Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa akionyesha mkoba wenye bajeti huku akiwa ameongozana na Naibu Waziri, Janet Mbene.
1 UTANGULIZI:
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liweze kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Pamoja na hotuba hii, nimewasilisha vitabu vinne vya Bajeti vinavyoelezea takwimu mbalimbali za Bajeti. Kitabu cha Kwanzakinaelezea makisio ya mapato. Kitabu cha Pili kinaelezea makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea; Taasisi na Wakala wa Serikali; cha Tatu kinahusu makisio ya matumizi ya kawaida kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na cha Nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2012 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2012 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nitumie fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Naahidi kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Naahidi kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa mawaziri kama ifuatavyo: Mhe. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo (Mb); Mhe. Mhandisi Christopher Kajoro Chiza (Mb); Mhe. Dkt. Harrison George Mwakyembe (Mb); Mhe. Dkt. Fenella Ephraim Mukangara (Mb); Mhe. Balozi Khamis Sued Kagasheki (Mb); Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda (Mb). Aidha, napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa kuwa naibu mawaziri katika Wizara mbalimbali, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb); Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb); Mhe. Dkt. Seif Suleiman Rashid (Mb.); Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb.); Mhe. January Yusuf Makamba (Mb.); Mhe. Dkt. Charles John Tizeba (Mb.); Mhe. Amos Gabriel Makalla (Mb.); Mhe. Angela Jasmine Kairuki (Mb.); Mhe. Stephen Julius Maselle (Mb.); na Mhe. Mhandisi Dkt. Binilith Satano Mahenge (Mb). Kadhalika, nampongeza Mhe. James Mbatia (Mb) kwa kuteuliwa na Mhe. Rais kuwa Mbunge.
4. Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia, Mhe. Alhaji Adam Kimbisa (Mb.); Mhe. Shy Rose Banji (Mb.); Mhe. Abdulah Alli Hassan Mwinyi (Mb); Mhe. Charles Makongoro Nyerere (Mb); Mhe. Dkt Twaha Issa Taslima (Mb); Mhe. Nderkindo Perpetua Kessy (Mb); Mhe. Bernard Musomi Murunyana (Mb); Mhe. Anjela Charles Kizigha (Mb.); Mhe. Maryam Ussi Yahaya (Mb.), ambao wamechaguliwa kutuwakilisha kwenye Bunge la Afrika Mashariki. Ni matumaini yangu watatuwakilisha vyema kwa maslahi na manufaa ya Taifa letu.
5. Mheshimiwa Spika, maandalizi ya Bajeti hii yamehusisha wadau na Taasisi mbalimbali. Napenda kuwashukuru walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha matayarisho yake. Kwa namna ya pekee, ninaishukuru Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi chini ya uenyekiti wa Mhe. Mtemi Andrew John Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi, pamoja na kamati nyingine za kisekta kwa ushauri mzuri waliotoa wakati wakichambua mapendekezo ya Bajeti hii. Aidha, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushauri na mapendekezo yao ambayo yamezingatiwa katika Bajeti hii.
6. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mhe. Stephen Masatu Wasira (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kwa ushirikiano alionipatia wakati wa maandalizi ya Bajeti. Aidha, nawashukuru Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb) na Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb). Namshukuru Katibu Mkuu Ndugu Ramadhani M. Khijjah; Naibu Katibu Wakuu, Ndugu Laston T. Msongole; Dkt. Servacius B. Likwelile; na Ndugu Elizabeth Nyambibo kwa mchango wao mkubwa katika matayarisho ya Bajeti. Vilevile, nawashukuru Prof. Benno Ndulu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania; Dkt. Phillip Mpango, Katibu Mtendaji Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango; Ndugu Harry Kitilya, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania; na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa. Nawashukuru wote kwa mchango wao katika maandalizi ya bajeti hii. Naishukuru pia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 na nyaraka mbalimbali za sheria ambazo ni sehemu ya Bajeti hii.
7. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Wakuu wa Idara, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha kwa ushirikiano wao. Aidha, namshukuru Mpigachapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha Hotuba hii kwa wakati. Nawashukuru pia wataalamu na wale wote waliotoa mapendekezo kuhusu sera, mikakati na masuala mbalimbali ya kodi ambayo yamezingatiwa katika kuandaa Bajeti hii.
8. Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa mwenyeji wa Mikutano ya Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa Mwaka 2012 iliyofanyika kuanzia tarehe 28 Mei hadi tarehe 2 Juni 2012 na kufunguliwa rasmi na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mikutano hii ilifanyika kwa ufanisi mkubwa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha na kuhudhuriwa na washiriki 2,350 kutoka ndani na nje ya Tanzania. Hii imekuwa ni nafasi ya kipekee kwa Tanzania kutangaza fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini. Aidha, washiriki wa ndani kutoka sekta binafsi walipata nafasi ya kufahamu fursa za mikopo zilizopo katika Benki ya Maendeleo ya Afrika. Napenda kutoa wito kwa sekta binafsi kutumia fursa hizo kikamilifu.
9. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2012/13 imelenga kukabiliana na changamoto zinazokabili uchumi ikiwa ni pamoja na; kuongeza fursa za kukuza uchumi, kushughulikia uhaba wa chakula nchini, kupambana na mfumuko wa bei, kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kusimamia matumizi, kushughulikia suala la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, kuwekeza katika miundombinu ya nishati ya umeme hususan ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, barabara, bandari na reli ya kati ili kupunguza gharama za kufanya biashara na kuongeza tija katika uzalishaji; pamoja na kulipa madeni ya ndani na nje.
II. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA
MWAKA 2011/12
10. Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/12. Mfumo wa Bajeti ya mwaka 2011/12 uliendeleza juhudi za Serikali za kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Aidha, bajeti ilizingatia utekelezaji wa vipaumbele vya Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16); Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA); Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; Mkakati wa Taifa wa Madeni; pamoja na kuimarisha usimamizi wa kodi na matumizi ya fedha za Umma.
11. Mheshimiwa Spika, misingi na shabaha za bajeti ya mwaka 2011/12, pamoja na mambo mengine, ililenga kukamilisha malengo ya Serikali ya kukabiliana na changamoto za kupunguza makali ya maisha kwa wananchi; kuendelea kuboresha mfumo wa makusanyo ya mapato ya ndani; kuboresha mazingira ya uwekezaji wa ndani na nje; kuendeleza sekta binafsi ili kupanua wigo wa kodi; kukamilisha maandalizi ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa; na kutenga rasilimali na kutekeleza miradi katika maeneo ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
12. Mheshimiwa Spika, maeneo mengine yaliyozingatiwa katika misingi na shabaha ya bajeti hiyo yalikuwa ni: kutekeleza mipango na mikakati maalum ya kuharakisha ukuaji wa uchumi; kutafuta mikopo ya masharti nafuu na ya kibiashara; kuharakisha utekelezaji wa Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na ya Binafsi ili kupanua fursa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo; Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012; kuhakikisha kwamba maduhuli ya Serikali yanakusanywa ipasavyo na kuwasilishwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali; pamoja na kulinda na kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika Sekta za huduma za jamii, hususan elimu na afya ambazo zimekuwa na upanuzi mkubwa wa huduma.
Hatua za Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/12
Kupunguza Makali ya Maisha
13. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/12, Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi kwa lengo la kupunguza makali ya maisha kunakotokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na: kurekebisha namna ya kukokotoa gharama za mafuta na kutangaza bei elekezi kila mwezi na kuanzisha utaratibu wa uagizaji mafuta kwa pamoja (bulk procurement). Hatua hizi zimesaidia kupunguza kasi ya upandaji wa bei ya mafuta hapa nchini.
14. Mheshimiwa Spika, Serikali imetumia shilingi bilioni 296 kutekeleza mpango wa dharura wa kukabiliana na tatizo la upungufu wa nishati ya umeme kwa kutumia mitambo ya kukodi. Utekelezaji wa jitihada hizi umeongeza megawati 324 kwenye Gridi ya Taifa. Kadhalika, Serikali ilitumia Dola za Marekani milioni 183 kugharamia ujenzi wa mitambo ya kufua umeme wa megawati 100 kwa mkoa wa Dar es Salaam mradi ambao umekamilika na uko kwenye hatua za majaribio na Megawati 60 kwa mkoa wa Mwanza ambao bado ujenzi unaendelea.
15. Mheshimiwa Spika, Serikali imetumia shilingi bilioni 27 kugharamia ununuzi na usambazaji wa tani 120,000 za mahindi katika masoko kwa lengo la kukabiliana na uhaba wa chakula kwa baadhi ya maeneo. Aidha, Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari bila kutoza ushuru wa forodha kiasi cha tani 200,000 ili kukabiliana na uhaba na kupanda kwa bei ya sukari. Kadhalika, Serikali ilipandisha kiwango cha riba inayotozwa na Benki Kuu kwa Taasisi za Fedha kutoka asilimia 7.58 hadi asilimia 12.58. Vilevile, Serikali ilipandisha kiwango cha amana ambacho benki za biashara zinapaswa kuhifadhi Benki Kuu kutoka asilimia 20 hadi asilimia 30. Hatua hizi zimesaidia kupunguza kasi ya kupanda kwa bei.
Kuwezesha Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira
16. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na tatizo la ajira, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuongeza fursa za ajira. Hatua hizo ni pamoja na: kuboresha mazingira ya kisera na kisheria kuwezesha sekta binafsi kukua; kupanua huduma za fedha ikiwa ni pamoja na kuongeza mitaji katika Benki ya Rasilimali, Benki ya Wanawake, Benki ya Posta na Twiga Bancorp, na kufanikisha uanzishwaji wa kampuni ya kutoa mikopo ya muda mrefu ya ujenzi wa nyumba na makazi. Hatua nyingine zilizochukuliwa na kuchangia ongezeko la ajira ni pamoja na kujenga miundombinu ya barabara, umeme, kilimo, mawasiliano na kuwezesha wananchi kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji. Aidha, kuna Taasisi mbalimbali ambazo zimechangia kutoa ajira kama vile, TASAF, SELF, VETA, Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO), Taasisi ndogondogo za Fedha, VICOBA, Benki za Kijamii na Mifuko ya Udhamini ya mikopo inayosimamiwa na Benki Kuu. Katika mwaka 2011/12, Serikali iliajiri Walimu wa Shule za Sekondari na Msingi 25,000, Maafisa Ugani wa Kilimo na Mifugo 4,499 na Watumishi wa Kada ya Afya 6,916.
Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Sekta Binafsi
17. Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji mwaka 2011 kufuatia kuidhinishwa kwake mwaka 2010. Kupitia Mpango huu, taratibu na kanuni za mawasilisho na malipo ya kodi na ushuru yanafanyika kwa njia ya mtandao. Utaratibu huu umeongeza ufanisi kwa kuondoa usumbufu na upotevu wa muda katika ulipaji wa kodi. Hadi sasa, zaidi ya asilimia 75 ya walipa kodi wakubwa na walipa kodi wengine 2,795 wanafanya mawasilisho yao kwa njia ya mtandao. Aidha, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianzisha mfumo unaounganisha usimamizi wa kodi (Asycuda, ITAX) na benki za biashara ili kurahisisha ulipaji wa kodi. Mfumo huu umeunganisha jumla ya benki 25. Kadhalika, Mamlaka inatumia huduma za M-Pesa (Vodacom) na “NMB mobile” kwa ajili ya kulipia kodi ya majengo na kodi ya mapato.
18. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na jitihada za kupunguza urasimu katika utoaji wa mizigo bandarini kwa kuanzisha utaratibu wa kuwasilisha nyaraka kwa njia ya mtandao kabla ya mizigo kuwasili. Utaratibu huu umelenga kupunguza tatizo la mrundikano na upotevu wa nyaraka na kupelekea kupungua kwa muda na gharama za uagizaji na usafirishaji mizigo nje ya nchi. Serikali imepunguza vizuizi vya usafirishaji mizigo ndani ya nchi kutoka 50 vilivyokuwepo kufikia 15, isipokuwa vituo vya mizani na forodha. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za kufanya biashara na usumbufu wanaopata wafanyabiashara.
Sera za Mapato
19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali iliendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani yanayotokana na kodi na yasiyo ya kodi kwa kuchukua hatua za kiutawala, kisera pamoja na marekebisho ya viwango vya kodi na sheria.
20. Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 ili kuboresha uzalishaji katika sekta za Kilimo, Mifugo, Viwanda, Biashara na Utalii. Marekebisho hayo ni pamoja na kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vipuri vya zana za kilimo; chakula cha kukuzia kuku; nyuzi za kutengenezea nyavu za kuvulia samaki; pamoja na kuanzisha utaratibu wa kuwarejeshea kodi wageni kwa bidhaa walizonunua nchini wakati wanaondoka.
21. Mheshimiwa Spika, Serikali ilifuta msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye kuuza na kupangisha majengo ya nyumba za kuishi za Shirika la Nyumba la Taifa - NHC; kuondoa unafuu wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali isipokuwa kwenye vifaa vya misaada kwa vituo vya kulelea watoto yatima na shule.
22. Mheshimiwa Spika, Serikali pia ilifanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kwa kufuta kodi ya Zuio kwa usafirishaji wa samaki nje ya nchi ili kuongeza utoaji wa huduma za usafirishaji wa mazao ya samaki kutokea hapa nchini badala ya kupitia nchi za jirani. Aidha, marekebisho yalifanyika katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kwa kupunguza ushuru wa bidhaa kwenye mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ili kupunguza gharama za uzalishaji.
23. Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ushuru wa Mafuta ya Petroli, SURA 220 ilifanyiwa marekebisho kwa kutoa msamaha wa ushuru unaotozwa kwenye mafuta yanayotumika katika kuendesha meli, na vifaa vingine vinavyotumika katika utafiti wa mafuta na gesi ili kupunguza gharama. Aidha, marekebisho yalifanyika kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004 kufuatia kuridhia kwa Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama kufanya marekebisho mbalimbali katika kukuza Sekta za Viwanda, Usafirishaji, Mifugo, Biashara na Utalii. Vilevile, marekebisho yalilenga katika kuboresha afya ya jamii na kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
24. Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuhamasisha na kuhakikisha mashine za kielectroniki – EFD zinatumika ipasavyo; kuimarisha mfumo wa kusimamia vitalu vya kodi; kuongeza vituo vya kutoa huduma kwa wateja na vya kukusanyia mapato; kuimarisha mifumo ya malipo ya kodi; na kuboresha mfumo wa uthaminishaji kwa kuimarisha ukaguzi wa hesabu za walipa kodi.
Mwenendo wa Ukusanyaji Mapato
25. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Serikali ilipanga kukusanya mapato ya jumla ya shilingi bilioni 13,525.9 kutoka katika vyanzo mbalimbali na kutumia kiasi hicho kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Vyanzo vya mapato vilikuwa kama ifuatavyo: mapato ya ndani yalikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 6,775.9; mapato kutoka Serikali za mitaa yalikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 350.5; misaada na mikopo ya kibajeti ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 869.4; misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na ya kisekta ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 3,054.1; mikopo ya ndani na nje yenye masharti ya kibiashara ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 1,664.9; na mikopo ya kulipia dhamana na hatifungani zinazoiva zilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 810.9.
26. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri, hadi Aprili 2012 makusanyo yamefikia jumla shilingi bilioni 5,684.5. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 80 ya makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 7,126.4 kwa mwaka 2011/12.
27. Mheshimiwa Spika, makusanyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni 5,227.5 ambayo ni sawa na asilimia 84 ya makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 6,228.8. Kulingana na mwenendo wa makusanyo ya mapato ya kodi kwa kipindi cha miezi kumi ya mwaka 2011/12, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2011/12 Serikali inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 6,307.8 na hivyo kuweza kufikia lengo tulilojiwekea.
28. Mheshimiwa Spika, mapato yasiyotokana na kodi yamefikia shilingi bilioni 451.6 ikiwa ni asilimia 83 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 547.1 kwa mwaka. Kutokana na mwenendo huo, Serikali inatarajia hadi Juni 2012 kufikia lengo.
29. Mheshimiwa Spika, mapato ya Serikali za Mitaa yalifikia kiasi cha shilingi bilioni 143, sawa na asilimia 40.8 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 350.5 kwa mwaka. Hadi Juni 2012, Serikali inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 200 kutokana na chanzo hiki ikiwa ni asilimia 57 ya lengo la mwaka. Kutokufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato haya kumechangiwa na kuchelewa kuanza kutekeleza utozaji wa ada za leseni.
Misaada na Mikopo ya Masharti Nafuu Kutoka Nje
30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali ilikadiria kupata kiasi cha shilingi bilioni 869.4 kama misaada na mikopo ya kibajeti ambapo hadi sasa Serikali imepokea shilingi bilioni 916.3, ikiwa zaidi kwa shilingi bilioni 46.9. Ongezeko hili limetokana na baadhi ya wafadhili kutoa fedha zaidi ya kiwango walichoahidi. Kwa upande wa misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha mifuko ya kisekta, hadi kufikia Aprili 2012 ilifikia shilingi bilioni 1,450.4 sawa na asilimia 47 ya makadirio ya bajeti ya mwaka ya shilingi bilioni 3,054.1. Upungufu huu umesababishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa baadhi ya miradi na kuchelewa kupokea taarifa ya fedha hizi kutoka kwa washirika wa maendeleo na Wizara na Taasisi zinazotekeleza miradi husika.
Mikopo ya Ndani
31. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012, Serikali imekopa kiasi cha shilingi bilioni 526 kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva ikiwa ni asilimia 64 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 819.1. Aidha, Serikali ilipanga kukopa shilingi bilioni 393.4 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa kwa ajili ya kugharamia matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia Aprili 2012, Serikali ilikuwa imekopa shilingi bilioni 232.6 sawa na asilimia 59 ya makadirio ya mwaka.
Mikopo ya Nje yenye Masharti ya Kibiashara
32. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12 Serikali ilikadiria kukopa kiasi cha Dola za Marekani milioni 822, sawa na shilingi bilioni 1,271.6 kama mikopo ya kibiashara. Katika kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012, Serikali ilisaini Mkataba wa mkopo wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 310 na Benki ya Standard ya Afrika Kusini. Hadi kufikia Aprili 2012, jumla ya Dola za Marekani milioni 229 ambazo zilitumika kulipia madeni ya barabara ya mwaka 2010/11. Aidha, Serikali ilisaini Mkataba wa mkopo wa Euro milioni 61 na Benki ya HSBC. Mkopo huu umeelekezwa kugharamia ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa megawati 60 Nyakato Mwanza. Serikali pia imesaini mkataba wa mkopo wa Dola za Marekani milioni 350 kutoka Benki ya Credit Suisse ya Uingereza ambapo Dola za Marekani milioni 200 zimepokelewa mwanzoni mwa Mwezi Juni 2012. Kiasi kilichobaki cha Dola za Marekani milioni 150 kitapatikana na kutumika mwaka 2012/13.
33. Mheshimiwa Spika, Serikali imepata Mshauri Mwelekezi ambaye ataishauri Serikali katika zoezi la kujiandaa kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni (Sovereign Credit Rating). Maandalizi haya yataiwezesha nchi kufanyiwa tathmini yanatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2013. Kukamilika kwa zoezi hilo kutawapatia wakopeshaji imani na hivyo kuiwezesha Serikali kupata mikopo yenye masharti nafuu ya kibiashara kwa wakati.
Sera za Matumizi
34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali iliendelea kutekeleza sera za matumizi kulingana na upatikanaji wa mapato ya ndani, misaada pamoja na mikopo ya ndani na nje. Aidha, Serikali iliendelea kuboresha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, ikijumuisha udhibiti wa ulipaji wa mishahara, matumizi katika miradi ya maendeleo, ruzuku ya pembejeo, ununuzi wa umma na kuendelea kudhibiti malimbikizo ya madeni. Serikali imeandaa mkakati wa kulipa na kudhibiti madeni yatokanayo na malimbikizo ya madai ya watumishi; wakandarasi; wazabuni; na madeni mengineyo. Madeni hayo yatalipwa baada ya kuhakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani.
Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma
35. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, Serikali iliendelea kutekeleza programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha za umma katika Serikali Kuu na Serikali za mitaa. Katika utekelezaji wa programu hiyo Serikali imeweka mtandao wa IFMS katika Halmashauri 133. Aidha, Serikali imetoa mafunzo ya ulipaji kwa mfumo wa malipo ya kibenki -TISS kwa watumishi wa kada ya Uhasibu katika mikoa 20, Hazina ndogo zote, Ofisi ya Bunge, TAMISEMI na Ofisi ya Mrajisi wa vyama vya Ushirika. Vilevile, Serikali imetoa mafunzo kwa Wahasibu wa Wizara, Idara, Mikoa na Balozi zetu 32 katika kuandaa Hesabu za Serikali kwa viwango vya Kimataifa (IPSAS – Accruals basis).
36. Mheshimiwa Spika, kutokana na maboresho hayo, usimamizi wa fedha katika Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa unaendelea kuimarika. Hali hii inajidhiirisha katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2010/11 ambapo Hati safi za ukaguzi kwa Wizara, Idara na Sekretarieti za Mikoa zimeongezeka kutoka asilimia 71 hadi asilimia 85. Wakati Hati zenye shaka zimepungua kutoka asilimia 26 mwaka wa fedha 2009/10 hadi asilimia 15 kwa mwaka wa fedha 2010/11 na hapakuwepo na Hati zisizoridhisha ikilinganishwa na mwaka 2009/10 ambapo Hati hizo zilitolewa kwa Taasisi mbili.
37. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Balozi zetu Hati safi zimeongezeka kutoka asilimia 71 mwaka 2009/10 na kufikia asilimia 85 mwaka 2010/11 na hapakuwepo na Hati zisizoridhisha katika mwaka 2010/11. Aidha, kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa Hati safi zimeongezeka kutoka asilimia 49 mwaka wa fedha 2009/10 hadi asilimia 54 mwaka 2010/11 na Hati zenye shaka zimepungua kutoka asilimia 64 mwaka 2009/10 na kufikia asilimia 56 mwaka 2010/11.
38. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali imefungua akaunti sita kwa kila Halmashauri kwa ajili ya uendeshaji wa majukumu yao. Akaunti hizo ni za Mapato; Amana; Matumizi ya kawaida; Mishahara; Maendeleo; na Mfuko wa Barabara. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uendeshaji, urasimu wa matumizi, ugumu wa kutoa taarifa za matumizi, ulimbikizaji wa fedha kwenye akaunti bila kutumika kwa muda mrefu na kudhibiti fedha zisitumike katika shughuli ambazo hazikuidhinishwa.
Mwenendo wa Matumizi
39. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, Serikali ilikadiria kutumia kiasi cha shilingi bilioni 13,525.9 katika mwaka wa fedha wa 2011/12. Mgawanyo wa matumizi ya Serikali katika kipindi hiki ulikuwa kama ifuatavyo; kiasi cha shilingi bilioni 8,600.3 zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 4,925.6 zilikadiriwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Matumizi ya kawaida
40. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012 matumizi ya kawaida yamefikia shilingi bilioni 7,349.8 sawa na asilimia 85.5 ya makadirio ya mwaka kama ilivyo katika ridhaa ya matumizi. Kati ya kiasi hicho, malipo ya mishahara ya watumishi wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma yalikuwa shilingi bilioni 2,760.5 sawa na asilimia 84.4 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 3,270.3. Malipo ya riba kwa mikopo ya ndani na nje yalikuwa shilingi bilioni 316.1 sawa na asilimia 102.4 ya makadirio ya shilingi bilioni 308.7 kwa mwaka. Malipo ya mikopo ya nje yalikuwa shilingi bilioni 57.3 sawa na asilimia 85.7 ya makadirio kwa mwaka. Serikali ilitumia shilingi bilioni 526 kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali za muda mfupi na Hatifungani za Serikali zilizoiva. Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika kulipa madeni kwa wakati ili kuepuka malimbikizo ya riba.
41. Mheshimiwa Spika, matumizi mengineyo katika Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Mikoa na Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 2,384.9 ikiwa ni asilimia 72.8 ya makadirio ya shilingi bilioni 3,275.1 kwa mwaka. Kati ya matumizi mengineyo, kiasi cha shilingi bilioni 284.1 zilitumika kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ikiwa ni asilimia 89 ya bajeti ya mwaka ya shilingi bilioni 317.4, na hivyo kunufaisha jumla ya wanafunzi 93,176. Kadhalika, Serikali ililipa kiasi cha shilingi bilioni 44.0 za madai ya walimu wa shule za msingi na sekondari yaliyohakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani.
Matumizi ya Maendeleo
42. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Matumizi ya Maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 2,657.2 ziligharamia miradi ya maendeleo ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya kutumia shilingi bilioni 4,924.6. Fedha za ndani zilikuwa shilingi bilioni 1,201.6 ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 1,871.5 sawa na asilimia 64.2. Upungufu huu umetokana na kuchelewa kupatikana kwa wakati kwa mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara. Jumla ya shilingi bilioni 663.8 ziligharamia miradi ya miundombinu, kati ya hizo shilingi bilioni 296 zilitumika kwenye miradi ya umeme na shilingi bilioni 367.8 kwenye miradi ya barabara. Matumizi ya maendeleo yaliyogharamiwa kwa fedha za nje yalikuwa shilingi bilioni 1,450.4 ikilinganishwa na makadirio ya shilingi bilioni 3,054.1 sawa na asilimia 47.
Vitambulisho vya Taifa na Anwani za Makazi
43. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na azma yake ya kutekeleza mradi wa Vitambulisho vya Taifa ambavyo vitasaidia, pamoja na mambo mengine, kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma za kifedha. Mradi huu unaenda sambamba na uanzishwaji wa anwani za makazi. Vitambulisho hivyo vitaanza kutolewa katika robo ya kwanza ya mwaka 2012/13 kwa Zanzibar na Mkoa wa Dar es Salaam.
Sensa ya Watu na Makazi na Utafiti Kuhusu Hali ya Umaskini
44. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi Serikali imeendelea kugharamia maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 95. Hadi sasa Serikali imetumia shilingi bilioni 23.6 kugharamia maandalizi ya zoezi la Sensa. Sensa hiyo imepangwa kufanyika tarehe 26 Agosti 2012. Aidha, Serikali iliendelea kugharamia utafiti wa mapato na matumizi katika kaya. Utafiti huu ulianza mwezi Oktoba 2011, na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2012 na matokeo yanatarajiwa kutoka mwezi Julai 2013. Utafiti huu utatoa picha halisi ya hali ya umaskini, hususan wa kipato tangu mwaka 2007 hadi mwaka 2012. Hii itasaidia kutambua mwenendo wa umaskini wa kipato na sababu zilizopelekea mwenendo huo.
Utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II)
45. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/12, serikali iliendelea kutekeleza MKUKUTA awamu ya pili unaojielekeza katika maeneo ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato, kuboresha maisha na ustawi wa jamii, na utawala bora na uwajibikaji sambamba na Melengo ya Maendeleo ya Milenia. Ili kufikia matokeo tarajiwa katika kila eneo, sekta kadhaa huchangia katika utekelezaji kupitia sera, mikakati na mipango ya kisekta. Kwa mantiki hiyo, utekelezaji wa MKUKUTA II unahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali za uchumi katika hatua ya upangaji na utekelezaji.
46. Mheshimiwa Spika, MKUKUTA ni mkakati unaoziweka pamoja juhudi za Serikali na wadau mbalimbali katika kupambana na umaskini. Aidha, umaskini ni suala pana linalojumuisha umaskini wa kipato na usio wa kipato. Ni kweli kuwa umaskini wa kipato umekuwa ukipungua kwa kasi ndogo. Hata hivyo, Serikali inachukua hatua mbalimbali za kupunguza umaskini kwa kujenga mazingira bora ili wananchi washiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika elimu, afya, miundombinu na sekta ya fedha.
47. Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto zilizojitokeza, hususan mtikisiko wa uchumi duniani, uchumi uliendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha. Kiwango cha ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2011, kilikuwa asilimia 6.4 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2010. Aidha, pato la wastani la Mtanzania limeongezeka kutoka shilingi 770,464 kwa mwaka 2010 hadi shilingi 869,436 kwa mwaka 2011. Kwa wastani, ongezeko hili limeongeza uwezo wa wananchi kupata huduma bora ikiwa ni pamoja na nyumba bora, simu za mkononi, pikipiki na usafiri wa baiskeli.
48. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutekeleza programu mbalimbali za huduma ya jamii kwa lengo la kuboresha maisha na ustawi wa jamii. Matokeo ya utekelezaji wa programu hizo zinaonesha mabadiliko chanya. Katika sekta ya elimu, viwango vya uandikishaji na kumaliza katika ngazi zote za elimu vinaridhisha. Mfano, kiwango cha uandikishwaji katika elimu ya msingi, kilikuwa asilimia 94 na katika elimu ya sekondari ni asilimia 35 kwa mwaka 2011. Huduma za afya kwa mtoto na mama zinaendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa mpango wa afya ya mtoto na mama. Aidha, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama imeendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa programu ya sekta ya maji iliyoanza mwaka 2007.
49. Mheshimiwa Spika, katika kudumisha utawala bora na uwajibikaji, Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na: kuimarisha sekta ya sheria kwa kuongeza idadi ya mahakimu wa Mahakama za mwanzo; kuimarisha mfumo wa sheria na haki za binadamu; kuhamasisha umma kuhusu haki za binadamu na wajibu wa jamii; na kushiriki katika mpango wa nchi za Afrika kujitathmini zenyewe katika masuala ya utawala bora. Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma, kwa kuimarisha ofisi za ukaguzi katika wizara, mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Sekta ya Fedha
50. Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya mageuzi mbalimbali katika sekta ya fedha ili kuhakikisha kwamba inachangia kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kukuza Pato la Taifa. Mageuzi haya yameleta mafanikio makubwa.Hadi kufika mwezi Aprili mwaka 2012 idadi ya benki imeongezeka na kufikia 49 kutoka benki 43 Aprili mwaka 2011. Kadi za simu za mkononi zinazotumika kutoa huduma za kifedha zimefikia 21,184,808 mwaka 2011 kutoka 10,663,623 mwaka 2010. Aidha, idadi ya Taasisi ndogo ndogo za kifedha zimefikia 150 mwaka 2011.
51. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutoa Mikopo ya kilimo kupitia dirisha la Kilimo lililopo katika Benki ya Rasilimali Tanzania. Hadi kufikia Machi, 2012 jumla ya mikopo 81 yenye thamani ya shilingi bilioni 22.9 ilitolewa, kati ya mikopo hiyo, 42 ni ya SACCOS, 32 ni kwa ajili ya makampuni na 7 kwa Taasisi ndogondogo za fedha (MFIs). Mikopo iliyotolewa kwa MFIs na SACCOS ilitumika kukopesha miradi mingi ya wakulima wadogo wadogo vijijini. Aidha, Serikali imetoa shilingi bilioni 30 kwa ajili ya mtaji wa Benki ya Kilimo.
52. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na utekelezaji wa programu ya mageuzi na maboresho ya Ushirika nchini ili kuimarisha vyama vikuu vya ushirika na kuviwezesha kutoa huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi hususan waliopo vijijini. Mwaka 2011, idadi ya Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) iliongezeka na kufikia 5,346 kutoka vyama 5,314 mwaka 2010. Vile vile, idadi ya wanachama iliongezeka kwa asilimia 5.7 na kufikia wanachama 970,655 kutoka wanachama 917,889 mwaka 2010. Aidha, Hisa, Akiba na Amana za wanachama ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 236.8 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 399.0 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 68.5. Mikopo iliyotolewa kwa wanachama iliongezeka kutoka shilingi bilioni 539.2 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 627.2 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 16.3.
53. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi 2012, mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 21.9 ikilinganishwa na asilimia 23.3 Machi 2011. Ongezeko hili linaenda sambamba na kuongezeka kwa rasilimali za fedha za ndani kwenye benki pamoja na kupungua kwa ukuaji wa rasilimali za fedha za kigeni kwenye benki. Sehemu kubwa ya mikopo hii ilielekezwa katika shughuli binafsi asilimia 21.9; biashara asilimia 19.9; uzalishaji bidhaa viwandani asilimia 11.9; kilimo asilimia 11.8; na usafiri na mawasiliano asilimia 7.9.
54. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza upatikanaji wa mikopo, Serikali imepata Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kuanzisha taasisi ya kuratibu taarifa za wakopaji (Credit Rerefence Bureau) na mfumo wa kuhifadhi taarifa za wakopaji (Credit Reference Databank). Mshauri mwelekezi ameanza zoezi la kuweka mitambo na kutoa mafunzo kwa watumiaji. Aidha, Serikali imeboresha mazingira ya upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na kati kwa ajili ya nyumba, Kilimo na uwekezaji ambapo kanuni za taasisi za fedha za maendeleo ziliandaliwa na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali la Machi 2012.
55. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali imeendelea kufanya maboresho katika sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa kufanya tathmini ya uwekezaji wa mifuko, uhai wa mifuko, pamoja na kuandaa mwongozo za uwekezaji wa mifuko hiyo. Aidha, Serikali imefanya marekebisho ya Sheria za Mifuko yote pamoja na Mamlaka ya Usimamiaji wa Shughuli za Mifuko (SSRA) ili kuboresha usimamizi wa mifuko hiyo.
Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
56. Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu lilipitisha sheria mpya ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ya mwaka 2010 ili kutoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika ujenzi wa miundombinu na kuiendesha kwa lengo la kutoa huduma bora za kijamii na kiuchumi kwa wananchi. Katika mwaka 2011/12, Serikali imefanya maandalizi ya utekelezaji wa Sera ya Ubia ikiwa ni pamoja na kuanzisha madawati ya PPP kwa kila Wizara na kuandaa miongozo itakayotumika kuchambua na kuidhinisha miradi ya Ubia kwa mujibu wa sheria. Aidha, Serikali imeanza hatua za awali kubaini miradi inayoweza kutekelezwa kwa utaratibu wa Ubia kwa mujibu wa sheria.
57. Mheshimiwa Spika, dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi inatekelezwa kwa kutumia sheria mbili – Sheria ya Ubia ya mwaka 2010 na Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 iliyorekebishwa mwaka 2011. Sababu za kurekebisha Sheria ya Ununuzi wa Umma pamoja na mambo mengine ni kuingiza vifungu vinavyowezesha Taasisi za Serikali kupata Wabia makini wa uwekezaji katika miradi ya Umma kwa njia zilizo wazi. Aidha, katika mwaka 2012/13, Serikali itakamilisha Kanuni za Sheria ya Ununuzi wa Umma ambazo zinazingatia mazingira ya kipekee ya Sheria ya Ubia ambayo inawezesha kupata Wabia walio tayari kuwekeza katika miradi husika. Serikali itahakikisha kanuni na taratibu zote za kuidhinisha na kusimamia miradi ya ubia zinazingatiwa.
58. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali itatoa mafunzo ya uelewa wa dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi kwa watumishi wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi za Serikali, na Halmashauri zote. Aidha, Serikali itachagua miradi michache ya kuanza nayo ili kupata uzoefu wa uendeshaji wa miradi hiyo. Maeneo tunayotarajia kuanza nayo ni barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, maji pamoja na ujenzi wa ofisi.
59. Mheshimiwa Spika, Napenda kutumia fursa hii kuziomba Wizara, Idara zinazojitegemea, Mashirika ya Umma, na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhamasisha Sekta Binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa kuzingatia taratibu na kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria.
Usimamizi wa Deni la Taifa
60. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma yake ya kuboresha miundombinu ya kimkakati, Serikali imeendelea kukopa kutoka nje na ndani ya nchi ili kugharamia miradi mbali mbali ya maendeleo. Hadi mwishoni mwa Machi 2012, deni la taifa lilikuwa shilingi bilioni 20,276.6 ikilinganishwa na deni la shilingi bilioni 17,578.9 Machi 2011 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 15.4. Kati ya hizo, shilingi bilioni 15.306.9 zilikuwa ni deni la nje na shilingi bilioni 4,969.7 ni deni la ndani. Kati ya kiasi cha deni la nje, shilingi bilioni 12,342.5 zilikuwa ni deni la umma na kiasi kilichobaki cha shilingi bilioni 2,964.4 ni deni la sekta binafsi. Aidha, hadi kufikia Machi 2012, deni la ndani la Serikali lilifikia shilingi bilioni 4,969.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 4,496.5 mwezi Machi, 2011, sawa na ongezeko la asilimia 10.5. Sababu kubwa ya kuongezeka kwa deni la taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo na utumiaji wa dhamana za muda mfupi za Serikali kwa ajili ya kudhibiti mfumuko wa bei katika uchumi na kushuka kwa thamani ya shilingi kuliongeza deni la nje.
61. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Deni la Taifa linasimamiwa vizuri, mwezi Februari, 2012, Serikali ilifanya tathmini ya uhimilivu wa deni (Debt Sustainability Analysis) likijumuisha dhamana zinazotolewa na Serikali kwa Wizara, Mashirika na Taasisi za Umma ambapo matokeo ya tathmini hiyo yanaonesha kuwa Deni la Taifa linahimilika.
Usimamizi wa Mashirika ya Umma
62. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Taasisi, Wakala na Mashirika ya umma yanatekeleza majukumu yao, Serikali imetoa Waraka Na.1 wa mwaka 2012 unaoelekeza Wizara mama na Bodi za Wakurugenzi kuingia katika mikataba ya utendaji, Waraka huo umeanza kutumika Januari, 2012. Aidha, ukaguzi wa kiutendaji (Management Audit) katika Taasisi za Serikali umefanyika kwa baadhi ya Taasisi na Mashirika ya umma kwa kuangalia uzingatiaji wa kanuni, Sheria na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali ikiwa ni pamoja na uwajibikaji na utawala bora, matumizi ya fedha na taratibu za ajira. Zoezi hili ni endelevu na linalenga kuboresha uendeshaji wa Mashirika na Taasisi za Serikali. Kadhalika, Serikali imefanya uhakiki wa mashirika 170 yaliyobinafsishwa. Kati ya hayo, mashirika 41 yalikutwa yanajiendesha kwa faida, mashirika 66 yanajiendesha kwa hasara na mashirika 63 yalikuwa muflisi. Kwa yale ambayo yanaendeshwa kwa hasara yatawekwa chini ya mfilisi kwa lengo la kuyachambua na kupendekeza hatua za kuchuliwa. Aidha, kwa yale yaliyokuwa muflisi hatua za kuyafilisi zinaendelea.
III. BAJETI YA MWAKA 2012/13
63. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2012/13 itazingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13; Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na program za maboresho katika sekta ya umma. Lengo likiwa ni kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
64. Mheshimiwa Spika, pamoja na miongozo hiyo, Bajeti hii inazingatia pia changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/12. Changamoto hizo ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika; kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la Dunia; uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo; kupanda kwa bei za bidhaa na huduma; kutopatikana kwa wakati fedha za kugharamia miradi ya maendeleo kulikosababishwa na masharti magumu na urasimu kwa mikopo ya kibiashara; na kuongezeka kwa malimbikizo ya madeni ya ndani, hususan ya wazabuni, wakandarasi na watumishi. Mambo mengine yaliyozingatiwa ni pamoja na mwenendo wa uchumi wa dunia na makubaliano ya kikanda na kimataifa. Serikali imepanga hatua mbalimbali za kuchukua kukabiliana na changamoto hizo kama nitakavyoeleza hapo baadae.
Shabaha na Malengo ya Bajeti ya mwaka 2012/13
65. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2012/13, imejielekeza katika kufikia Shabaha na malengo yafuatayo:
i. Kukuza Pato halisi la Taifa kwa asilimia 6.8 mwaka 2012 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.4 mwaka 2011;
ii. Kuimarisha miundombinu ya uchumi, ikijumuisha umeme, barabara, reli na bandari;
iii. Kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha;
iv. Kuongezeka kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano na Pato la Taifa wa asilimia 18 kwa mwaka 2012/13 kulinganisha na mwelekeo wa asilimia 16.9 mwaka 2011/12;
v. Kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei ili urudi kwenye viwango vya tarakimu moja;
vi. Kuwa na kiwango tengemavu cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha;
vii. Kukua kwa mikopo kwa sekta binafsi kwa kiwango cha asilimia 20 ya Pato la Taifa mwishoni mwa Juni 2013 sambamba na jitihada za kudhibiti mfumuko wa bei;
viii. Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne na nusu;
ix. Kuimarisha utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ili kupanua fursa za kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo;
x. Kuboresha mazingira ya wafanya biashara wadogo na wakati;
xi. Kulinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika Sekta za huduma za jamii;
xii. Kuimarisha utawala bora na uwajibikaji; na
xiii. Kujenga uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi na kifedha pamoja na kushiriki kwa ufanisi katika ushirikiano kikanda na kimataifa.
Misingi ya Bajeti ya Serikali kwa Kipindi cha mwaka 2012/13
66. Mheshimiwa Spika; ili kufikia malengo yaliyoainishwa hapo juu, misingi ya Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2012/13 ni hii ifuatayo:
i. Kuendelea kuimarika kwa utengamavu wa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii;
ii. Kuwepo kwa nishati ya umeme wa uhakika na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia;
iii. Kuimarika kwa utekelezaji wa Sera za Fedha na Bajeti;
iv. Kuendelea kuimarika kwa mahusiano na Washirika wa Maendeleo;
v. Kuendelea kutekeleza sera ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi;
vi. Kuendelea kutekeleza maboresho katika sekta ya umma ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma;na
vii. Kuendelea kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kuongezeka kwa tija na fursa za uwekezaji.
Sera za Mapato
67. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na azma yake ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali katika maeneo ya mapato yatokanayo na kodi na yasiyotokana na kodi; na kupanua wigo wa makusanyo. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha taratibu za kukusanya mapato pamoja na kupunguza misamaha ya kodi ili kuweza kugharamia kwa kiwango kikubwa matumizi ya kawaida kwa kutumia mapato ya ndani. Sera za mapatozitakazozingatiwa kwenye Bajeti ya mwaka 2012/13 ni pamoja na;
i. kuboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamiaji wa mapato yasiyo yakodi kwa kupitia upya mfumo wa utoaji stakabadhi na leseni, pamoja na kuboresha viwango vya kubakiza maduhuli kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali;
ii. kupanua wigo wa kodi kwa kuendelea kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo wa kodi;
iii. kuendelea kufanya mapitio ya sheria za Wakala/Taasisi za Umma zinazokusanya maduhuli ili ziweze kuchangia zaidi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali;
iv. kuendelea kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo;
v. Kupitia upya mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo katika majiji, manispaa, miji, wilaya na miji midogo ili kuuboresha zaidi;
vi. kufanya mapitio ya vyanzo vya mapato na mfumo wa ukusanyaji katika Serikali za Mitaa ili kuongeza mapato; na
vii. Kujenga uwezo wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Wakala wa Ukaguzi wa Madini ili kusimamia ukusanyaji wa mapato katika maeneo ya madini, gesi na petroli.
Hatua za Kuboresha Uzalishaji na Huduma
68. Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo waheshimiwa wabunge kuhusu haja ya kuboresha mazingira ya uzalishaji katika sekta za Uvuvi, Viwanda, Kilimo, Mifugo na Utalii. Hatua ambazo Serikali imepanga kuchukuwa ni pamoja na:
i. Kupitia upya vivutio kwa sekta ya viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi za ndani vikiwemo viwanda vya nguo na mafuta ya kula;
ii. Kutafuta utaratibu mzuri wa kubainisha vipuri vya mashine na mitambo inayosamehewa kodi ili kuondoa usumbufu wanaoupata waagizaji;
iii. Kupitia upya viwango vya kodi katika sekta ya Kilimo na Uvuvi kwa lengo la kuviwianisha na kupunguzwa;
iv. Kupitia upya maudhui na viwango vya Tozo ya Kuendeleza Stadi (Skills Development Levy) na Leseni ya Magari (Motor Vehicle Licence). Kwa kufanya hivyo, Serikali inalenga katika kupanua wigo wa kodi, kuwapunguzia mzigo waajiri na kupanua ajira hapa nchini. Aidha, mapitio ya Leseni za Magari yatazingatia kurejea madhumuni ya kuanzishwa kwa leseni hiyo; na
v. Kufanya mapitio ya Sheria ya VAT kwa lengo la kuibadili kwa kuzingatia uzoefu wa kimataifa “Best Practice”.
69. Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinahimizwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuzingatia fursa zilizopo. Aidha, OWM – TAMISEMI kwa kushirikiana na Shirika la Misaada na Utaalamu la Ujerumani – GIZ watakamilisha na kusambaza kwenye Halmashauri mfumo wa kompyuta wa utunzaji kumbukumbu za mali na majengo (Integrated Property Rating Information Management System - IPRIMS) ili kuboresha ukusanyaji wa mapato hususan kodi ya majengo. Natoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali kuweka msukumo utakaowezesha Halmashauri kukusanya kikamilifu kodi ya majengo pamoja na mapato mengine ili kuziongezea uwezo wa kuhudumia wananchi na kuwaletea maendeleo endelevu.
70. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za mapato zilizoainishwa hapo juu, Serikali inalenga kukusanya mapato ya ndani (bila kujumuisha Halmashauri) shilingi bilioni 8,714.7 sawa na asilimia 18 ya Pato la Taifa. Kati ya kiwango hicho, mapato ya kodi shilingi bilioni 7,080.1 na mapato yasiyo ya kodi shilingi bilioni 644.6. Mapato yanayotokana na vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 362.2 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.
Mikopo ya Ndani
71. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na utaratibu wake wa kukopa katika soko la ndani la fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na kulipia hatifungani za Serikali na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva. Katika mwaka 2012/13, Serikali inakusudia kukopa kiasi cha shilingi bilioni 1,632 kutoka soko la fedha la ndani. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 483.9 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo na kiasi cha shilingi bilioni 1,148.1 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani za Serikali na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva. Kiwango hiki kimezingatia viashiria vya kiuchumi pamoja na kuhakikisha kuwa Taasisi za Fedha zinaendelea kutoa mikopo kwa Sekta binafsi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Misaada na Mikopo Mipya yenye Masharti Nafuu
72. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na Washirika wa Maendeleo ili kuhakikisha Misaada na mikopo inapatikana kwa wakati na kuchangia katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali. Katika bajeti ya mwaka 2012/13 serikali inatarajia kupata kiasi cha shilingi bilioni 3,156.7 kutokana na misaada na mikopo yenye masharti nafuu. Kati ya fedha hizo, Misaada na mikopo ya kibajeti ni shilingi bilioni 842, sawa na Dola za Marekani milioni 495. Misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikijumuisha mifuko ya kisekta inatarajiwa kuwa shilingi bilioni 2,314.2.
73. Mheshimiwa Spika, pamoja na misukosuko ya kiuchumi na majanga ya kiasili iliyozikumba nchi Wahisani, bado zimeendelea kutoa misaada na mikopo kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Napenda kuwatambua washirika wetu wa maendeleo ambao ni: Uingereza, Norway, Canada, Marekani, Uholanzi, Ubelgiji, China, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Japani, Korea ya Kusini, Denmark, Hispania, Sweden, Uswisi, India, Italia, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Umoja wa Ulaya, Global Funds, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), BADEA, Kuwait Fund, Nordic Fund, Opec Fund, Saudi Fund, na Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Tunawashukuru Sana.
Mikopo ya nje yenye Masharti ya Kibiashara
74. Mheshimiwa Spika, sera ya Serikali ni kutafuta mikopo nafuu kutoka mashirika na nchi wahisani kwa ajili ya kugharamia Bajeti yake ya maendeleo. Hata hivyo, kwa kuzingaita mahitaji makubwa ya kuendeleza miradi ya miundombinu kwa mwaka 2012/13, Serikali inatarajia kupata kutoka nje mikopo yenye masharti ya kibiashara kiasi cha shilingi bilioni 1,254.1 sawa na Dola za Marekani milioni 749. Fedha hizi zitatumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13 ikijumuisha mchango wa Serikali (counterpart fund) katika ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, mradi wa maji wa Ruvu chini na ujenzi wa barabara. Uamuzi wa kuendelea kukopa kwa masharti nafuu na ya kibiashara unazingatia uhimilivu wa Deni la Taifa uliopo.
Sera za Matumizi
75. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, sera za matumizi zitazingatia yafuatayo:
i. Matumizi yataendelea kuzingatia mapato halisi yanayopatikana;
ii. Nakisi ya bajeti haitazidi asilimia 5.5 ya Pato la Taifa, ikijumuisha ruzuku;
iii. Mafungu yataendea kuzingatia viwango vya matumizi vitakavyoidhinishwa na Bunge;
iv. Maafisa Masuuli wataendelea kuzingatia Sheria ya Fedha na ya Ununuzi wa Umma; na
v. Serikali inaendelea kukusanya madeni yote kwa lengo la kuyahakiki na kuyapangia utaratibu wa kuyalipa.
Matumizi ya Kawaida
76. Mheshimiwa Spika, Sera za matumizi ya kawaida kwa mwaka 2012/13 zinalenga pamoja na mambo mengine katika kugharamia mishahara; madeni ya mikopo ya ndani na nje; uboreshaji wa huduma za kiuchumi na maendeleo ya jamii; mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; mitihani ya shule za msingi na sekondari; ununuzi na usambazaji wa dawa; mahitaji ya Tume ya Kuratibu Mabadiliko ya Katiba; matengenezo ya mali ya Serikali; ununuzi wa chakula cha hifadhi; mahitaji ya kawaida kwenye miradi iliyokamilika; pamoja na kuendelea kulipa madai mbalimbali ya watumishi na wazabuni.
77. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu, kilimo kisichokuwa na tija na ukosefu wa ajira, Serikali imetenga fedha katika maeneo yafuatayo: Shilingi bilioni 30 kwa ajili ya Benki ya Rasilimali; shilingi bilioni 40 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo na hivyo kufikisha mtaji wa shilingi bilioni 100. Aidha, shilingi bilioni 7.5 zimetengwa kwa ajili ya kurejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, ambapo katika awamu ya kwanza vijana 5,000 wanatarajiwa kujiunga. Vilevile, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 70.7 katika maeneo mapya ikiwa ni Mikoa, Wilaya na Halmashauri kugharamia matumizi ya kawaida na maendeleo.
Matumizi ya Maendeleo
78. Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2011 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu Mhe. Stephen Masatu Wasira, aliainisha miradi ya kitaifa ya kimkakati pamoja na miradi katika maeneo muhimu ya ukuaji wa uchumi. Bajeti hii itazingatia vipaumbele hivyo:
a) Miundombinu
i. umeme - mkazo utawekwa katika upatikanaji wa umeme wa kuhakika kwa kuongeza uzalishaji, usafirishaji na usambazaji ambapo jumla shilingi bilioni 498.9 zimetengwa kwa ajili hiyo. Aidha, Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa mkopo kutoka Benki ya Exim ya China wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1,225.3 utakaosimamiwa na TPDC.
ii. usafirishaji na uchukuzi – uimarishaji wa reli ya kati ikijumuisha ukarabati wa injini na mabehewa ya treni. Kwa upande wa barabara, miradi inayopewa kipaumbele ni pamoja na barabara zenye kufungua fursa za kiuchumi. Katika usafiri wa anga na majini, miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na uendelezaji wa gati ya Ziwa Tanganyika. Jumla ya shilingi bilioni 1,382.9 zimetengwa katika eneo hili.
iii maji safi na salama - kuongeza upatikanaji wa
maji safi na salama mijini na vijijini. Kiasi cha shilingi bilioni 568.8 kimetengwa.
iv Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
– kuimarisha mawasiliano kwa kutumia TEHAMA ili kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa taarifa za masoko ya ndani na nje ya nchi; ukusanyaji wa mapato; huduma za afya; elimu; huduma za kifedha; n.k. Jumla ya shilingi bilioni 4 zimetengwa katika eneo hili.
b) Kilimo, Uvuvi na Ufugaji
79. Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na sekta binafsi, Serikali itawekeza katika kilimo cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya Wami, Ruvu, Kilombero na Malagarasi pamoja na kuongeza tija na thamani, kubadilisha mfumo wa kilimo na kukuza kilimo cha misitu. Hii ni pamoja na kuendeleza shughuli za ufugaji na uvuvi ili ziwe na tija kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji; kwa kufanya hivyo kutapunguza umaskini wa kipato.
80. Mheshimiwa Spika, katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula, Serikali itaimarisha utekelezaji wa dhana ya Kilimo Kwanza kwa kuhakikisha kwamba nguzo zake zote zinaendelea kuzingatiwa; kuhakikisha kwamba walengwa wanapata pembejeo kwa wakati; Maafisa ugani kutakiwa kuwa na mashamba yao ya mfano (mashamba darasa) ili kuwaelimisha wakulima kilimo cha kisasa; kuongeza msukumo kwenye kilimo cha umwagiliaji ili wakulima waweze kufanya shughuli zao za kilimo katika misimu yote badala ya kutegemea mvua;Kuimarisha masoko ya mazao kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko ambayo imeshaanza shughuli zake; na Mikoa kutakiwa kuendelea kutenga ardhi na vijiji kutakiwa kupima na kurasimisha ardhi kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na wa nje. Kiasi cha shilingi bilioni 192.2 kimetengwa katika eneo hili.
c) Maendeleo ya Viwanda
81. Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini; viwanda vinavyoongeza thamani ya madini; viwanda vikubwa vya saruji; na viwanda vya eletroniki na TEHAMA pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kutenga maeneo maalum ya uwekezaji mijini na vijijini na kukuza ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Hatua hii inaenda sambamba na kuboresha na kuimarisha viwanda vidogo vidogo nchini. Jumla ya shilingi bilioni 128.4 zimetengwa katika eneo hili.
d) Maendeleo ya Rasilimali Watu na Huduma za Jamii
82. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali imepanga kuboresha viwango vya elimu katika ngazi zote hususan katika maeneo ya utafiti, ufundi stadi, afya; sayansi na ujuzi maalum kuhusu madini, gesi, urani, chuma na mafuta; hatua hii inajumuisha ukarabati wa maabara na upatikanaji wa vifaa vya maabara. Shilingi bilioni 84.1 zimetengwa katika eneo hili.
e) Utalii
83. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha huduma zitolewazo katika eneo hili ikiwa ni pamoja na kutangaza utalii na kuboresha mazingira ya kitalii na kutoa mafunzo ya utalii, kuainisha maeneo mapya ya utalii na kuboresha vyuo vya utalii.
Huduma za Fedha
84. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za kifedha hususan mifumo ya kuweka akiba na kukopa kama vile SACCOS, VICOBA na benki za kijamii ili kuwawezesha wananchi kupata mitaji kwa ajili ya biashara na uzalishaji. Kiasi cha shilingi bilioni 2.6 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha mtaji wa Benki ya Wanawake, Mradi wa SELF na Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Aidha, Wizara ya Fedha itaendelea kusimamia maendeleo ya Taasisi za fedha zinazojihusisha na utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali. Ili kufanikisha hili kitengo kilichopo cha maendeleo ya sekta ya fedha kitahuishwa na kuwa idara kamili. BONYEZA HAPA KUSOMA ZAIDI
1 comment:
"Everybody wants to go to Heaven but nobody wants to die" how is that? Its funny uh? Kila mbongo anataka kuwa na maisha mazuri na kila mbongo anataka kuona bongo kuwa nchi nzuri ya kuishi, hii ikiwa na maana elimu bora, huduma bora za afya, mabarabara mazuri, umeme wa uhakika, teknologia yetu, kutokomeza mbu na nzi you name it, lakini hakuna hata mmoja anayetaka kujishughulisha in order all thise to happen. Tanzanian people where are we? We need collective effort and unity of action. Let's start now by singling out each necessity and work on it. Let's balance entertainments and politics VS production. When I say production I mean industrial products and agricultural produces.
Post a Comment