ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 18, 2012

Shivji: Walalahoi wasipopambana hawataipata katiba inayowaridhisha

Profesa Issa Shivji
Florence Majani
MHADHIRI Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Issa Shivji amesema kuwa, Tanzania haiwezi kufanya mchakato wa katiba mpya bila kuwepo kwa dhana ya mapambano.
Akizungumza katika mhadhara wa Katiba uliorushwa na kituo cha televisehni cha ITV, Profesa Shivji  alisema, mapambano yanahitajika katika kupata Katiba mpya kwa kuwa, mara nyingi mfumo unaotawala na taasisi zake hujimea katika kujipendelea jambo ambalo huifanya Katiba iangalie maslahi yatakayowanufaisha watawala.


“Katika taifa lenye watawala na watawaliwa, Katiba haiwezi kupatikana kama zawadi, bali ni sehemu ya mapambano,” alisema Profesa Shivji.

Aliongeza: “Walalahoi wasipopambana hawawezi kupata katiba inayowaridhisha.”
 Akifafanua hoja hiyo, Profesa Shivji alisema, dhana ya Katiba ilizaliwa katika mapambano kati ya vikundi vyenye maslahi yanayogongana.“Katiba ni uwanja wa mapambano kati ya vikundi vya ‘walala heri na walala hoi,” alisema Shivji.
Alisema hayo akitolea mfano wa tabaka la wachumi na wanasiasa ambao huweza kuitengeneza Katiba kwa maslahi ya matabaka yao.

“Katika nchi nyingi duniani, fikra zinazotawala za kikatiba ni fikra za tabaka linalotawa, kwa watawala, katiba ni mipaka ya kulinda maslahi yao” alisema.
Aidha Profesa Shivji aliwataka wananchi kufanya mijadala ili kupata muafaka wa Katiba hiyo.
“Ili mchakato wa Katiba mpya ufikie muafaka, hakuna budi kuwepo kwa mijadala ambayo ndiyo njia pekee ya amani ya kuipata katiba mpya,” alisema Profesa Shivji.

Alisema, mijadala itawasaidia wananchi kupata elimu kwani watazungumza, watatoa manung’uniko yao, wataeleza wanachokipenda na mambo ambayo hawayataki yawemo katika katiba hiyo.“Mijadala itawawezesha watu kujifunza na kujenga hoja, lakini niwasihi kuwa, katika mijadala lazima mzikubali hoja za wengine,” alisema.
Hata hivyo, Mhadhiri huyo mstaafu alisema, pamoja na kuwa Katiba ni mapambano lakini muafaka wake haulazimishwi kwa mabavu.

“Kwa kuwa zipo pande mbili zenye mvutano, hivyo basi lazima uwepo muafaka ambao hata hivyo hautakiwi upatikane kwa mabavu,” alisema.

 Mbali na mijadala, Profesa Shivji alisema, ili kujenga muafaka wenye manufaa kwa wote, taifa halina budi kuwa na dira na viongozi watakaowezesha mchakato huo.

Alitoa mfano wa dira kwa taifa kuwa ni Azimio la Arusha ambalo baba wa taifa mwalimu Julius nyerere, alilianzisha ili kujenga taifa la ujamaa na kujitegemea.
Mnamo Novemba mwaka jana Rais Jakaya Kikwete alitia saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 na hivyo kuifanya kuwa sheria.

Hatua hiyo ya kutia saini Muswada huo ilihitimisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuwa limepitisha Muswada huo uliowasilishwa na Serikali bungeni.
 Katika kuundeleza mchakato huo, hivi karibuni Rais alitaja majina ya wajumbe wa Tume ya Katiba mpya ambayo itafanya kazi ya kuratibu na kukusanya maoni.
 Tume hiyo ambayo mwenyekiti wake ni Jaji Joseph Sinde Warioba, imeanza kazi Mei Mosi mwaka huu na inatarajiwa kufanya kazi kwa kipindi cha miezi 18.

Mwananchi

No comments: