ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 31, 2012

Maige amvaa Nape


  Amtaka ajipime kazi imemshinda
  Ajibiwa kuwa yeye siyo zaidi yake
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Ezekiel Maige
Ezekiel Maige aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye alitemwa katika Baraza la Mawaziri mapema mwezi huu,  amemvaa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, akimtaka aache tabia ya kutoa kauli ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaelekea kukidhohofisha chama.

Maige ambaye pia ni Mbunge wa Msalala (CCM) Mkoani Shinyanga, alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua matawi mawili ya wakereketwa wa CCM ambao ni wajasiriamali katika kijiji cha Isaka wilayani Kahama na kusema kuwa hivi sasa kuna wimbi kubwa la wanachama wa chama hicho kuhamia chama kingine.


Maige alimtaka Nape apime utendaji wake tangu alipoishika nafasi hiyo na wanachama wangapi wamekwisha kujiunga na chama hicho.

Alisema kutokana na hali hiyo, Nape, atajipima na kuona kama anaimudu kazi yake.

Alisema mbali na Nape kushindwa kuzuia wimbi la wanachama kukihama chama hicho, pia alikwishatoa kauli ambayo haistahili kuvumiliwa na wana-CCM wenye uchungu na chama, ya kudai kuwa hata kama wanachama watahama wote yeye (Nape) hawezi kuhama na kwamba ni vema abaki peke yake na CCM haitakufa.

Maige alisema kuwa kauli hiyo haiendani kabisa na hali halisi ya kisiasa ilivyo kwa sasa nchini na pia ni kauli ambayo haikijengi chama, bali ni kuleta makundi ambayo yanaweza kukibomoa chama.

Alibainisha kuwa yeye kama mwana-CCM na wengine wanaona kwamba hivi sasa Nape hafanyi kazi ya uenezi na kukirejeshea chama haiba na mvuto ambao kimeupotea kwa wananchi na kwamba kazi anayoifanya sasa ni kukuza makundi.

“Jamani Nape anachokifanya sasa ndani ya chama mimi ninaweza kuamini kwamba anatumika na kukidhi matakwa ya waliomtuma na siyo kwa manufaa ya chama,” alisema Maige.

“Kwa hali hii ambayo Nape amekifikisha chama hapa kilipo, ni vizuri sasa akajipima uwezo wake kama una tija gani ndani ya chama, ni vyema sasa akajiona mwenyewe kwamba yeye ni gamba namba moja na hivyo ni vyema akijivua badala ya kusubiri wana-CCM kumvua gamba lake,” alisema.

NAPE: MAIGE SIYO SAIZI YANGU 

Nape alipotakiwa na NIPASHE kuzungumzia kauli hiyo ya Maige, alisema hana muda wa kujibizana naye kwa kuwa siyo saizi yake.

“Saizi yake ni kwenye wilaya, tawi na kata, huko ndiko watakakoshughulika naye. Hivyo, sina muda wa kujibizana naye,” alisema Nape.

Hata hivyo, Nape alisema hajapewa taarifa rasmi za mtandao wa chama juu ya shughuli hizo za kichama zilizofanywa na Maige wilayani humo.

AAPA KUIBANA SERIKALI BUNGENI


Katika hatua nyingine, Maige, amesema kuwa kuanzia sasa ataelekeza makali yake bungeni ambapo ataihoji serikali mambo mbali mbali kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wa jimbo lake wanapata maendeleo kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010.

Maige alisema kuwa ahadi zote ziko kwa maandishi kwenye Ilani ya CCM, hivyo atasimama imara ili kuhakikisha zinatekelezwa kwa wakati.

Maige aliyasema hayo kwa nyakati toafuti wakati akihutubia wananchi kwenye mikutano ya hadhara baada ya kuwasili jimboni humo.

“Sasa mimi ni kama mbwa mkali aliyekuwa amefungwa na kamba na sasa amekata kamba....unajua mbwa mkali aliyefungiwa kwenye banda lake akikata kamba na kuingia mitaani ni hatari sana, sasa pale Dodoma patachimbika, nafikiri wananchi wenzangu mlikuwa mkiniona kabla Rais wetu Kikwete hajanipatia nafasi ya uwaziri,” alisema.

Alisema kuwa hatakuwa tayari wala kutetereka katika kuibana serikali, kwani sasa anayo nafasi kubwa ya kuibana tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kama waziri alikuwa na wajibu wa kuitetea serikali.

Alisema kuwa hatakuwa tayari kuona wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu wanatimuliwa kwenye maeneo yao waliyoyagundua wao wenyewe kisha maeneo hayo kupewa watu wengine.

“Sitakuwa tayari kuona wachimba madini wadogo wadogo wakitimuliwa kwenye maeneo yao waliyogundua dhahabu kwa kuambiwa kuwa ni leseni ya mtu wala sitakuwa tayari kuona mradi wa umeme wa kijiji cha Segese unachelewa wakati ahadi hiyo sasa ni ya miaka 12 tangu utawala wa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa,” alisema.

“Sitakuwa tayari kuona wananchi wangu wakikosa mbolea na kuletewa mbegu za pamba zilizooza huku waliofanya hivyo wakiwa ni wafanyakazi wa serikali na wakiendelea kutesa bila usumbufu wowote wala hatua za kisheria kutokuchukuliwa dhidi yao,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa hatakuwa tayari kunyamaza huku migogoro ya ardhi miongoni mwa wananchi ikiendelea, ikiwa ni pamoja na wafugaji kuvamia katika maeneo ya wakulima bila serikali kuchukua hatua.

Alisema atasimama imara katika kutetea na kuwa mwakilishi mzuri wa wananchi wa jimbo lake bungeni na kwamba sasa mawaziri wajipange sawasawa katika kukabiliana naye, kwani lengo kubwa ni kahakikisha wananchi wake wanapata maendeleo na ahadi za serikali zinatekelezwa na kwa wakati.

Juzi Maige ambaye amefuatana na Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja, alihutubia maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Isaka na kuwaomba kumpa ushirikiano wa kutosha ili jimbo hilo lipate maendeleo endelevu na kuwaeleza waachane na siasa alizoziita kuwa  ni za maji taka na za kupakana matope.

Kwa upande wake, Mgeja alisema kuwa CCM mkoani Shinyanga inajua na kuthamini mchango uliotolewa na unaoendelea kutolewa na Maige katika suala zima la maendeleo ya wananchi na chama kwa ujumla.

Mgeja alisisitiza kuwa  chama hicho mkoani humo kamwe hakiwezi kumsaliti Maige hata siku moja.

Maige ni miongoni mwa mawaziri sita na manaibu mawaziri wawili walioacchwa na Rais KIkwete katika mabadiliko ya baraza la mawaziri alilolitangaza Mei 4, mwaka huu.

Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyowasilishwa katika mkutano wa saba wa Bunge na Mwenyekiti wake, James Lembeli, ikimtuhumu Maige kushindwa kudhibiti ubadhirifu katika wizara yake kama ulivyobainika katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii na usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi.

Mawaziri wengine waliachwa kutokana na tuhuma mbalimbali zilizotokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC); kwamba walishindwa kusimamia wizara zao na kuisababishia serikali hasara na wengine kutumia vibaya mabaraka yao.

Walioachwa ni Mustafa Mkulo (Fedha); Omar Nundu (Uchukuzi); William Ngeleja (Nishati na Madini); Dk. Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara). Manaibu mawaziri walioachwa ni Athuman Mfutakamba (Uchukuzi) na Dk. Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii).


 
CHANZO: NIPASHE

No comments: