MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA (NIDA)
YAH: FOMU ZA USAJILI ZA VITAMBULISHO VYA TAIFA, ZAUZWA KATIKA BAADHI YA MIKOA NCHINI
Kumekuwepo taarifa kwenye baadhi ya mikoa nchini, kwamba fomu za usajili na utambuzi wa watu zenye lengo la kuchukua taarifa za wananchi na hatimaye kuwapatia Kitambulisho cha Taifa, kuanza kuuzwa kinyume na taratibu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ndugu Dickson E. Maimu, vitendo hivyo vimebainika kufuatia taarifa toka kwa wasamaria wema walioshuhudia fomu hizo zikiuzwa kwa wananchi.
Amesema vitendo hivi vinalenga kuwahadaa wananchi na hivyo kuwataka wawe waangalifu na kuwafichua wale wote wanaojihusha na uuzaji huu, ambao ni kinyume cha taratibu, kanuni na Sheria ya Usajili.
Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA), haijaanza kutoa fomu zozote za usajili kwa wananchi wa mikoani, zaidi ya mazoezi ya usajili kwa watumishi wa Umma kwa Dar-as-salaam, na Zanzibar, na zoezi la majaribio wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro lililofanyika mwezi Machi mwaka huu. Usajili rasmi wa wananchi kwa jumla unakusudiwa kuanza mapema mwezi Juni mwaka huu, kwa kuanzia na mkoa wa Dar-es-salaam.
Kwa mujibu wa taratibu zilizoko, Mamlaka ya Vitambulisho inasisitiza Fomu za Utambuzi na Usajili wa Watu ni BURE na HAZIUZWI, aidha kitambulisho pia kitatolewa bure kwa Wananchi, hivyo wananchi wasikubali kununua fomu mtaani. Utaratibu wa ugawaji fomu utatangazwa kwa wananchi hicho wakati utakapowadia kupitia vyombo vya habari.
Wananchi mnaombwa yeyote atakaye baini au kuwa na taarifa ya vitendo hivi kutoa taarifa kwenye kituo chochote cha polisi kilichoko karibu.
Mamlaka inawasihi wananchi mikoani kuwa watulivu kipindi hiki wakisubiri kuanza kwa usajili katika mikoa yao na kwamba NIDA itakuwa ikitoa taarifa za mara kwa mara kwa wananchi ili kujiandaa na usajili katika maeneo yao husika.
Dickson E. Maimu
MKURUGENZI MKUU
Mamlaka ya Vitambulisho Vya Taifa
22 / 05 / 2012
No comments:
Post a Comment