ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 14, 2012

Taifa Queens yaweka heshima IFNA-Mwananchi


Taifa Queens
Jessca Nangawe
TIMU ya taifa ya netiboli ya Tanzania, Taifa Queens, imeweka heshima katika mchezo huo baada ya kushika nafasi ya pili katika michuano ya mataifa ya Afrika kwa netiboli yaliyomalizika juzi usiku kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa.

Mchezo wa mwisho ulikuwa kati ya Tanzania na Botswana ulimalizika kwa wenyeji kushinda 32-23 katika mchezo ulioharibiwa kuvuja kwa paa la uwanja huo na kusababisha mpira kusimama kila mara.

Malawi ambao wanashika nafasi ya tano duniani na ya kwanza Afrika kwa ubora, walitwaa ubingwa huo baada ya kushinda mechi zake zote. Tanzania ni ya nne Afrika na 20 duniani.

Tanzania iliyoingia kambini tangu Febuari 20, ilipoteza kwa Malawi pekee kwa mabao 34-30 lakini ikazifunga Lesotho 57-13, Zimbabwe 25-18 , Zambia 37-33 na Botswana 32-23 katika mchezo wake wa mwisho.

Makocha wa timu hiyo, Mary Protas na Mary Waya walionyesha furaha yao baada ya kumalizika mechi za juzi kwa timu hiyo kushika nafasi ya pili na kusema iko siku itatwaa ubingwa wa michuano hiyo ambayo mwakani inafanyika Malawi.

Waya, kocha anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Netiboli, IFNA, alisema wanajipanga kwa michezo mbalimbali ya dunia. Mwenzake, Protas aliwasifu wachezaji kwa jitihada zao na kuweka heshima.

Mashindano hayo yalifungwa na Mke wa Makamu wa Rais, Mama Bilal kwa wanamichezo walioshiriki kupita mbele wakiongozwa na brasi bendi ya polisi. Zambia ilishika nafasi ya tatu.

No comments: