Advertisements

Thursday, March 22, 2012

Ng’humbi ambana Mnyika mahakamani

Mbunge wa Ubungo,John Mnyika
James Magai 
UTATA mkubwa umeibuka mahakamani kuhusu matokeo ya uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Ubungo baada ya kudaiwa kuwepo kwa kura 14,854, ambazo hazijulikani zilikotoka. Utata huo ulielezwa jana wakati wa kesi ya uchaguzi katika jimbo hilo iliyofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia CCM, Hawa Ng’humbi ilipokuwa ikisikilizwa. 

Katika kesi hiyo namba 107 ya mwaka 2010 inayosikilizwa na Jaji Upendo Msuya, Ng’humbi kupitia kwa wakili wake, Issa Maige anapinga ushindi wa mbunge wa sasa wa jimbo hilo, John Mnyika wa Chadema. Mnyika alitangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo kuwa mshindi wa kinyang’anyiro hicho  Novemba 2, 2010 akimzidi Ng’humbi kwa kura 16,168.  

Ng’humbi akiwa shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, aliibua utata wa kuwepo kwa kura hizo hewa akihoji mahali zilikotoka na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi mambo aliyodai kuwa yanafanya matokeo hayo yawe batili. Akiongozwa na Wakili Maige, Ng’humbi alidai kuwa katika uchaguzi huo kulikuwa na jumla ya wagombea 16 kutoka katika vyama mbalimbali vya siasa. Alidai kuwa kwa mujibu wa fomu ya matokeo yaliyotangazwa, yeye alipata jumla ya kura 50,544 na kwamba Mnyika alipata jumla ya kura 66,742 huku wagombea wengine 14 wakipata kura 15,207 kwa pamoja. 

Ng’humbi alifafanua kuwa kwa mujibu wa fomu hiyo, kura halisi zilikuwa ni 119,823, kura halali zilikuwa ni 117,639 huku kura zilizokataliwa (zilizoharibika) zikiwa ni 2,184. Lakini alidai kuwa ukijumlisha kura zake na za Mnyika wote kwa pamoja kisha zikitolewa kutoka katika kura halali zilizopigwa, zinabaki kura 353 ambazo ndizo zitagawanywa kwa wagombea wengine 14 jambo ambalo alisema si kweli.

 Huku akijulimsha, idadi ya kura za kila mgombea kati ya wale 14, Ng’humbi aliieleza Mahakama kuwa wote kwa pamoja watakuwa na jumla ya kura 15,207. “Wagombea waliobaki wana jumla ya kura 15,207 ukitoa kura 353 (ambazo wanastahili kuwa nazo kwa mujibu wa fomu hiyo) kuna kura 14,854, hizi ni hewa hazipo mahali popote na hazijulikani zilikotoka.” 

Kura 14,854 ni nyingi sana zinaathiri matokeo kwani mimi sijui kuwa za kwangu zilikuwa ni ngapi kwa sababu hazijulikani zilitoka wapi. Kuna mkanganyiko katika mchanganuo huu nah ii inatia mashaka,” alidai Ng’humbi. Akizungumzia jinsi kura hizo zilivyoathiri matokeo ya uchaguzi huo, Ng’humbi alidai kuwa inawezekana ziliongezwa kwa Mnyika na kufikisha idadi ya kura alizozipata au kura zake zimechotwa zikapelekwa kwa Mnyika au za wagombea wengine zimechotwa na kupewa Mnyika. 

Alisema dosari nyingine katika matokeo hayo ni wakati wa kuhesabu kura akisema Mnyika alipeleka kompyuta zake ndogo ambazo ndizo zilizotumiwa  na wasimamizi wa uchaguzi katika kuhesabia kura jambo ambalo alidai kuwa ni kinyume cha sheria. “Kila taasisi ina utaratibu wake, Tume ya Uchaguzi ndiyo yenye dhamana ya kuleta vifaa vya uchaguzi na kuvikagua, kompyuta za mgombea zilitumika kuhesabia kura bila kuhakikiwa. Inawezekana hizo kura hewa zilitokana na kutokuhakikiwa kwa kompyuta hizo, ndiyo maana nikasema hapa kuna kasoro na mkanganyiko maana hadi sasa hatujui nani alipata nini,” alisema.

Alisema baadhi ya fomu zilizotoka katika vituo mbalimbali zilizotumika kuhesabia matokeo zilikuwa na kasoro kwa kuwa zilikuwa hazina uwiano wa matokeo kati ya kura halisi, kura halali na kura zilizoharibika. Pia alidai kuwa ndani ya chumba cha kujumlishia matokeo kulikuwa na watu wengi wasiohusika hususan wanachama wa Chadema kinyume cha sheria. 

Alidai kuwa wakati wa kampeni, Mnyika akihutubia mkutano wake eneo la River Side, Kata ya Makuburi, Jimbo la Ubungo, Mnyika alimkashfu kwa kuwaeleza wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa wasimchague yeye Ng’humbi kwa kuwa ni fisadi na kwamba aliuza jengo la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT). Alidai kuwa tuhuma hizo zilimwathiri kwa wapiga kura kwa kupoteza imani yao kwake kwa kumuona kuwa si mwaminifu hivyo kuiomba mahakama ibatilishe na kutengua matokeo yaliyompa ushindi Mnyika, iamuru uchaguzi huo urudiwe na alipwe gharama zake za kesi. 

Pia anaiomba mahakama hiyo iamuru uitishwe uchaguzi mdogo katika jimbo hilo ambao utakuwa huru, wazi na wa haki, imzuie Mnyika kushiriki katika uchaguzi huo na kuwaamuru walalamikiwa katika kesi hiyo kulipa gharama zote za kesi. Wakati akihojiwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Justice Mulokozi kuhusu tuhuma za Mnyika juu ya kuhusika kuuza jengo la UWT kuwa ni nani anayeweza kuthibitisha ukweli au uwongo wa tuhuma hizo alijibu kuwa ni yeye mwenyewe. 

Alidai kuwa tuhuma hizo si za kweli na kumtaka Mnyika ambaye ndiye aliyemtuhumu amthibitishie tuhuma hizo. Akijibu maswali mbalimbali kutoka kwa Wakili wa Mnyika, Edson Mbogoro, Ng’humbi alidai kuwa halalamikii kuwa ni nani alishinda au hakushinda, bali ukiukwaji wa taratibu na Sheria ya Uchaguzi. Kwa upande wake, shahidi wa pili Robert Kondela alidai kuwa Septemba 11, 2010 wakati wa kampeni, alihudhuria kampeni za Mnyika, Riveside na alimsikia Mnyika akiwashawishi wananchi waliofika katika mkutano huo wasimchague Ng’humbi. 

Kondela alidai kuwa Mnyika aliwaeleza wananchi hao kuwa ni fisadi aliyeshiriki kuuza jengo la UWT na kwamba kauli zile ziliwafanya wananchi wakose imani kwa Ng’humbi kuwa si mwaminifu na kwamba inawezekana walipeleka taarifa hizo hata kwa watu wengine ambao hawakuhudhuria mkutano huo. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Jumatatu Machi 26 itakapoendelea kwa kusikilizwa mashahidi wengine wa upande wa madai.

Kesi ya Lema Wakati huohuo; shahidi wa nne upande wa utetezi katika shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi Jimbo la Arusha Mjini, Samson Mwigamba jana aliieleza Mahakama kuwa hakuwahi kumsikia Mbunge wa jimbo hilo, Godbless Lema akijinadi au kufanya kampeni kwa kutumia kauli au lugha zenye mwelekeo wala hisia za kidini, kikabila wala ukaazi.

Akihojiwa na wakili wa Serikali, Juma Masanja shahidi huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha alidai kuwa katika mikutano mitano ya kampeni aliyohudhuria hakuwahi kumsikia Lema akitoa kauli za kibaguzi, kashfa wala udahalilishaji dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Batilda Burian. Mwigamba aliieleza Mahakama mbele ya Jaji Gabriel Rwakibarila kuwa wakazi wa jimbo hilo na mkoa mzima hawachagui viongozi wao kwa kufuata wala kuzingatia dini, ukabila wala eneo analoishi mtu, bali wanazingatia uwezo na sifa. 

“Ndiyo maana mimi ni mwenyeji wa Mkoa wa Mara lakini leo hii ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha. Hata Mheshimiwa Lema ni mzaliwa na Mkoa wa Kilimanjaro lakini aligombea na kushinda ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini,” alidai Mwigamba. 

Alidai isingekuwa rahisi kwa mbunge huyo kujinadi kwa kutumia hisia na kauli zenye ubaguzi kidini na kikabila kwa sababu mikutano yake ilikuwa ikihudhuriwa na umati mkubwa wa watu kutoka dini na makabila tofauti na asingeweza kuwatofautisha imani wala makabila yao.


Mwananchi

No comments: