UJAUZITO wa miezi minne aliokuwa nao Bimal Alvind (36) uliyenusurika baada ya kupigwa risasi ya tumbo na kumwagiwa tindikali kwa madai ya kuuza pombe Zanzibar, umeharibika.
Mume wa Bimal, Alvind Asawla (42) aliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa ujauzito wa
mkewe uliokuwa na miezi minne ulitoka ghafla jambo lililomchanganya zaidi mkewe.
Alisema sasa mkewe aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili amekuwa kama mtoto mdogo akishtuka mara kwa mara na bado amelazwa na madaktari wamesema watamruhusu mara baada ya vidonda vyote kukauka.
Mfanyabiashara huyo na mkewe walimwagiwa tindikali na kupigwa risasi wakati wakitoka
katika biashara yao Januari mwaka huu.
Bimal alipigwa risasi tumboni akiwa na ujauzito huo lakini ulinusurika baada ya risasi hiyo kutolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili bila kuathiri ujauzito huo.
Tindikali hiyo ilimjeruhi mwilini kuanzia usoni, kifuani hadi kwenye matiti, mikono yote miwili
na tumboni.
Asawla (42) alipigwa risasi kichwani kwenye paji la uso katikati ya macho iliyotokea nyuma
chini ya shingo na sasa amepooza upande mmoja.
Katika hatua nyingine, Polisi Zanzibar wamesema bado hawajamkamata mtu yeyote kuhusu
tukio hilo kutokana na kutopata ushirikiano kutoka kwa majeruhi hao.
Kamanda wa Polisi Mjini Magharibi, ACP Azizi Mohamed alisema kuwa majeruhi hao hawako tayari kusaidia Polisi kufanya uchunguzi kwa madai ya kuwa bado hali zao siyo nzuri.
Alidai kuwa kuendelea kuchelewa kutoa ushirikiano, kunasababisha uchunguzi kuwa mgumu
na kuongeza kuwa wangewahi kutoa maelezo yao ingekuwa rahisi kuwapata watuhumiwa.
Hata hivyo Asawla alipinga madai hayo ya Polisi na kufafanua pamoja na kwamba alikuwa amelazwa hospitalini na hajisikii vizuri, polisi walifika kumhoji na mkewe wakawapa maelezo yote.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment