Wednesday, June 6, 2012

UNAPENDWA, UNAACHWA TATIZO NI NINI?-2

KUJUA sababu ya tatizo angalau ni mwanzo wa kuelekea kwenye utatuzi, maana unakuwa umeshafahamu kwa nini jambo fulani linalotokea katika maisha yako. Marafiki zangu, kuachwa ni tatizo kubwa sana katika mapenzi.
Linaumiza sana. Linachoma na kuwanyima raha wahusika. Sikia nikuambie kitu kimoja, kuumia moyoni peke yake hakutoshi kukuondoa kwenye tatizo. Lazima ujiulize, kwa nini unaachwa? Hapo utakuwa katika nafasi nzuri ya kuhakikisha unaondoka katika utumwa huo.

Ndiyo shabaha hasa ya mada hii. Wiki iliyopita nilianza kwa dondoo tatu, leo tunaingia katika hatua ya mwisho. Karibuni darasani marafiki.
UNASHAURIKA?
Tabia ya kung’ang’ania mambo ambayo mpenzi wako hapendi ni kati ya sababu zinazotosha kabisa kukufanya uachike. Inawezekana mpenzi hapendi aina fulani ya mavazi, tabia fulani mbaya na amekuambia kwa nini hapendi lakini wewe ukaendelea kung’ang’ania. Hili ni tatizo.
Acha uking’ang’anizi, jaribu kuwa muelewa. Mwenzi wako anapokataa kitu na kukueleza sababu za msingi, msikilize na kama unaona anachokuambia hakifai basi mjibu kwa hoja na siyo kumuwekea kiburi.
DHARAU
Wanawake wenye dharau wapo katika nafasi kubwa zaidi ya kuachwa na wapenzi wao. Utakuta mwingine dharau zake zinazidi mipaka mpaka kwa ndugu wa mpenzi wake. Wakigombana kidogo, anaweza kutaja hata wazazi au ndugu wa karibu na mpenzi wake.
Ni mwanaume gani anayependa kuishi na mwanamke mwenye mdomo mchafu? Mwenye dharau? Anayeamini kila kitu anaweza mwenyewe? Sifa ya kwanza ya mwanamke ni heshima, kama mwanamke huna heshima basi fahamu kwamba huwezi kuishi na mwanaume hata siku moja.
Katika maisha ya ndoa kati ya mambo ya msingi ambayo huzingatiwa na wengi ni pamoja na kila mmoja kukubalika na ndugu wa pande zote, sasa itawezekana vipi wewe kuolewa ikiwa hata hao ndugu wenyewe unawadharau? Unawadhalilisha kwa maneno makali? Itawezekana vipi?
Mwanamke lazima uwe na heshima, uwe na haiba ya kike, siyo unaishi mradi siku zinakwenda. Kama huwa unaachwa kila wakati, chunguza tabia hii nayo inaweza kuwa chanzo cha wewe kuachwa!
UNAITAMBUA NAFASI YAKO?
Baadhi ya wanawake huwa hawataki kutambua na kutumikia nafasi zao, mwanamke hawezi kuwa sawa na mwanaume kwa kila kitu. Hata kama kwa bahati mbaya mmetofautina, kama mwanamke ambaye anatarajiwa mpenzi wako aje kuwa ‘kichwa cha nyumba’ yako, lazima uonyeshe unyenyekevu.
Tulia, msikilize kwa makini, hata kama ni yeye amekosea, usitumie kauli chafu ambazo zitamuudhi. Zungumza naye kwa staha ukitambua nafasi yake. Wakati mwingine wanawake wenyewe wanasababisha waachike. Usikubali kuwa hivyo!
KURUDIA MAKOSA
Hakuna binadamu ambaye hakosei. Inaelezwa kwamba, kukosea ni sehemu ya ukamilifu wa mtu. Mwanasaikolojia mmoja aliwahi kusema: “Ni vizuri watu wakosee ili wajifunze, huwezi kujua kitu bila kukosea, lakini unaruhusiwa kukosea mara moja tu!”
Kama ukichambua neno moja baada ya lingine la Mwanasaikolojia huyo, utaweza kuona jinsi sentesi yake fupi ilivyo na maana kubwa. Kwa mantiki hiyo hata kama utakosea mara mia moja, hakuna tatizo, lakini yawe makosa mapya. Kosea kila siku, lakini kitu kipya, hii inamaanisha kwamba, kwa sababu kukosea ni kujifunza, basi kama utakosea mara mia, utakuwa umejifunza pia mara mia moja. Upo hapo?
Sasa wanaume wengi hawapendi wanawake ambao wanakosea na kusahau! Jenga utaratibu wa kuheshimu unachoambiwa; Ukielezwa hakifai, usikaidi, huna sababu ya kurudia tena.
Kurudia kwako mara nyingi ni kuzidi kumkera mwezi wako ambaye lengo lako hasa ni kuishi naye hapo baadaye.
BADILIKA
Kama hayo yote hapo juu yanakuhusu ni wazi kwamba unatakiwa kufanya mabadiliko ya haraka sana katika maisha yako, kama ni kweli unataka kuolewa. Siyo rahisi mwanaume ambaye anatafuta mke akakubali kuwa katika uhusiano na mwanamke mwenye tabia zako.
Anza taratibu, rekebisha moja baada ya lingine, halafu kuwa makini katika kila jambo, mwisho wake utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata mwenzi wa maisha. Naamini somo limeeleweka, hadi wiki ijayo kwa mada nyingine, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is Your Valentine? vilivyopo mitaani.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake