Usiyafanye mazungumzo yenu kuwa mahojiano. Jiweke kwenye kipengele cha mapenzi, kwa hiyo wewe siyo polisi.
Pengine majibu yake yakawa siyo ya kunyooka, unachotakiwa kufanya ni kumuelewa au pale anapokuwa anasitasita, jaribu kumuongoza kuelekea kwenye jibu ambalo litasaidia ujenzi wa uhusiano wenu.
Hasira, jazba, ukali na mikunjo ya sura yako, vinaweza kumfanya ashindwe kukupa majibu sahihi. Kutokana na woga ambao atakuwa nao baada ya kuisoma ndita iliyopo usoni mwako, si ajabu akakuongopea. Ni kosa kubwa mno kuwa na uhusiano ambao unadumishwa na uongo. Tafuta uelekeo sahihi wa penzi lako.
Wewe ni muelewa, kwa hiyo unafahamu maana ya ‘kuchati’. Hoja zako zijenge katika mtindo wa majadiliano. Zungumza na yeye azungumze. Tena apewe nafasi anayoona inastahili, asije akasema ulimnyima uhuru, kwa hiyo alishindwa kujibu inavyotakiwa kwa sababu ulimkomalia kupita kiasi.
Hata hivyo, unashauriwa kuachana na vitu vingi, badala yake unatakiwa kukusanya yote uliyopokea kuhusu mwenzi wako, mengine unapuuza halafu yale machache unayoona yanatakiwa majibu, ndiyo uyawasilishe kwake akupe majibu. Kumbuka kwamba unatakiwa uelewe kwa urahisi kile anachokwambia.
Tabia ya kukusanya mambo mengi na kutaka majibu kwa wakati mmoja ni mbaya, kwani hutoa picha kuwa umemkamia kwa maswali, kwa hiyo mwisho wake atakuona una gubu. Ishi kwa upendo, tatua mambo yako kidiplomasia. Usikubali uonekane una gubu, kwani hiyo ikipita itakufanya mapenzi yakushinde.
2. USIISHI KWA DHANA
Hutokea mtu ameketi, ghafla anaanza kusumbuliwa na mawazo kuwa mwenzi wake yupo sehemu ya hatari akifanya mambo yasiyokubalika. Hili ni tatizo la wivu ambalo huwatesa wengi, hivyo kuelekea kukamilisha mada hii, nakutaka uachane na maishi ya dhana. Tafsiri matukio.
Dhana ikitawala maisha yako, utakuwa unapenda kutuhumu bila hoja. Mbele ya safari ya maisha yako ya kutuhumu, utajikuta ni mwingi wa mawazo na kujiumiza moyo pasipo maelezo yoyote. Hujawahi kumfumania mwenzi wako lakini humuamini tu. Hii inamaanisha wewe mwenyewe hujikubali.
Tambua kuwa kama unafikiria mabaya kwa mwenzi wako bila sababu, hiyo ni dalili ya kukosa uaminifu. Mantiki hapa ipo kwenye hoja kuwa kuwaza kwamba mwenzi wako anafanya madudu, inamvunjia heshima, vilevile nawe unakuwa kwenye kapu baya, kwani si muaminifu. Jihadhari na tatizo hilo.
Unaweza kupona kwenye kipengele kuwa si muamifu kama kuna jambo aliwahi kukufanyia, hivyo ukamtoa imani. Hata hivyo, muongozo kwako uwe kwenye ukweli kuwa kama mlishaketi, mkazungumza na kukubaliana kusameheana, hutakiwi kutomuamini, kufanya hivyo ni kujiumiza. Usiishi kwa wasiwasi.
Kuna msemo: Aliwazalo mjinga ndilo linalomtokea. Maana yake ni kuwa matukio ambayo unaweza kuyaunga kwenye ubongo wako, ni rahisi kukutokea. Hutakiwi kuwaza mabaya, hebu tafakari mambo katika sura chanya. Mheshimu mwenzi wako naye akupe heshima yako unayostahili.
Ikiwa utawaza mambo mabaya, inawezekana ukamgombeza. Ukamnyima raha. Maswali yakawa mengi, huku ukimjaza tuhuma lukuki. Mwisho wa kero zake, naye atakasirika, hivyo ikiwa ana akili chafu, anaweza kufanya kweli ili unayowaza yatimie.
Unaweza kumpigia simu mwenzi wako lakini akashindwa kupokea. Usikimbilie kufikiria yupo hotelini anafanya uchafu, fikiria kazi zake kuwa ni nyingi. Baadaye akikupigia, usipande jazba kuwa hakukupokelea simu yako, zungumza naye kwa upole, kama ni maswali muulize kwa lugha laini.
Anza leo kufanyia kazi hili: Umempigia simu mwenzi wako, hajapokea. Baadaye ukimpata hewani au akikupigia, kabla ya kuzungumza lolote, unaanza kumpa pole kwa kutingwa na mambo mengi mpaka akashindwa kupokea simu ulipompigia. Hiyo ina maana kubwa, inaepusha migogoro.
Ipo wazi kuwa ubongo wa mtu mwenye wivu, hufikiria kwamba anasalitiwa kila anapopiga simu ya mwenzi wake na kutopokelewa au kuchelewa kupokelewa. Hawezi kufikiria kama mpenzi wake anaweza akawa amepata ajali. Kama simu haipatikani, hatafikiria kuwa betri imekufa. Atawaza mambo mabaya tu.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake