ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 18, 2012

UMESHINDWA KUWA MWAMINIFU KWA MPENZI WAKO? - 4

NI Ijumaa nyingine tunakutana tena katika safu yetu ya Let’s Talk About Love. Lengo ni lile lile, kupeana mawazo mapya ya namna ya kuboresha uhusiano. Nina imani mtakuwa wazima wa afya njema na mpo tayari kujifunza kitu kipya.
Tunaendelea kuangalia namna ya kuweza kuwa katika uaminifu wa kweli kwa mpenzi wako. Kama mtakumbuka, katika matoleo ya mwanzoni nilisisitiza kwamba,suala la uaminifu limo ndani ya mtu lakini wakati mwingine ni jambo linalohitaji juhudi binafsi za mtu.

Yapo mambo ambayo kama hutakuwa nayo makini, unaweza kujikuta umeingia kwenye usaliti, lakini moyo wako ukiwa na maumivu kutokana na uamuzi huo ambao utakuacha na majuto makubwa.
Hebu sasa twende tukaone katika sehemu hii ya mwisho. Karibuni sana darasani marafiki.
MARAFIKI
Marafiki ni kiungo muhimu sana katika maisha ya binadamu aliyekamilika. Hawa ndiyo washauri wakubwa, ndiyo wa kuwaeleza (wakati mwingine) siri zako hata zile za ndani. Habari mbaya ni kwamba, marafiki wana uwezo mkubwa wa kuharibu!
Kama ukikosea katika kuchagua marafiki sahihi ni tatizo. Angalia wale ambao mnaendana kitabia. Achana na marafiki wenye tabia za hovyo. Mfano walevi, wahuni, wenye tabia za kuchanganya wapenzi n.k
Watakusaidia nini zaidi ya kukufundisha ujinga? Ni vizuri pia kama utazingatia ‘type’ yako. Mfano, utakuta msichana mdogo, ana urafiki na mama mtu mzima! Atakupa mawazo gani? Mfano, kama umeoa au kuolewa ni vizuri sasa kuchagua marafiki ambao nao wana familia. Hawa watakupa msaada mkubwa wa mawazo na kubadilisha uzoefu kuhusu familia. Huu ndiyo ukweli.
JIVUNIE UHUSIANO WAKO
Ili uweze kujidhibiti katika suala la uaminifu, pia vyema kama utajijengea tabia ya kujivunia mpenzi wako. Hata unapokuwa na marafiki zako, sema unampenda sana mpenzi wako, unajiona mwenye bahati kuwa wake n.k
Hata kama kuna mtu alikuwa anakuzengea au kuna mtu alitumwa kukuchunguza, atakutana na majibu tofauti kabisa kutoka kwako. Kushawishiwa kimapenzi ni jambo moja lakini kuingia kwenye usaliti ni jambo lingine.
Yote kwa yote, mwanzo ni ushawishi, sasa kama ukiweka kinga ya kushawishiwa, inakuwa si rahisi sana kuingia kwenye mtego. Tetea uhusiano wako mwenyewe.
ACHA KUSHABIKIA USALITI
Uaminifu unaanzia moyoni, ni vile unavyouweka moyo wako. Ukianza mambo ya kushabikia mtu anayesaliti kwa kumuona mjanja, maana yake utakuwa unaukubali usaliti ndani ya moyo wako bila kujua.
Utakuja kushtuka, tayari umeshachelewa. Upo chimbo na patna mwingine ukimsaliti mpenzi wako. Utabaki na maumivu yako, lakini ukweli utabaki vile vile kuwa umeshasaliti!
ISHI KATIKA IMANI
Hii ni nguzo kubwa zaidi kuliko zote. Kuwa ndani ya imani na kufuata maagizo yake, kutafuta uwe na hofu ya kwenda nje ya mwenzi wako.
Je, unaiamini imani yako kikamilifu? Kama ndivyo, jiulize, inakuruhusu kufanya usaliti? Bila shaka hapana. Hakuna imani yoyote inayoruhusu watu kutokuwa waaminifu. Uaminifu ni kati ya nguzo muhimu sana za imani.
Hata wapagani nao wanaamini katika uaminifu. Ndiyo...wapagani hawaruhusiwi kuiba! Jijenge kwenye imani yako, itakusaidia kuwa mbali na usaliti.
KAZI NI KWAKO
Naam! Sasa imebaki kazi kwako, kuamua kuwa mwaminifu au kutokuwa mwaminifu kwa mwenzako. Si kazi kubwa sana kuwa mwaminifu ikiwa ndani ya moyo wako unapenda iwe hivyo.
Baada ya nia ya moyoni mwako, sasa kazi nyingine inayokuhusu ni ile ya kukubali kufanya mambo ambayo yatakufanya uwe katika himaya ya uaminifu. Uamuzi uko mikononi mwako!
Naweka kituo kikubwa hapa, hadi wiki ijayo kwa mada nyingine itakayokuacha na mafunzo makubwa, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is Your Valentine? vilivyopo mitaani.

No comments: