent, ambaye ni mmoja wa askari walioshiriki katika operesheni ya kuwaondoa wananchi kwenye eneo lililotengwa na Serikali kwa ajili ya hifadhi, alipandishwa kizimbani jana na kusomewa shitaka la mauaji katika Mahakama ya Hakimu wa Mkoa wa Morogoro. 
Watu hao waliouawa kwa kupigwa risasi, wanadaiwa kuwa ni wakulima na wafugaji wa kijiji cha Maguba.
Akisoma hati ya mashitaka mbele ya Hakimu Seraphine Nsana, Mwendesha Mashitaka, Inspekta wa Polisi Anganile Nsiani, alidai kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Machi 17, mwaka huu saa 8:00 mchana katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Maguba iliyopo wilayani Ulanga.


Nsiani alidai mahakamani hapo kuwa mauaji hayo yalitokea wakati mshitakiwa huyo alipokuwa kwenye operesheni ya kulinda hifadhi hiyo ili isivamiwe na watu kwa ajili ya kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo, ufugaji na uwindaji.
Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa bila halali huku akijua kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria, mshitakiwa huyo akiwa na bunduki aina ya SMG, aliwaua watu watano waliokuwa kwenye hifadhi hiyo kwa kuwapiga risasi.
Aliwataja waliouawa kuwa ni Sanyiwa Ndahya (28), Ngelembende Lukeresha (26), Kashindye Msheshiwa (35), Kulwa Luhende na Lutala Ndahya (45). 
Baada ya kusomewa shitaka hilo, mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kukosa mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi za mauaji.
Kesi hiyo ilivuta hisia za wakazi wengi wa Manispaa ya Morogoro kutokana na kufahamika kwa mshitakiwa huyo ambaye awali alikuwa akifanya kazi katika ofisi ya Mshauri wa Mgambo Wilaya ya Morogoro.
Mshitakiwa huyo alirudishwa rumande hadi Aprili 11, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena wakati upelelezi ukiwa unaendelea.
Hatua ya kumfikisha mahakamani mshtakiwa huyo imetokana na Jeshi la Polisi nchini kuunda kikosi maalumu kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo baada ya kujitokeza kwa utata wa taarifa za mauaji hayo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: