POAC YAKATAA HESABU ZA TBS, YAHOJI SHILINGI 28 BILIONI
Waandishi Wetu
KAMATI ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imembana Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ikimtaka aeleze ni kwa nini vitabu vya bajeti ya wizara hiyo vimechelewa kufikia wajumbe wa kamati hiyo.
Hatua ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa imekuja siku chache baada ya baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Miundombinu kuikataa Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, ikihoji sababu za bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2011/12 kutekelezwa kwa kiwango cha asilimia 40.
Juzi jioni, taarifa zilizopatikana kutoka kwenye kikao cha kamati hiyo ya mambo ya nje zilisema wajumbe walichukizwa na hatua ya wizara hiyo kuchelewa kuwapatia vitabu kwa mujibu wa taratibu.
Taarifa hizo zilisema, Lowassa alihoji sababu za msingi za wao kuchelewa kupata vitabu hivyo siku mbili kabla na badala yake kuvipata siku ya mkutano.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliliambia gazeti hili kwamba wajumbe waligomea bajeti hiyo kutokana na kuchukizwa na kitendo hicho cha kucheleweshwa kwa vitabu na kutokuonyesha madeni ya wizara.
Pia wajumbe hao walichukizwa na hatua ya ujumbe huo wa wizara hiyo kuchelewa kufika katika kikao hicho.
Hata hivyo, Lowassa alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo alikataa na kumtaka mwandishi athibitishe taarifa hizo kwa mtu aliyezitoa... “Siwezi kusema lolote kuhusu hilo na wala mimi sijui. Mwulize aliyekupa taarifa, yeye ana maelezo zaidi lakini siyo mimi.”
Chanzo hicho cha habari kilisema kamati hiyo pia ilihoji kuhusu uwasilishaji wa michango ya wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii, ikiwemo NSSF.
Hata hivyo, baadaye kamati ilipitisha bajeti hiyo ya Sh80 bilioni na kumtaka Waziri Membe na ujumbe wake kuwasilisha mapema vitabu vyao katika siku zijazo ili wajumbe waweze kuhoji utekelezaji wa mikakati ya Serikali.
Utetezi wa wizara
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Wizara hiyo, Assah Mwambene alipinga taarifa hizo za kwamba walichelewa kufika ukumbini na bajeti ya wizara kususiwa.
Mwambene alisema kilichotokea ni hoja ya vitabu kuchelewa lakini tayari waziri aliwaeleza kuwa hilo ni suala ambalo lilitokana na kamati husika.
Alisema majibu ya waziri yalikuwa wazi, yalieleweka kwani vitabu hivyo viliwasilishwa mwisho wa wiki, lakini kwa kuwa labda ilitokea kwamba haikuwa siku za kazi, ndiyo maana havikuwafikia mapema.
POAC yakataa hesabu za TBS
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imekataa kupitia hesabu za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) za mwaka 2010/11 hadi shirika hilo litakapotoa taarifa za fedha za ukaguzi wa magari zaidi ya Sh28 bilioni ambazo ziliripotiwa kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kupotea.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa TBS, Charles Ekelege kusimamishwa kazi kutokana na tuhuma za shirika hilo kuwa na ofisi hewa za ukaguzi wa magari nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe alisema jana kwamba fedha hizo ziko mikononi mwa mawakala wasio na leseni, ambao wamefanya kazi kwa miaka mitatu bila uongozi wa shirika kuwachukulia hatua.
Alisema mawakala hao wanapatikana Japan na Dubai na wale wa Hong Kong na Singapore wamefungiwa.
Zitto alisema hali hiyo imesababisha Serikali kukosa mapato yake, jambo ambalo limeonyesha wazi kuwa mikataba yao imetolewa bila ya kufuata sheria.
“Kuna mawakala wanne, watatu wanatoka Dubai na mmoja Japan, hawa hawana leseni ya kufanya kazi ya ukaguzi wa magari, jambo ambalo limesababisha hasara ya zaidi ya dola 18 milioni (Sh28 bilioni),” alisema Zitto.
Alisema taarifa iliyotolewa na CAG imeonyesha kuwa fedha hizo zilifuatwa na mkurugenzi huyo bila ya kushirikisha mtu mwingine, jambo ambalo limeonyesha wazi kuwa taratibu za kisheria hazikufuatwa.
Alisema vibali vya mawakala hao viliisha miaka mitatu iliyopita, lakini mkurugenzi huyo aliwapa kazi ya kukagua magari bila ya kutangaza zabuni ya aina yoyote, huku akijua kuwa anachokifanya ni kosa kisheria.
Zitto alisema mbali na fedha hizo, pia mawakala hao hawajawasilisha kiasi Sh404.8 milioni TBS.
Alisema kamati yake imeitaka TBS kuwasilisha mapendekezo ya mfumo mpya wa ukaguzi wa magari pamoja na utaratibu wa uteketezaji wa mali zisizo na ubora.
Zitto alisema kamati yake inaangalia makosa ya kijinai katika tuhuma hizo ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Alisema kamati yake itakutana na TBS tena Juni 30, mwaka huu Mjini Dodoma kuangalia njia mbalimbali za ukaguzi ambazo zinaweza kuiletea Serikali faida.
Mapema mwaka huu Kamati ya POAC ilitembelea vituo vya ukaguzi wa magari Singapore na Hong Kong, China na kubaini kuwa shirika hilo halina ofisi za ukaguzi wa magari.
Baada ya kurejea kamati hiyo ilimlipua Mkurugenzi wa TBS bungeni ikitaka awajibishwe kwa sababu si mkweli na kwamba fedha za ukaguzi zimekuwa zikiishia mifukoni mwa wajanja wachache.
Tunduru na bei ya yai
Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeagiza Tamisemi kumuonya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Ephraem Ole kwa taarifa mbaya za mahesabu.
Taarifa hiyo mbaya ni pamoja na hesabu hizo kuonyesha kuwa bei ya yai moja ni Sh900.
Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Iddi Azzan aliwataka viongozi wa halmashauri hiyo kutaja bei ya yai moja huko Tunduru wakasema kwa pamoja kuwa ni Sh500.
“Bei ya yai kwenye hesabu hizi mnaonyesha kuwa ni Sh900 lakini, nyie hapa mnasema ni Sh500, huu ni uzembe au ufisadi?” alihoji Azzan.
Alisema kama wameweka nyongeza yao kwenye bei ya mayai inawezekana kabisa hata kwenye matumizi mengine wakaweka nyongeza.
Azzan alisema mbali na kuzidisha bei hiyo, pia hakuna mchanganuo wa matumizi ya fedha za miradi mbalimbali inayoonyeshwa kwenye vitabu hivyo.
“Fedha zimetumika bila kuonyesha kwamba zimetumika vipi, huu ni uzembe kwa nyie viongozi mkiongozwa na mkurugenzi wenu,” alisema Azzan.
Mkurugenzi Ole aliishukuru kamati hiyo kwa maelekezo na kuahidi kuiboresha katika kipindi walichopewa.
Wakati huohuo; LAAC imeipa wiki mbili Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kurekebisha miradi miwili iliyomo katika ripoti yake ya mwaka 2010/11 baada ya kubaini kuwa Sh1 bilioni hazikuelezwa jinsi zilivyotumika.
Akizungumza katika kikao cha kamati hiyo, Azzan alisema miradi hiyo ni wa kilimo (DADP) ambao ulikuwa umetengewa Sh564 milioni na wa afya (Basket Fund) uliotengewa Sh570 milioni.
Alisema katika mchanganuo wa matumizi ya fedha katika miradi hiyo, licha ya kuonyesha jinsi fedha zilivyotumika, haikufafanua zilinunulia vifaa gani.
Alisema walibaini kuwa kuna Sh15 milioni ambazo halmashauri hiyo ilieleza kuwa zimenunulia kiwanja kwa ajili ya kujenga Shule ya Sekondari Zinga, lakini kamati yake ilitembelea eneo hilo na kubaini kuwa kiwanja hicho kilitolewa na wananchi na hakikununuliwa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake