Na: Ally Mbetu
NAAM tumekutana kwa mara nyingine, afya yangu namshukuru Mungu ni salama, nina imani nanyi pia mu wazima wa afya, kama kuna mgonjwa, nampa pole kisha namuombea kwa Muumba ampe afya njema.
NAAM tumekutana kwa mara nyingine, afya yangu namshukuru Mungu ni salama, nina imani nanyi pia mu wazima wa afya, kama kuna mgonjwa, nampa pole kisha namuombea kwa Muumba ampe afya njema.
Baada ya salamu, tuwe pamoja kwenye mada yetu ya leo ambayo naomba uelewe undani wake usije kusema hujanielewa. Sasa hivi kati ya watu kumi, watano wanamiliki simu ya mkononi. Hii imekuwa ikirahisisha mawasiliano, lakini baadhi ya watu wamebadili maana ya simu na kuibebesha kazi nyingine ambayo si yake.
Nimekuwa nikipokea malalamiko ya matatizo mengi katika mapenzi sababu kubwa ikiwa ni simu ya mkononi. Wengi wamewaona wapenzi wao kama si waaminifu na wengine kuamini kabisa hawapendwi, sababu ikiwa ni hii simu ya mkononi.
Kumekuwa na utaratibu wa kutumiana ujumbe wa mapenzi kwa wapenzi ambao huwa kama ndiyo tafsiri hasa ya yaliyo moyoni.
Si ujumbe mzuri tu wa simu bali hata kuzungumza maneno matamu yatokayo midomoni yanayoonyesha ninyi kama wapenzi mnapendana kwa dhati.
Kutokana na hali hiyo, wengi huamini kwa asilimia 100 kuwa wanapendwa, lakini mawasiliano yanapopungua au kukatika mhusika mmoja au wote lazima wataanza kuamini kuwa mapenzi yamepungua.
Nataka kuwafumbua masikio wote wanaoamini simu ndiyo tafsiri sahihi ya mapenzi, niwaambie tu kuwa mapenzi ya kweli hayakai ndani ya simu, bali moyoni mwa mtu, si wote wanaopenda kutumia simu wakati wote.
Wapo ambao hupenda kutumia usiku tu na wapenzi wao hasa wanapokuwa wamepumzika, kwa kuwa mchana huwa na mambo mengi. Hapa wenza wengine hasa wale wasiojua muda sahihi wa kuchati au kuzungumza na wapenzi wao, huamini kuwa mapenzi yamepungua.
Kipindi cha kazi ni muda wa kujuliana hali na siyo wakati sahihi wa kuchati au kuzungumza kwa muda mrefu, wengine wapo kazini lakini muda mrefu wanazungumza mambo ya mapenzi na kujisahau, wanatakiwa kutambua kuwa simu ina wakati wake.
Kwa hali kama hiyo, wengi hushindwa kuelewa maana ya simu kwamba si kipimo cha mapenzi bali upendo wa mtu upo moyoni.
Wengi wamekuwa wakiamini yote yanayoandikwa katika ujumbe wa mapenzi ni mapenzi kamili, unaweza kuwa na mpenzi ambaye kawaida yake ni kuchukua ujumbe wa mapenzi kwenye gazeti na kukutumia lakini si kilichomo moyoni mwake.
Kuujua upendo wa kweli si kwa maneno au ujumbe mtamu bali vitendo vya kuonyeshana kweli mnapendana.
Asilimia kubwa ya walioanzisha uhusiano kwa njia ya simu, wameumizwa na hizohizo simu, hadi kufikia hatua ya kusafiri umbali mrefu na mwisho wake kukuta tofauti kubwa na yaliyoandikwa kwenye ujumbe au maneno matamu kwa njia ya simu.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwaeleza wote ambao huamini ujumbe au maneno matamu katika simu ndiyo mapenzi kamili, usiukabidhi moyo wako kwa mtu kwa ajili ya simu.
Siku zote ili kupata mpenzi wa kweli, unatakiwa kutumia muda mrefu kuchunguza tabia yake, ukiridhika ndipo uutoe moyo wako ukiamini unayempa ni mtu sahihi.
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment