RAIS wa zamani wa Liberia, Charles Taylor amehukumiwa kifungo cha miaka 50 jela na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai iliyopo The Hague, Uholanzi.
Hukumu ya mwanasiasa huyo anayejulikana kama ‘Bwana wa Vita’, ilitolewa baada ya mahakama hiyo kuridhishwa na ushahidi kuwa alihusika kuwaficha, kuwasaidia na kupanga mikakati na waasi waliokuwa wakifanya vitendo vya unyanyasaji na utesaji wakati wa utawala wake.
Akisoma hukumu yake jana, Jaji wa mahakama hiyo, Richard Lussick, alieleza kuwa Taylor anastahili adhabu hiyo ya kifungo cha muda mrefu ili iwe fundisho kwa viongozi wengine wa kada yake wanaojihusisha na makosa ya jinai kama hayo.
Habari kutoka mahakama hiyo zinasema kuwa kutokana na ukubwa wa kosa, waendesha mashitaka wa mahakama hiyo walipendekeza afungwe kifungo cha miaka 80 au zaidi, lakini kimepunguzwa na jaji huyo.
Taylor ni rais wa kwanza kupatikana na hatia na kuhukumiwa na Makahama ya Kimataifa tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia. Mwanasiasa huyo wa zamani ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 64, anatarajia kumalizia miaka ya uhai wake gerezani.
Taarifa kutoka katika mahakama hiyo zinaeleza kuwa wakati akisomewa hukumu aliamriwa kusimama, alitii lakini wakati wote alikuwa ameinamisha uso wake chini huku akiwa kimya.
Baada ya hukumu kutolewa, wanasheria wake walieleza nia yao ya kukata rufaa kwa madai kwamba adhabu hiyo ni kubwa na haikuzingatia hali halisi ya mteja wao kama vile afya na umri wake.
“Mahakama hiyo ilipaswa kuzingatia ukweli kwamba kiongozi huyo aliondoka madarakani kwa utashi hivyo ilipaswa kumtendea haki kwa kuzingatia ukweli huo,” alieleza Morris Anya ambaye ni mwanasheria aliyekuwa akimwakilisha mahakamani hapo.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment