ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 27, 2012

Chadema wabomoa ngome ya Magufuli Chato




Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jimbo la Chato, Mkoa mpya wa Geita kimezidi kusambaratisha ngome za Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni mbunge wa jimbo hilo, Dk. John Magufuli baada ya kutwaa vijiji vinane kati ya 11 vilivyokuwa vikishindaniwa katika uchaguzi mdogo.

Uchaguzi huo ulifanyika kufuatia vifo vya waliokuwa wenyeviti wa vijiji hivyo na wengine kuhamia Chadema.

Kulikuwa na vituko vya hapa na pale na katika tukio lililovuta hisia za wengi ni lile la aliyekuwa mgombea wa CCM kijiji cha Minkoto, Lupil Siengo, kuhamia Chadema muda mfupi baada ya kutangazwa matokeo aliyekuwa mpinzani wake, Alphonce Kanungo wa Chadema kuibuka kidedea.

Uchunguzi wa NIPASHE umebaini nafasi zote zilizokuwa zikigombaniwa vyama vya Chadema na CCM katika kinyang’anyilo hicho, awali vilikuwa vikikaliwa na CCM kabla ya kujiuzulu nyadhifa zao, kufariki dunia, kuhamia vyama pinzani na wengine kuhama makazi yao ya awali.



Akizungumza na waandishi wa habari jana msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo, Sodio Nyuga, alisema Chadema kimefanikiwa kutwaa nafasi nane wakati CCM ikiambulia nafasi tatu kati ya vijiji 11 vilivyokuwa vikishindaniwa.

Uchaguzi huo pia ulihusisha nafasi za wenyeviti wa vitongoji na wajumbe wa serikali za mitaa ambapo CCM kilipata wenyeviti wa vitongoji 28 huku Chadema kikifanikiwa kupata nafasi 10 na kwamba wajumbe wa serikali za mitaa CCM kilijinyakulia wajumbe 92 dhidi ya Chadema kilichopata wajumbe 46.

Nyuga alidai uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na utulivu licha ya dosari ndogondogo zilizojitokeza kutokana na jiografia ya wilaya Chato.

Akizungumza na NIPASHE Katibu wa Chadema wilaya ya Chato, Mange Sai, alisema ushindi waliopata ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwa baadhi ya vitongoji chama chake kilifanikiwa kupitisha wagombea pasipo kuwa na upinzani wa chama tawala kitendo kinachoonyesha kukubalika kwa chama hicho kwa wananchi.

“Kimsingi uchaguzi huu umeonyesha dira kwa wanachato kwani haikuwa rahisi kwa chama cha upinzani kama Chadema kupitisha wagombea wake kwenye nafasi mbalimbali pasipo kuwa na upinzani wa wagombea wa CCM...hatua hii inaonyesha wazi jinsi wananchi walivyo na imani na Chadema kwa kuwa ndicho chama makini katika kupigania haki za wanyonge nchini,” alisema Sai.
Aidha, mbali ya mgombea huyo wa CCM kujiunga Chadema, wanachama kadhaa wa CCM kijiji cha Minkoto walimfuata ambao ni Samson Nyanda, Enock Budodi, Ester Paul, Juma Ally, Sheli Lusungula, Pius Mathias, Thomas Masomi, Jesca Myeka na Alex Kaloli.
CHANZO: NIPASHE

No comments: