ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 8, 2012

Ikulu yakanusha, JK hana biashara binafsi-Habari Leo

OFISI ya Rais, Ikulu imetangaza kuwa Rais Jakaya Kikwete haendeshi, hajawahi kuendesha 
na wala hana mpango wa kuendesha biashara, iwe yeye binafsi au na familia yake tofauti. 

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, 
ilieleza kwamba shughuli ambazo Rais Kikwete anazipenda na ambazo anajishughulisha nazo ni 
kilimo na ufugaji. 

“Kwa ajili hiyo ana mashamba Sanzale, Kiwanga na Msoga. Hata shughuli hizo hazijafikia kiwango cha kibiashara kwani hutumia fedha zake za mfukoni kugharimia shughuli hizo,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu. 

Taarifa hiyo ilikanusha habari za gazeti la kila wiki la Dira ya Mtanzania toleo la jana, lenye kichwa cha habari ‘Familia ya JK yachafuliwa’ ikimhusisha Rais Kikwete na biashara. 

Katika habari hiyo, gazeti hilo lilidai kuwa familia ya Rais Kikwete inafanya biashara na Kampuni ya Home Shopping Centre (HSC) ya Dar es Salaam na kuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Said Saad ndiye msimamizi wa biashara za familia hiyo ya Rais. 

“Tunapenda kuujulisha umma habari hizo si za kweli. Ni uongo unaolenga kuupotosha umma na kuchafua jina la Rais Kikwete na familia yake au vinginevyo unalenga kuchafua jina la Kampuni ya Home Shopping Centre. Kama nia ni kufanya hivyo tafadhali msilitumie jina la familia ya Rais. 

“Badala ya kutoa tuhuma za jumla jumla zisizokuwa na ushahidi wowote ni vema muwe wawazi. Ni vema gazeti likaeleza namna gani au likamtaja ni nani ndani ya familia ya Rais Kikwete anaendesha biashara kwa kushirikiana na Kampuni ya Home Shopping Centre,” ilieleza taarifa hiyo. 

Ikulu katika taarifa hiyo, imeeleza kuwa inatarajia gazeti hilo litatoa majibu ya masuala hayo 
muhimu katika toleo lake lijalo, vinginevyo familia ya Rais itakuwa na haki ya kuchukua hatua stahiki za kisheria.

No comments: