ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 17, 2012

Majambazi wavamia, waua mtoto wa mwaka 1-Habari Leo

MAJAMBAZI wamevamia mfanyabiashara nyumbani kwake na kuua mtoto wa mfanyabiashara huyo mwenye umri wa mwaka mmoja kwa kumkata panga kichwani na kumpora Sh milioni 8. 

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Advocate Nyombi alisema kuwa uvamizi huo ulifanyika saa 7 usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Mamba wilayani Chunya. 

Alimtaja mtoto aliyeuawa baada ya kukatwa na panga kichwani na miguuni kuwa ni Shomo Gida na wazazi wake Gida Mawe (35) na Pili Kabithe (25) walijeruhiwa kwa na kulazwa katika hospitali ya Chunya kwa matibabu zaidi. 

Nyombi alisema mbinu iliyotumika na majambazi hao ni kuvunja mlango kwa kutumia shoka kisha kuingia ndani. Kwa mujibu wa Kamanda Nyombi, mtuhumiwa Ndango Mbeshi anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi. 

Wakati huo huo, bweni la wanafunzi wa sekondari ya Chimala Misheni limeteketea kwa moto pamoja na mali zote zilizokuwa ndani na thamani bado haijafahamika. 

Ajali hiyo ilitokea saa 1.30 usiku juzi katika shule hiyo iliyoko Mbarali na hakuna madhara yaliyotokea kwa wanafunzi na chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika na uchunguzi unaendelea. 

Katika tukio lingine watu wawili Rodrick Mwanzukwa (19) na Dani Joseph (20) wakazi wa Utengule, Mbeya Vijijini wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kukutwa na misokoto 99 ya bangi sawa na gramu 480. 

Watuhumiwa hao walikamatwa juzi Utengule na askari wa doria na watafikishwa mahakamani wakati wowote upelelezi utakapokamilika.

No comments: