MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo ametoa siku 14 kwa watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema wanaokabiliwa na tuhuma za kufuja fedha za umma kujibu tuhuma hizo kwa barua kwa Kamati ya Nidhamu ya Baraza la Madiwani.
Amesema wasipojibu tuhuma hizo ndani ya muda huo baada ya kuandikiwa barua na kamati hiyo juu ya tuhuma zinazowakabili ambazo zimeripotiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wataburutwa mahakamani.
Mbali na watumishi hao 25, pia ameliagiza Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Sengerema kutoa uamuzi wa haki kwa watumishi wote waliotuhumiwa kufuja fedha za halmashauri hiyo.
Agizo hilo la Mkuu wa Mkoa lililotolewa juzi, limekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kubadili Baraza la Mawaziri kutokana na baadhi yao kutuhumiwa kwa kashfa mbalimbali ikiwemo usimamizi duni wa wizara zao.
Ripoti hiyo ya CAG, ilibaini ubadhirifu mkubwa wa fedha za halmashauri hiyo zaidi ya Sh bilioni mbili zilizotajwa kutumika kinyume cha maelekezo ya Serikali huku baadhi ya watuimishi wakishindwa kusimamia idara zao.
Idara zilizobainika kuwa na ubadhirifu wa fedha hizo zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni Idara ya Ununuzi na Ugavi, Fedha, Ardhi, Kilimo, Maji, Ujenzi na Bodi ya zabuni.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuzungumza na madiwani na kutoa maelekezo ya yanayotokana na taarifa ya CAG, Ndikilo alisema kuwa watendaji 25 amewapa siku 14 kujieleza.
Aliwataka madiwani kutumia mwanya huo kuisafisha halmashauri yao kutokana na kukithiri kwa ubadhirifu wa fedha na kuwafananisha watumishi waliohusika katika upotevu wa fedha hizo na mdudu ajulikanaye kwa jina la dumuzi.
Akifafanua namna fedha zilivyotumika vibaya, Ndikilo alisema ni pamoja na ukiukwaji wa ununuzi unaofikia thamani ya Sh milioni 733.9, usimamizi dhaifu na matumizi mabovu ya Sh milioni 749.3.
Pia ukiukwaji wa malipo ya Sh bilioni 1.4, hali iliyosababisha halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka katika miaka miwili mfululizo ya 2009/2010 na 2010/2011.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment