ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 16, 2012

Kesi ya kupinga matokeo Igunga yanguruma-Habari Leo

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora imepokea ushahidi wa Mussa Tesha, mkazi wa Igunga aliyemwagiwa tindikali wakati wa kampeni za Uchaguzi Mdogo ikiwa ni mwendelezo wa kusikiliza maelezo yake kwenye kesi ya kupinga matokeo yaliyompatia ushindi Mbunge wa Igunga, Dk. Dalaly Kafumu (CCM). 

Tesha, ambaye ni shahidi wa pili katika kesi hiyo iliyofunguliwa na Joseph Kashindye, aliulizwa maswali mbalimbali na mawakili wa upande wa mlalamikaji na hakujibu chochote zaidi ya kukaa kimya mahakamani. 

Jaji Mary Shangali anayesikiliza kesi hiyo, alimwamuru shahidi huyo atoke kizimbani hapo huku wasikilizaji mahakamani wakimshangaa kwa kutojibu maswali. 

Kashindye, aliyekuwa mgombea wa ubunge Igunga kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alifungua kesi hiyo dhidi ya Dk. Kafumu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi. 

Awali, shahidi huyo wa pili, Tesha alidai mahakamani jana kwamba Agosti 10, mwaka jana alikuwa na kazi ya kubandika mabango ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jimboni Igunga. 

Alidai baada ya kumaliza kazi, alirudi nyumbani na alipofika jirani na ofisi ya Chadema, aliona watu watatu waliomvamia na kumtupia ndani ya gari na kumpeleka kusikojulikana ambako alimwagiwa tindikali. 

Alidai kutoa maelezo, kuwa baada tukio hilo alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando na kisha Muhimbili ambako ilishindikana na hivyo kwenda India kwa matibabu zaidi. 

Kutokana na ushahidi huo, hakuna wakili wa upande wa madai aliyeuliza swali kwa kile kilichodaiwa kuwa ushahidi wa Tesha ulikuwa ni wa jinai na siyo wa madai na shahidi huyo hakuwapo kwenye kampeni hizo. 

Badala yake, mawakili walimwuliza maswali mengine mbalimbali ambayo hakuyajibu. Kesi hiyo inaendelea leo kwa mashahidi wa kujibu madai. Idadi ya mashahidi wa upande wa mlalamikaji imefikia 15.

No comments: