Advertisements

Tuesday, May 1, 2012

Wafanyakazi wampa JK kilio cha mishahara


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwasalimia wafuasi wa CUF waliofika kumlaki Uwanja wa Ndege Tanga, jana. Rais Kikwete yupo mjini hapa kuhudhuria sherehe za Mei Mosi zinazofanyika leo. Picha na Ikulu
Waandishi wetu
WAFANYAKAZI nchini leo wanaungana na wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi), huku wakieleza kilio chao kuwa ni ukubwa wa viwango vya kodi ya mapato (PAYE) na kiwango kidogo cha mishahara ikilinganishwa na ongezeko la mfumuko wa bei.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana walisema watapeleka kilio hicho kwa Rais Jakaya Kikwete leo katika maadhimisho ya sherehe hizo ambazo yeye atakuwa mgeni rasmi. Maadhimisho ya Sikukuu ya Mei Mosi yanafanyika kitaifa mjini Tanga.

Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (Tucta) limesema mshahara mdogo, mfumuko wa bei na viwango vikubwa vya kodi ni moja ya changamoto zinazowakabili wafanyakazi nchini ambayo inafanya washindwe kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Nicolaus Mgaya alisema kutokana na hali hiyo Serikali ina jukumu la kuhakikisha kuwa inaboresha mishahara ya wafanyakazi ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Alisema kitendo cha kulipwa mishahara midogo kinachangia wafanyakazi kushindwa kuwajibika, jambo ambalo linaweza kusababisha uchumi wa nchi kuporomoka.

“Wafanyakazi ni tabaka kubwa, lakini ndio wanaoongoza kwa umaskini. Hii inatokana na kulipwa mishahara midogo, kukatwa kodi kubwa NA mifuklo ya jamii kuwakamua hadi mwisho. Kutokana na hali hiyo Serikali inapaswa kusikiliza kilio chao na kukifanyia kazi,” alisema Mgaya.

Aliongeza, "Mbali na matatizo hayo, kitendo cha Serikali kushindwa kudhibiti mfumuko wa bei kimezidi kuwakandamiza wafanyakazi hao na kuwaweka katika hali ngumu kimaisha."

Kwa mujibu wa Mgaya, Serikali inaweza kuwasaidia wafanyakazi hao kwa namna mbili, kudhibiti mfumuko wa bei, kupunguza kodi kwenye mifuko ya jamii na makato pamoja na kuongezewa  mishahara.

Alisema kila mwaka wafanyakazi wamekuwa wakilalamikia nyongeza hiyo ambayo mpaka sasa Serikali imeshindwa kutekeleza na kwamba inachokifanya Tucta ni kuhakikisha kuwa wanaishauri Serikali ili iweze kutekeleza.

Alifafanua kwamba mwaka 2007, Tucta ilifanya tathmini ya kubaini kipato cha mfanyakazi na kutoa mapendekezo yake, huku ikiitaka  Serikali kuongeza kima cha chini cha mishahara hadi Sh315,000 badala ya Sh150,000.

Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema walimu wana kero nyingi ambazo hazijapatiwa ufumbuzi hivyo sherehe hizo za Mei Mosi zinafaa kutumika kama chachu ya kuangalia matatizo hayo na kuyapatia ufumbuzi.

“Kesho (leo) Rais atahutubia kwenye sherehe hizo, ningependa kwanza nimsikilize anachosema ili tujue nini hajakigusia halafu tuwe katika mazingira mazuri ya kuzungumza. Lakini kilio chetu ni kero nyingi zinazowakabili walimu," alisema.

Rais huyo alisema wanaisubiri kwa hamu kubwa hotuba ya Rais Kikwete na wanataka kuona iwapo ina majibu au majawabu ya kero na madai yao ya muda mrefu, “tunataka kusikia iwapo ana majibu au majawabu,” alisema Mukoba ambaye alibainisha kuwa jawabu ni suluhisho la muda mrefu na jibu ni suluhisho la muda.


Mukoba alisema kuwa anawaunga mkono walimu wa Manispaa mbili za Kinondoni na Ilala kugoma kushiriki sherehe za Mei Mosi kutokana na serikali  kuzidi kuwadharau walimu.


Alisema uongozi wa CWT, unasubiri hotuba za viongozi wa Serikali baada ya sherehe hizo ili waitathimini na kuona kama italenga kupunguza  matatizo ya walimu, vinginevyo watajipanga kujikomboa wenyewe.

Kwa upande wa baadhi ya walimu waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti walisema kuwa wamechoshwa na manyanyaso na Serikali kwa kushindwa kuwapa madai yao muhimu badala yake wamekuwa wakitishiwa wanapotaka kugoma.

Awali, Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliahidi kulipa fedha hizo kati ya Novemba na Desemba mwaka jana, lakini hadi sasa haijafanya hivyo na madai hayo ni tofauti na megine 13 ambayo yamepata kuanishwa na Umoja wa Maofisa Elimu Tanzania (UMET).

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa Mkwakwani leo asubuhi ili kumsikiliza Rais Kikwete.

Alisema Mkoa wa Tanga ulichaguliwa kuwa mwenyeji wa sherehr hizo mwkaa huu kutokana na historia ya mkoa huo ikiwa ni pamoja na kuwa na mashamba makubwa ya Mkonge na chai.

Imeandaliwa na Joseph Zablon, Gedius Rwiza na Patricia Kimelemeta, Dar, Burhani Yakub na Steven William, Tanga.


Mwananchi

No comments: