ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, May 1, 2012
Takukuru yawachunguza Mawaziri wanaotuhumiwa
Boniface Meena
SAKATA la ufisadi ulioanikwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), limeingia sura mpya baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuanza kuwachunguza watendaji wote waliohusika, wakiwamo mawaziri.
Hatua hiyo ya Takukuru imekuja wakati tayari Kamati Kuu (CC) ya CCM imebariki uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kulisuka upya Baraza la Mawaziri kama hatua mojawapo katika kutekeleza maazimio ya Bunge kutaka mawaziri wanane na watendaji waliotajwa katika ripoti ya CAG wawajibishwe.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema jana kuwa pamoja na hatua ya Rais ya kufanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri, taasisi hiyo imeanza uchunguzi wake dhidi ya wahusika.
Dk Hoseah alisema ofisi yake imeshaanza kushughulikia tuhuma zote za rushwa zilizotolewa na CAG na baadaye kupigiwa kelele na wabunge ili watakaobainika wafikishwe kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
“Sheria inatutaka tufanye uchunguzi wa tuhuma zozote na katika hili, CAG alitakiwa atupe taarifa. Lakini sisi baada ya kusikia bungeni tulimwandikia barua (CAG) kumwomba atupatie ripoti ya mambo yanayotuhusu tuanze kuyashughulikia haraka,” alisema Dk Hoseah.
Hata hivyo, Dk Hoseah alisema asingeweza kuwataja watu wanaowachunguza kwa majina, kwa kuwa sheria (Kifungu cha 37 cha Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007, kinazuia kuzungumzia mchakato wa uchunguzi).
Lakini, mawaziri waliotajwa katika ripoti hiyo ya CAG na hivyo kushinikizwa kujiuzulu ni William Ngeleja wa Nishati na Madini na Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu.
Wengine ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika; Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami.
“Siwezi kusema tunamchunguza nani kwani sheria hairuhusu ila elewa tu kwamba tuko serious (makini) na tunafanyia kazi tuhuma zote na wote tutahakikisha tunawafikia,” alisema Dk Hoseah.
CAG akiri
Kwa upande wake CAG, Ludovick Utouh alikiri kuwasiliana na Takukuru kuhusu kuwachunguza wote waliotajwa katika ripoti yake.
“Kimsingi ofisi yangu inafanya kazi kwa karibu na Takukuru na barua waliyotuandikia tunaendelea kuifanyia kazi. Sheria inatueleza kwamba katika ukaguzi wetu, tunapokutana na suala lolote la rushwa tuliwasilishe Takukuru na tumekuwa tukifanya hivyo,” alisema Utouh.
Awali, wakati sakata hilo likiwa bungeni, kuliibuka malumbano ya hapa na pale miongoni mwa mawaziri na wasaidizi wao huku watendaji hao wa wizara, wakitupiana mpira kuhusu kashfa mbalimbali zinazoelekezwa kwenye ofisi zao.
Kashfa za mawaziri
Waziri Nundu na Naibu wake, Athuman Mfutakamba kwa upande mmoja na Waziri Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu walianza kutupiana mpira huku kila mmoja akijisafisha kiaina.
Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu katika utetezi wake alisema Naibu wake huyo amekuwa akishinikiza Kampuni ya China Communication Construction Company (CCCC), ipewe kazi ya kujenga gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa ilimgharamia safari kadhaa kwenda nje.
Waziri Nundu pia alishangazwa na shinikizo la Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu chini ya Mwenyekiti wake, Peter Serukamba kuingia na kushinikiza CCCC ipewe kazi hiyo huku akihoji kuna nini?
Hata hivyo, Mfutakamba alipoulizwa kuhusu safari zake hizo za nje kugharamiwa na CCCC na baadaye kuandika ripoti akishinikiza ipewe kazi ya kujenga gati hizo, alikiri kusafirishwa na kampuni hiyo, lakini akasema alifuata taratibu zote za kiserikali.
Nyalandu kwa upande wake, alionekana kutua mzigo wa kashfa ulioigubika wizara hiyo ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege kudaiwa kuiingizia Serikali hasara ya karibu Sh30 milioni kwa ukaguzi hewa wa magari nje ya nchi akisema alimshauri Waziri wake, Dk Chami kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo mapema.
Lakini Dk Chami alisema hadi Bunge linamalizika mjini Dodoma, alikuwa hajaiona ripoti ya Kamati ndogo ya Bunge iliyomchunguza Ekelege ambayo alisema ingemsaidia kupata tuhuma zinazomkabili mkurugenzi huyo ili kuchukua hatua.
Mkulo ambaye alikuwa waziri wa kwanza kutakiwa ajiuzulu, anatuhumiwa kuvunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ili kuficha tuhuma zake ikiwemo uuzaji wa kiwanja Na.10 kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL).
Mkuchika alitakiwa aachie ngazi baada ya ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) kubaini mtandao mkubwa wa wezi wa mali za umma. Ripoti hiyo ilibainisha kuwa kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2010, Sh583.2 milioni zililipwa kama mishahara hewa, kiasi ambacho kingetosha kujenga madarasa 194.
Ripoti ya CAG ilibaini kuwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa mwaka mmoja wa fedha linafanya ununuzi wenye thamani ya Sh300 bilioni hadi Sh600bilioni, hivyo kumtaka Waziri Ngeleja awajibike.
Katika mwaka wa fedha 2009/2010, Tanesco ililitumia Sh1.8bilioni ukilinganisha na Sh65 milioni zilizokuwa zimepangwa katika bajeti ya ukarabati wa gati mojawapo katika Kituo cha Bwawa la Mtera na kuingia mikataba isiyo na tija kwa taifa.
Waziri Maige anakabiliwa na tuhuma za kutengeneza mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji, ambao inadaiwa ulitawaliwa na dosari nyingi ikiwa ni pamoja na kutangaza majina ya waliopata vitalu bila kuonyesha maeneo waliyopewa.
Pia, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi na Maliasili ilieleza kuwa kampuni 16 zilizopewa vitalu hivyo hazikuomba na kwamba vitalu hivyo vilikuwa vya daraja la kwanza na la pili.
Mbali na tuhuma hizo, Maige pia anakabiliwa na kashfa ya kununua nyumba kwa Dola za Marekani 700,000 iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam, tuhuma ambazo alizipinga na kusema kuwa nyumba hiyo ameinunua kwa Dola 410,000, (wastani wa Sh600 milioni).
Waziri Mponda ametakiwa kuwajika baada ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ambako ukaguzi maalumu wa MSD uliofanyika kubaini kuwapo tofauti ya Sh658.9 milioni ikiwa ni pungufu ya kiasi ambacho kilipokewa na kuripotiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwenda MSD na ushahidi wa kupokewa haukutolewa.
Pia kulikuwa na kiasi cha Sh100 milioni kilichopelekwa na MSD kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kikatumiwa na MSD bila kuwapo na mchanganuo wa matumizi.
Ukaguzi maalumu ulibaini pia kuwapo kiasi cha Sh4.5 bilioni zilizotoka Hazina kwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa vya hospitali, lakini ni kiasi cha Sh4.344 bilioni tu kilichopokewa na MSD ikiacha Sh196 milioni bila kuwepo na ushahidi wa kupokewa na MSD kutoka wizarani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment