ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 2, 2012

Wavulana watamba kidato cha sita


Katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa Joyce Ndalichako akitangaza matokeo ya kidato cha sita jijini Dar es Salaam jana.Picha na Emmanuel Herman
Leon Bahati
BARAZA la Mtihani la Tanzania (Necta), limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha sita iliyofanyika Februari mwaka huu yakionyesha kuongezeka kidogo kwa kiwango cha ufaulu kwa ujumla huku wavulana waliofaulu wakiwaacha mbali wasichana.

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako, kati ya watahiniwa 46,499 waliofanya mtihani huo,  wavulana waliofaulu ni 30,466 wakati wasichana ni 16,033. Hata hivyo, kumekuwa na mchuano mkali katika ufaulu kwa asilimia ambao wasichana walipata 87.37 na wavulana 87.69.

Sekondari ya Wasichana ya Marian, Bagamoyo ndiyo iliyoongoza kitaifa na mwanafunzi wake, Faith Assenga ndiye aliyeshika namba moja katika masomo ya Sayansi.

“Katika masomo ya Biashara, aliyeshika nafasi ya kwanza ni Alex Isdor wa Sekondari ya Kibaha na Lugha ni Faridi Abdallah wa Sekondari ya Mpwapwa,” alisema Dk Ndalichako.

Dk Ndalichako alisema kiwango cha kufaulu kwa watahiniwa 46,499; wakiwemo wale wa kujitegemea, kimeongezeka kutoka asilimia 87.24 mwaka jana hadi 87.58 mwaka huu.

Hata hivyo, alisema mwaka huu watahiniwa wa shule wameanguka katika masomo ya kemia, hisabati ya msingi, uchumi na maarifa ikilinganishwa na mwaka jana.

“Masomo ambayo wanafunzi walifanya vizuri zaidi ni Historia, Jiografia, Kiswahili, Kiingereza, Fizikia, Elimu ya Mimea, Biashara, Uhasibu na Hisabati daraja la juu," alisema.

Shule Bora

Dk Ndalichako alisema Necta imezigawa shule zilizofanya vizuri katika makundi mawili; zenye watahiniwa zaidi ya 30 na zenye watahiniwa chini ya 30.

“Kwa shule zenye watahiniwa 30 au zaidi, sekondari 10 zilizofanya vizuri zaidi ni Marian (wasichana) ikifuatiwa na Feza (wavulana), Kisimiri, Kibaha, Ilboru, Mzumbe, Msalato, Tabora (wavulana), St. Mary's Mazinde Juu na Consolata Seminari.

Sekondari zilizofanya vibaya zaidi katika kundi la shule hizo ni Pemba Islamic, Zanzibar Commecial, Kongwa, Uweleni, Mazizini, Lumumba, Ben Bela, Mlima Mbeya, Laurate International na Haile Selassie.

Sekondari iliyoongoza kwa kufaulu katika kundi la shule zenye watahiniwa chini ya 30 ni Uru Seminari ikifuatiwa na Iwawa, Maua Seminari, Harrison Uwata, Beroya, Palloti, Lutengano, Makita, Mwanga na Visitation (wasichana).

Sekondari zilizofanya vibaya zaidi kwenye kundi hilo ni Mbarali Preparatory, Philter Federal International, High-View International, Kifai Modern, Sha, Dar es Salaam Prime, Kandoto Sayansi, Popatlal, Al-Falaah Muslim na Kiuma.

Wanafunzi bora

Dk Ndalichako alisema mwaka huu walishindanisha ubora wa watahiniwa kwa kuzingatia aina ya masomo wanayochukua.

Katika kundi la wanafunzi bora kwenye Sayansi lililoongoza na Faith, aliyefuata ni Zawadi Mdoe (Feza), Belnadino Mgimba (Minaki), Jamal Juma (Feza) na Imaculate Mosha (Marian).

Watano waliofanya vizuri katika masomo ya Biashara wakiongozwa na Alex ni Ephraim Tumwidike (St Joseph's Cathedral), Vaileth Mussa (Weruweru), Seleman Manyiwa (Kibaha) na Hussein Issa (Azania).

Katika masomo ya Lugha na Sayansi ya Jamii aliyemfuata Faridi ni Jema Rwihura (Weruweru), Mariam Hincha (Weruweru), Neema Mbandwa (Igawilo) na Hemed Hussein (Tosamaganga).

Wasichana watano bora kwa masomo ya Sayansi, wote wametoka Marian ambao ni Faith Immaculate Mosha, Rachel Sigwejo, Mary Kiangi na Nashival Kivuyo.

Wavulana bora katika Sayansi ni Zawadi, Belnadino, Jamal Juma (Feza), Gwamaka Njobelo na Nickson Mwamsojo; wote kutoka Mzumbe.

Wasichana waliofanya vizuri zaidi katika masomo ya Biashara, nafasi ya kwanza hadi ya nne ilichukuliwa na wanafunzi wa Weruweru, ambao ni Vaileth, Gloria Murro, Stella Richard na Helen Komba. Nafasi ya tano ilichukuliwa na Veronica Sauli wa St. Antony.

Wavulana waliofanya vizuri katika masomo ya biashara ni Alex, Aphraim, Suleiman, Hussein na Ally Katala wa Azania.

Wasichana watano waliofanya vizuri masomo ya Lugha na Sayansi ya Jamii ni Jema, Mariam, Neema Mbandwa (Igawila), Angel Ruhumbika (Loreto) na Jaquline Chambua (St. Mary's Mazinde Juu).

Wavulana waliofanya vizuri katika masomo ya Lugha na Sayansi ya Jamii ni Faridi, Hemed, Elibaraka Mmari (Lyamongo) na Salvatory Kessy (Majengo).

Matokeo yaliyozuiwa

Dk Ndalichako alisema watahiniwa sita, watatu kati yao wakiwa wa kujitegemea walifutiwa matokeo yao baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu.

Alisema pia Necta imezuia matokeo ya watahiniwa 51 ambao kwa mujibu wa kumbukumbu zao hawajalipa ada ya mtihani.Dk Ndalichako alisema matokeo yao yatatolewa na Necta pindi watakapokamilisha taratibu za malipo hayo.

Sekondari 10 Bora
1. Marian (wasichana) - Pwani
2. Feza (wavulana)      - Dar es Salaam
3. Kisimiri                   - Arusha
4. Kibaha                     - Pwani
5. Ilboru                       - Arusha
6. Mzumbe                   - Morogoro
7. Msalato                         - Dodoma
8. Tabora (wavulana)         - Tabora
9. St. Mary's Mazinde Juu - Tanga
10. Consolata Seminari      - Iringa

Wanafunzi 5 bora Sayansi

1. Faith Assenga  - Marian
2. Zawadi Mdoe  - Feza
3. Belnadino Mgimba  - Minaki
4. Jamal Juma  - Feza
5.Imaculate Mosha  - Marian

Wanafunzi 5 bora biashara

1. Alex Isdor -Kibaha
2. Ephraim Tumwidike - St Joseph's Cathedral
3. Vaileth Mussa -Weruweru
4. Seleman Manyiwa -Kibaha
5. Hussein Issa - Azania

5 bora Lugha na Sayansi ya Jamii

1. Faridi Abdalla - Mpwapwa
2. Jema Rwihura - Weruweru
3. Mariam Hincha - Weruweru
4. Neema Mbandwa - Igawilo
5. Hemed Hussein - Tosamaganga

Mwananchi

No comments: