ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 17, 2012

KUTEMWA UWAZIRI: Maige afichua siri *Mwanasheria ajipanga kuchukua hatua *Kuanika uozo wa Maliasili bungeni

Bw. Ezekiel Maige, Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii
Na Salim Nyomolelo

ALIYEKUWA Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige, amefichua siri nzito zilizochangia kung'olewa katika wizara mojawapo ikiwa ni kugusa maslahi vigogo wenye nguvu kubwa na ushawishi wa hali ya juu.

Bw. Maige ilifichua siri hiyo jana kupitia ujumbe wake alioutoa kwenye mtandao wa kijamii. 

Aliongeza kuwa maamuzi aliyokuwa akiyatoa wakati akiwa waziri wa wizara hiyo alijua fika kuwa hayawafurahishi vigogo hao.



"Kwa kifupi sana, niwafahamishe kuwa yaliyotokea ni ushahidi kwamba maliasili ni ngumu... ni ngumu kukabiliala na wabaya. Wapo waliojipanga ukiwavamia hovyo hovyo unaondoka wewe," alisema Bw. Maige na kuongeza; "Ndivyo ilivyotokea."

Alisema maamuzi yake aliyokuwa akisimamia ndiyo yamemfanya yamfike yaliyotokea. Alisema akiwa wizarani alisimamia sheria na kuwapa vitalu Watanzania maskini wenye sifa na kuwaacha wazungu kama sheria ilivyoelekeza. 

"Ni Waziri gani aliyewafikisha mahakamni watorosha twiga akina Kamrani na wenzake? Watu wametumia records (kumbukumbu) za matukio ya mwaka 2009/10 kuficha matendo na maamuzi ya kishujaa ya Maige ya 2011," alisema Bw. Maige na kuongeza;"Yawezekana hawakutaka nipate sifa, lakini ipo siku nitaipata. Tena si siku nyingi. 

Niliwaomba wenzangu wamwogope Mungu...bado nasisisitiza hivyo."Alihoji kuwa; "NI waziri gani  aliyefunga biashara ya wanyamahai, ni waziri gani aliyeonesha mfano wa kuchukua hatua kwa watumishi pale alipoona hawatendi sawa? Lakini mimi sikusita kuchukua hatua."

Alisema anawahakikishia wazalendo kuwa wamepoteza mpambanaji  aliyejitolea kupambana na wahalifu angani, majini, porini, mijini na vijijini ndani na nje ya nchi.

Bw. Maige alisema alitumia kila aina ya uwezo wake kuzawadia taifa lake utumishi uliotukuka. 

Alisisitiza kuwa maamuzi hayo magumu  yamegusa watu wenye nguvu na ushawishi mkubwa. "Nilitegemea vita hii, na ninaamini tutashinda," alisema Bw. Maige akinukuu maneno aliyowahi kuyatamka Bungeni na kuongeza;"Watanzania wapenda haki wanisikilize kwa makini muda haukuruhusu, ila nitarudi bungeni na nitasema."

Kuhusu sakata la nyumba alisema suala hilo amelifafanua na kutoa vielelezo. "Kila mbunge aliyetaka alikopeshwa sh. milioni 290, wengine wameanzisha biashara na wengine wamenununua magari na wengine majumba," alisema.

Alisema mwenye mashaka aende kwa Msajili wa Hati Wizara ya Ardhi, au kwa kamishna wa maadili, au CRDB tawi la Azikiwe na Dodoma alikokopa au amtafute muuzaji.

Alisema maeneo yote hayo atapata rekodi ya bei. "Wapo wahuni, kwa maslahi ya kisiasa na chuki binafsi wametangaza bei tofauti na niliyonunulia...mwanasheria wangu anashughulikia suala hilo," alisema Bw. Maige.

Kwa upande wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Maige alisema haikumgusa, kwani ilikuwa inaishia Juni 2010, wakati yeye alipewa dhamana ya kuongoza wizara hiyo Novemba 2010.

Kuhusu biashara ya wanyamahai, Bw. Maige alisema hakuna wanyama waliosafirishwa kinyume cha sheria wakati wa uongozi wake mwaka 2011 na kuwa matukio ya utoroshaji yalipobainika, walifungua mashitaka kwa watuhumiwa na kufunga biashara hiyo.

Aliahidi kuwawakilisha wananchi wa Jimbo lake la Msalala kwa mujibu wa katiba na ahadi zake kwao atazitekeleza hadi 2015 watakapopata fursa ya kuamua vinginevyo. Bw. Maige kabla ya kuteuliwa kuwa waziri kamili wa wizara hiyo mwaka 2010, alikuwa naibu waziri akiwa chini ya Bi. Shamsa Mwangunga.

Majira

3 comments:

Anonymous said...

Mambo ya kumwaga unga na mimi nimwage mboga

muddy washington said...

namkubali maige ni mzalendo sema ile wizara ina watu vichwa maji sana toka enzi za kina ndolanga,kuna wizara mbili zenye watu vichwa maji ambao huwapa hard time mawaziri,hiyo na wizara ya ardhi

Anonymous said...

Inashangaza sana kuona kuwa wabunge wanakopeshwa shillingi 290! wakati wanafunzi hawana hata madawati ya shule!mahospitali hayana madawa na vitanda vya kutosha!Huu ubinafsi ni mbaya sana,kila kiongozi anajifikiria nafsi yake na familia yake lakini hawafikirii shida za wananchi!Hata Maige ni mmbinafsi pia,sasa anabwata hovyo baada ya kuondolewa cheo? Hayo ni maneno ya mkosaji!viongozi wengi wanafikiria matumbo yao tu,hakuna hata mmoja aliyekuwa bora,wote wanalindana kwa maslahi yao binafsi,Mafisadi ni wengi tu!