ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 29, 2012

Tume, Chadema na CCM vuta nikuvute

WAKATI muda ukizidi kuyoyoma kabla ya kufanyika uchaguzi mdogo Arumeru Mashariki Jumapili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekutana na viongozi wa vyama vya siasa na wadau kujadili maandalizi ya uchaguzi huo katika kikao kilichozua vuta nikuvute baina yake, CCM na Chadema. 

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limethibitisha kukithiri kwa vitendo vinavyozua hofu ya machafuko katika kipindi hiki cha mwisho kabla ya uchaguzi, yakiwamo matukio mawili ya shambulio la kudhuru mwili na mashambulio ya kawaida manane na kuonya juu ya hali hiyo. 

Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, ndiye aliyeongoza msafara mzito wa viongozi wa NEC ukijumuisha Makamu Mwenyekiti, Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahammud Hamid, Makamishna Mtanga Mjaka, Profesa Amon Chaliga, Jaji mstaafu John 
Mkwawa na watendaji wengine wa juu wa Tume hiyo walipokutana na viongozi na wadau mbalimbali wanaoshiriki uchaguzi huo jana. 

Jaji Lubuva alisema kuna maendeleo mazuri ya kampeni na kuwapo kwa kasoro za hapa na pale na kwa upande wake, NEC imekamilisha maandalizi yote muhimu ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika ilivyopangwa. 


“Tumejipanga kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanyika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo kama ambavyo vyama vyote viliahidi. Tunaomba utulivu uliopo uendelee. 
Tume inaagiza vyama kuzingatia makubaliano yakiwamo ya kupanga wakala mmoja kwa kila kituo na mawakala ambao ni wakazi wa kata husika, ili kuwa rahisi kutambua wapiga kura,” alisema Jaji Lubuva. 

Alisema mawakala wa vyama vyote wanapaswa kufuatilia kwa makini mwenendo wa upigaji kura kuanzia ufunguzi wa vituo hadi utangazaji matokeo. 

Alisema anaamini vyama vyote vitakuwa vimewasilisha majina ya mawakala wao kama sheria ya uchaguzi namba moja ya mwaka 2010 sura ya 343 inayotaka orodha ya mawakala kuwa imefika kwa msimamizi wa uchaguzi siku saba kabla inavyotaka. 

Alisema hatua hiyo itasaidia kuepusha usumbufu usio wa lazima kabla ya uchaguzi na kwamba kukosekana kwa wakala katika kituo cha kupiga kura kwa chama fulani hakutaathiri mwenendo mzima wa upigaji kura. 

Alisema mawakala watagharimiwa na vyama. Aliongeza kuwa mwananchi ambaye amejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na kuwa na picha yake, hataruhusiwa kupiga kura endapo atakuwa hana kadi kama sheria inavyoeleza. 

Alisema mawakala wataruhusiwa kushuhudia idadi ya masanduku na ya karatasi za kupigia kura ili kuweka uwazi katika mpango mzima wa uchaguzi. 

Katika hatua nyingine, Jaji Lubuva alisema ni marufuku kwa chama cha siasa au mgombea kufanya kampeni siku ya upigaji kura na pia ni marufuku kwa wananchi kuzagaa katika vituo vya upigaji kura baada ya kupiga kura ili kuepusha vurugu. 

Alisema ni marufuku pia kwa mawakala kuorodhesha majina na namba za kadi za wapigakura. 
Mawakala ndio watahusika na kusimamia upigaji kura na usindikizaji wa kura kwenda katika kata na baadaye katika ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi ili matokeo yajumlishwe na mshindi 
atangazwe. 

Mvutano wa NEC, vyama 
Hata hivyo kauli hiyo ya NEC haikupokewa kirahisi na viongozi wa vyama vya siasa na wadau wanaoshiriki uchaguzi huo.

John Mrema, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chadema, alisimama na kuomba ufafanuzi wa NEC juu ya fomu namba 17 ambayo kisheria inaruhusu mtu aliyejiandikisha katika Daftari na picha 
yake kuwapo, apige kura kwa kutumia fomu hiyo hata kama atakuwa amepoteza kadi. 

Mrema alisema sheria ya uchaguzi inaruhusu mtu aliyepoteza kitambulisho kwa sababu ambazo ni za msingi, ajitokeze kuomba kuruhusiwa kupiga kura kwa kujaza fomu namba 17 na 
Chadema inasisitiza na itaendelea kuwasisitiza wanachama wao waliopotolewa na vitambulisho kujitokeza na kupiga kura kwa kuomba kujaza fomu hiyo. 

Pamoja na kupewa ufafanuzi na viongozi wa NEC, bado Mrema aliwabana viongozi hao kwa kutumia sheria hiyo, hatua ambayo ilimfanya Jaji Mkwawa kuwaagiza viongozi wa 
Chadema kuwasilisha kwa maandishi NEC suala hilo ili liweze kufanyiwa kazi. 

Hata pamoja na hilo, Mrema pia alilaani jambo alilosema ni hujuma la kuongezwa kwa idadi ya vituo vya kupigia kura kutoka 327 hadi 382, mpango aliosema ulishitukiwa mapema na chama hicho, na hivyo idadi hiyo kubakia 327, huku akionesha orodha ya vituo vilivyokuwa vimeongezwa na majina ya wapiga kura kwa kila kituo. 

“Mbali na hilo, hivi sasa tumegundua katika vituo karibu 86 kuna wapigakura kati ya 20 na 26 ambao wamezuiwa kupiga kura wakidaiwa kuwa na kasoro. Hapa mmetwambia ni wapigakura 
20 tu ndio wenye matatizo, jambo ambalo si sahihi tunaomba suala hili lirekebishwe na hawa watu wakubaliwe kupiga kura,” alisema Mrema. 

Vyombo vya habari, Polisi 
Katika hatua nyingine, Mrema alitumia nafasi hiyo kumwomba Jaji Lubuva kuandika barua na kuvionya vyombo vya habari vya Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN) na Shirika la Utangazaji 
Tanzania (TBC), viache kuandika na kutangaza zaidi mambo ya CCM na kutotilia mkazo habari za Chadema. 

Alisema vyombo vya umma vina wajibu wa kutangaza na kuchapisha habari za vyama vyote vya siasa bila kubagua na kwa uzito sawa, kutokana na kuendeshwa kwa kutegemea fedha 
za walipa kodi na kwamba sheria pia inaviagiza vyombo hivyo kufanya hivyo. 

“Mwenyekiti tunakuomba sasa kwa kutumia mamlaka yako na kwa mujibu wa sheria uviandikie vyombo hivi barua ili kuvionya vitii sheria za nchi.Tunataka haki sawa kwa vyama vyote.” 

Mrema pia alielekeza lawama kwa Polisi akisema pamoja na kujitahidi kufanya kazi zake ipasavyo lakini ina kasoro. 

Alisema Polisi inapaswa kufanya kazi zake bila kupendelea chama chochote cha siasa na kwamba zinapotolewa taarifa za uhalifu, Jeshi hilo linapaswa kutoa uzito sawa katika 
kushughulikia malalamiko ya vyama vyote bila kupendelea CCM. 

Alidai kwamba Chadema ina ushahidi wa CCM kuingiza kundi la vijana kutoka Moshi, Arusha, Musoma, Bunda, Tarime na Rorya, ili kuleta vurugu na Polisi inalijua suala hilo ingawa alisema haijachukua hatua zozote. 

Aliendelea kudai kwamba kama haki itatendeka hakuna sababu kwa NEC na Polisi kuhofia vurugu akaonya kuwa zitatokea kama kutakuwa na mazingira ya kuiba kura. 

Aliiomba NEC kutangaza haraka matokeo ya uchaguzi na kuhakikisha upigaji kura unaanza mapema na si mazingira ya utatanishi. 

Alisema Chadema itawasisitiza wanachama wake kukaa karibu na vituo vya upigaji kura umbali wa meta 200 kutoka eneo hilo kama sheria inavyotaka, ili kusubiri matokeo kutangazwa, lakini bila vurugu akisema ni haki yao kusubiri kusikia matokeo ya kura walizopiga. 

Jaji Lubuva aliitaka Chadema kuwasilisha malalamiko kwa Tume ya Maadili ya Jimbo, Taifa au Tume ya Rufani, pale inapoona chombo cha habari au Jeshi la Polisi hakitendi haki ili jambo hilo lishughulikiwe kwa kufuata sheria haraka na si kulalamika hatua inayoweza kusababisha uvunjaji wa kanuni na sheria. 

Dukuduku la CCM 
CCM kupitia kwa Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchaguzi, Matson Chizii, iliitaka NEC kusimamia ipasavyo sheria inayowataka wananchi kukaa meta 200 kutoka kituo cha upigaji kura ili kuepusha vurugu. 

“Naomba ufafanuzi katika hili, maana wakati mwingine tumekuwa tukishuhudiwa baadhi ya wafuasi wa vyama vingine wanaokaa meta hizo 200 au chini ya hapo hata baada ya kupiga kura wakidai kulinda kura zao jambo ambalo limekuwa likisababisha vurugu.” 

Aidha, Chizii alihoji pia juu ya sheria inayoagiza mgombea wa chama kuruhusiwa kuingia kwenye kituo cha kupigia kura yeye na wakala wake tu na si kufuatana na viongozi wengine wa 
chama akiwamo Mkurugenzi wa Uchaguzi. 

Alisema sheria hiyo imekuwa ikikiukwa kwa baadhi ya viongozi kushuka wote katika gari na kushinikiza kuingia ndani ya vituo vya kupigia kura ili kuhakiki mwenendo. 

Alishangazwa pia na hatua ya NEC kutaka wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki kutumia simu zao za mkononi kuomba ufafanuzi wa masuala yanayohusu uchaguzi kwa kuandika 
ujumbe mfupi wa simu na kutuma, akisema mpango huo unakwamisha ukuaji wa demokrasia kwa vile ni wananchi wachache wana uwezo wa kuwa na simu na kutuma ujumbe mfupi. 

Hata hivyo Chizii alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri inayofanya ya kudhibiti usalama katika Jimbo la Arumeru Mashariki na akawapongeza pia watendaji wa Tume ya Taifa ya 
Uchaguzi kwa kazi nzuri waifanyayo. 

Uvunjaji amani waongezeka 
Kamishna Msaidizi wa Polisi, Isaya Mngulu ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki ndani ya Jeshi hilo, anakiri kwamba matokeo ya uvunjaji amani 
yameongezeka hadi 36. 

Kwa mujibu wa Mngulu, matukio mawili ni ya shambulizi la kudhuru mwili ambayo yamelifanya Jeshi hilo kuyawasilisha kwa wakili wa Serikali ili kujua hatua za kuchukua. 

Alisema matukio manane ni ya shambulio ambayo yamewasilishwa mahakamani ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa. Alisema mengine 24 yapo katika hatua mbalimbali za uchunguzi. 

Alisema hatari kubwa imekuwa ikisababishwa na kauli na lugha chafu za viongozi wa vyama hivyo vya siasa kama ile iliyotolewa na CCM, kwa kusema itawaagiza vijana wao kuingia msituni na ya Chadema kwamba Arumeru itakuwa kitovu cha vurugu kama za Tunisia. 

Alitaja tishio lingine kuwa ni linalosababishwa na viongozi wa vyama vya siasa kuagiza wanachama na wafuasi wao kutoondoka katika vituo vya upigaji kura ili kulinda kura zao, jambo ambalo alisema ni kinyume cha sheria na linaloweza kusababisha uvunjifu mkubwa wa amani kabla ya matokeo kutangazwa. 

“Tunawaomba viongozi wa vyama vya siasa kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, ili kuendelea kulinda amani na utulivu hadi matokeo yatakapotangazwa.” 

Imeandikwa na Oscar Mbuza na Veronica Mheta, Arumeru


Habari Leo

No comments: