Advertisements

Friday, April 27, 2012

Gwaride tamu Muungano, Chadema wasusa

Msamaha kwa wafungwa 2,973, gwaride la kusisimua na halaiki ni miongoni mwa vitu vilivyopamba sherehe za maadhimisho ya miaka 48 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana, Rais Jakaya Kikwete aliongoza maelfu ya Watanzania, wakiwamo marais wastaafu, viongozi wa serikali, mashirika, vyama vya siasa na mabalozi, hata hivyo, hazikuhudhuriwa na mwakilishi yeyote wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).



Chadema ambacho kwa sasa ndicho chama kikuu cha upinzani nchini, taarifa za kutowakilishwa kwake katika sherehe hizo, zilithibitishwa pia na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika.

Sherehe hizo zilizopambwa na gwaride maalum la askari wa vikosi vya ulinzi na usalama, vijana wa halaiki, burudani za ngoma za utamaduni na michezo ya sarakasi, zilianza rasmi baada ya Rais Kikwete kuwasili uwanjani hapo.

Maelfu ya wananchi, wengi wao wakiwa wamevalia fulana na kofia za rangi nyeupe zenye ujumbe unaohusu seherehe hizo, walianza kumiminika mapema katika uwanja huo baada ya milango kufunguliwa kuanzia saa 1.00 asubuhi.

Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, aliwasili katika uwanja huo majira ya saa 4.00 asubuhi akiwa katika gari la wazi, akiwa amefuatana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange.

Huku akishangiliwa na umati wa watu, Rais Kikwete akiwa katika gari hilo lililosindikizwa na pikipiki zilizokuwa zikiendeshwa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, waliuzunguka uwanja huo, huku akiwasalimia wananchi kwa kuwapungia mkono.

Mara baada ya kuwasili, Rais Kikwete alipokea heshima kutoka kwa vikosi vya ulinzi na usalama, kabla ya mizinga 21 kupigwa, wimbo wa taifa, salamu ya utii na heshima kwa Amiri Jeshi Mkuu.

Baadaye, Rais Kikwete alikagua gwaride maalum lililoandaliwa na vikosi hivyo.

Vikosi vilivyoshiriki gwaride hilo ni pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania-JWTZ (kikosi cha bendera, ardhini, anga na majini), Jeshi la Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Polisi.

Vikosi hivyo vilipita mbele ya mgeni rasmi, jukwaa kuu na kutoa heshima kwa mwendo wa pole na mwendo wa haraka.

Askari wanawake wa vikosi vyote na wa polisi wanaume wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walikuwa kivutio kikubwa kwa maelfu ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo, kutokana na ukakamavu waliokuwa wakiuonyesha walipokuwa wakipita kwa mwendo wa haraka mbele ya Rais Kikwete.

Wanafunzi 727, wakiwamo 500 kutoka shule za msingi za Tanzania Bara na 200 za Zanzibar, waliumba maumbo mbalimbali ya halaiki na wengine 27 kutoka shule mbalimbali za msingi za serikali walionyesha michezo ya sarakasi na kuwa sehemu ya burudani katika sherehe hizo.

Miongoni mwa halaiki zilizoumbwa na vijana hao ni pamoja na bendera ya taifa, umbo la herufi zinazosomeka: “Miaka 48 ya Muungano”, maumbo ya mazao ya kiuchumi (katani, karafuu, mashua ya uvuvi pamoja na pamba), umbo la madini ya Tanzanite na kusimamisha bendera ya taifa.

Umbo lingine lilikuwa kwa ajili ya kuimba wimbo maalum usemao: “Uamuzi wa busara” kuwashukuru Mwalimu Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Aman Karume kwa kuanzisha Muungano na kudumisha umoja wa Watanzania.

Pia walitengeneza kaulimbiu ya sherehe hizo isemayo: “Miaka 48 ya Muungano shiriki kikamilifu katika sensa na mchakato wa mabadiliko ya Katiba.”

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliounda Taifa la Tanzania, uliasisiwa na Mwalimu Nyerere na Karume Aprili 26, 1964.

Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, pamoja na mawaziri wakuu wastaafu, Dk. Salim Ahmed Salim na Frederick Sumaye.

Wengine waliohudhuria ni Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilali, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Wengine ni Spika wa Bunge, Anne Makinda, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete na Mjane wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere, mawaziri na wabunge.

Vyama pekee vya siasa vilivyowakilishwa ambavyo viongozi wake walitangazwa na muongoza sherehe kuhudhuria sherehe hizo jana, ni CUF, UDP na Tadea.

CUF iliwakilishwa na Mwenyekiti wake Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba. UDP iliwakilishwa na Mwenyekiti wake Taifa ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo na Tadea iliwakilishwa na Rais wake, John Chipaka.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, aliliambia NIPASHE baada ya sherehe hizo kwa njia ya simu jana kuwa Chadema haioni sababu ya kufanya sherehe bila kushughulikia matatizo ya msingi yanayolikabili taifa kwa muda mrefu.

“Leo (jana) tuko kwenye sekretarieti ya chama taifa kwa ajili ya maandalizi ya mkutano wa kesho (leo) wa kamati kuu,” alisema Mnyika.

Aliongeza: “Mwenyekiti na katibu mkuu hawakuhudhuria kutokana na majukumu mengine, hata hivyo ifahamike kuwa Chadema tunaweka kipaumbele katika mijadala ya kuhakikisha Muungano unalindwa kwa mabadiliko ya msingi ya kikatiba na kimuundo kufanyika badala ya muundo wa sasa wa Muungano unaoendeleza kero za miaka 48 za Muungano. Hakuna sababu ya kusherehekea bila kushughulikia matatizo ya msingi yanayolikabili taifa kwa muda mrefu.”

WAFUNGWA 2,973 HURU

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 2,973, katika maadhimisho ya sherehe ya miaka 48 ya Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, ilisema Rais ametoa msamaha huo kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Katika taarifa hiyo, Nahodha alisema wafungwa watakaonufaika na msamaha huo ni ambao wanatumikia kifungo kisichozidi miaka mitano ambao hadi siku ya msamaha watakuwa wametumikia robo vifungo, wafungwa wenye magonjwa ya ukimwi, kifua kikuu na saratani ambapo katika kundi hili sharti wathibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mfawidhi wa mkoa au wilaya.

Wengine watakaonufaika na msamaha huo ni wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi, wafungwa wa kike walioingia gerezani wakiwa na mimba, walioingia na watoto wanaonyonya na wafungwa wenye ulemavu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo msamaha huo hautawahusu wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, wanaotumikia kifungo cha maisha, waliojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, wanatumikia kifungo cha makosa ya kupokea na kutoa rushwa na wale wanaotumikia kifungo cha makosa ya kutumia silaha.

Wengine ambao msamaha huu hauwahusu ni wafungwa wanaotumikia kifungo cha makosa ya kupatikana na silaha, makosa ya kunajisi, kubaka na kulawiti, wizi wa magari, waliowapa mimba wanafunzi, walioharibu miundombinu na wafungwa wazoefu.

Wengine ni wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msahama wa rais, wanaotumikia kifungo chini ya sheria ya bodi za Parole, waliowahi kutoroka au kujaribu kutoroka, wanatumikia kifungo cha kutumia vibaya madaraka na waliohukumiwa kwa kosa kuzuia watoto kupata masomo.

“Ni mategemeo ya serikali kwamba watakaoachiliwa huru watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na watajiepusha na kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani,” alisema Nahodha kwenye taarifa hiyo.

CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

babu seya vipi, mbona hajamtoaa?.Kikwete fikiria hilo.