WAKATI kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki zikipamba moto, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa, ameshangazwa na mchezo mchafu unaoendelea kuchezwa katika kampeni za uchaguzi huo. Alisema mchezo huo umegundulika baada ya chama hicho kunasa barua iliyoghushiwa nembo ya chama na namba bandia za kumbukumbu za chama hicho, huku ikiwachafua wanachama wake.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Nkoanekoli, kata ya Nkoaranga; Kikwe na Akheri, Dk Slaa alisema amesikitishwa na barua hiyo iliyosambazwa usiku wa manane, Tengeru na Leganga karibu na kambi ya Chadema.
Alisema kitendo cha kusambaza barua hizo, kinaashiria wazi wahusika wamefilisika kisiasa na wanakaribia kufa.
Aliongeza kuwa barua hiyo inaonesha kama imeandikwa na mtu asiyeifahamu Chadema vizuri, lakini cha ajabu jina lake limekosewa na kuandikwa Silaha “wakati siitwi hivyo na imeghushiwa nembo na kumbukumbu ya chama changu, huu ni wizi ambao haukubaliki hata kisheria”.
Alisema sehemu ya barua hiyo inamshauri kuachana na Vincent Nyerere (Meneja wa Kampeni na Mbunge wa Musoma Mjini) kwa sababu amemchafua Rais mstaafu Benjamin Mkapa, anayeheshimika Meru na nchi nzima, hivyo hali hiyo itasababisha kukosa kura Meru. Aidha, alisema barua hiyo imeendelea kumchafua Vincent kwa kudai kuwa si mtoto wa ndoa, bali wa nje ya ndoa.
“Sisi tumechukua barua hizi na nakala tumepeleka Polisi na namtaka Isaya Mngulu amtafute mhusika wa barua hii, ili ashughulikiwe, kwa sababu kughushi nembo ni kosa kisheria na njia za kumpata ni rahisi, sababu anatafutwa hata kwa njia ya kompyuta,” alisema.
Dk. Slaa alisema ugomvi wake si kukosea jina lake wala kumchafua Vincent, akisisitiza kwamba “watake wasitake marehemu Nyerere ni baba yake mkubwa, hivyo hakuna uhusiano wowote na uchaguzi huu.”
Alisema ugomvi wake ni kughushi nembo hiyo ya chama na amegundua imeghushiwa baada ya kuwasiliana na Naibu Katibu wake Zitto Kabwe, ambaye alikana kuandika barua hiyo na haijui.
Pia aliendelea kusema kuwa anashangaa kuona wapinzani wao wananunua shahada kwa Sh 30,000 hadi Sh 50,000, kitendo alichokiita kuwa ni cha ujambazi wa kisiasa.
Aliwaomba wapiga kura kutorubuniwa na mtu anayepita majumbani kununua shahada zao au kunakili namba za kadi hizo, badala yake watoe taarifa kwao ili watumwe watu wa kuwashughulikia.
Nassari aomba Mgombea wa chama hicho, Joshua Nassari, aliomba kura katika vijiji vya Kikwe, Akheri na Nkoaenekoli, ili awaletee maendeleo kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo hilo.
Alisema Mfuko huo unatengewa Sh milioni 47 kwa kila mwaka na hazitekelezi kitu chochote, hivyo akipata ubunge atashirikisha wananchi kubuni miradi itakayotekelezwa kwa fedha hizo.
Polisi yamshangaa Slaa Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Isaya Mngulu, alipopigiwa simu na mwandishi wa gazeti hili kuthibitisha tuhuma hizo, alimshangaa Slaa kwa kutoa taarifa zisizo sahihi na kuongeza kuwa taarifa za kipeperushi, waraka, polisi ndio walikuwa wa kwanza kuviokota na Dk Slaa hajafika kutoa taarifa yoyote kituoni.
Aliongeza kuwa Dk. Slaa alistahili kufika na kufungua jalada ili polisi wafuatilie aliyehusika, hivyo polisi wanafanya uchunguzi wao. Naye Oscar Mbuza anaripotiwa kuwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema endapo mgombea wake wa ubunge, Sioi Sumari, atachaguliwa lakini akashindwa kutatua kero za wananchi kwa miaka mitatu na nusu ijayo, wananchi wa Arumeru watachagua mwana CCM mwingine kushika nafasi hiyo mwaka 2015.
Aidha, wazee wa kabila la Washiri wamempa wosia Sioi wakimtaka akutane mara moja na vijana, wazee na wanawake, ili kusikiliza matatizo yao mara moja endapo atashinda. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Mary Nagu, akizungumza kwenye mkutano wa kampeni za mgombea huyo, katika kata ya Nkoaranga juzi, aliwaomba wananchi kumchagua Sioi kwa vile CCM inaamini ana uwezo wa kuletea wananchi maendeleo.
Alisema ingawa wananchi wa jimbo hilo waligawanyika katika kinyang’anyiro cha kura za maoni kutokana na kuwapo wagombea sita ndani ya CCM, wanapaswa kushikamana na kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi ili kumwezesha Sioi kushinda.
Alisema baada ya mchujo mkubwa, CCM iliona Sioi ndiye mgombea anayekubalika na wananchi wengi zaidi Arumeru Mashariki na kuona hakuna haja ya kutofautiana na maoni ya wananchi walio wengi.
“Tushikamane, tuhakikishe Sioi anashinda kwa kishindo. Ni kweli walikuwapo wagombea wengine ambao wote ni watoto wetu, lakini Sioi ndiye aliyekubaliwa na wananchi wengi zaidi, kinachotakiwa sasa ni kumwunga mkono kwa nguvu zetu zote.
“CCM ina imani na uwezo wa Sioi katika kuwaletea maendeleo. Nawaomba tumpe nafasi ya kuthibitisha uwezo wake, kama mtaona hawafai mtakuwa na nafasi ya kuchagua mwana CCM mwingine 2015,” alisema Nagu. Sarakikya ashauri Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Balozi Jenerali Mirisho Sarakikya, kwa niaba ya wazee wa jimbo hilo, alimtaka Sioi akutane na wazee, wanawake na vijana mara moja, baada ya kuchaguliwa.
Alisema vijana wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira, wanawake wanakosa fedha za kuanzisha miradi ya kiuchumi, huku wazee wakikosa msaada, kero ambazo alisema ni lazima Sioi asaidie kuzipatia ufumbuzi.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Sioi alisema akichaguliwa, ataanza mara moja kushughulikia matatizo ya kimsingi ya kata hiyo likiwamo la ukosefu wa maji ambapo alisema kuna mradi mkubwa unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ambao ataufuatilia ili utekelezaji wake uanze mara moja. SAU yasonga Wakati huo huo, Chama cha Sauti ya Umma (SAU) kimeendelea na kampeni za nyumba kwa nyumba na mtu kwa mtu katika eneo la Leganga, Tengeru.
Akiomba kura kwa madereva wa teksi wa Leganga, mgombea wa SAU, Shabani Kirita, alisema tangu waanze kampeni wamefungua matawi 17 na wanachama zaidi ya 400 wamejiunga pia uchaguzi huu hata kama akishindwa, atakuwa tayari amejipanga kwa uchaguzi mwingine unaokuja na kukiimarisha chama.
Meneja Kampeni wa SAU, Johson Mwangosi, alisema siasa za matusi hazijengi bali zinashusha hadhi kwa wagombea na kutoa angalizo kwa mameneja wa kampeni wa vyama vingine kuacha wabunge watarajiwa wajieleze watawafanyia nini wananchi badala ya mameneja kutoa matusi na kutumia muda mwingi kujibu tuhuma au matusi yasiyolenga sera za vyama na maadili. *Imeandikwa na Oscar Mbuza na Veronica Mheta, Arusha
Habari Leo
No comments:
Post a Comment