ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 8, 2012

Dk. Shein aongoza hitima ya Karume

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, akiweka shada la maua kweye kaburi la Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Abeid Amaan Karume katika Viwanja vya CCM Kisiwandui mjini Unguja. (Picha na Ramadhan Othman).

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohammed Shein jana aliongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, iliyofanyika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar. 


Hitma hiyo pia, ilihudhuriwa na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi aliyemwakilisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete. 

Pia walikuwepo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd na Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid Karume. 

Wengine ni viongozi wa serikali zote mbili na viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa, masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, wabunge na wawakilishi pamoja na mabalozi wadogo waliopo hapa Zanzibar. Hitma hiyo ilitanguliwa na Kuran Tukufu, iliyosomwa na Ustadh Rashid Jaffar na kuongozwa na Sheikh Mohammed Kasim kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar. 

Mara baada ya hitma hiyo, Sheikh Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Mussa Salum alitoa mawaidha na kumuelezea marehemu Karume kuwa ni kiongozi aliyewatetea wanyonge na aliyepigania maendeleo ya wananchi wa Zanzibar. 

Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka inapofika tarehe 7, Aprili siku ambayo Karume aliuawa, viongozi hao na wananchi walimuombea dua, marehemu Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa afisi hiyo ya CCM Kisiwandui

Habari Leo

No comments: