ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 21, 2012

Mahakama yaionya CUF

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro.
Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imemtaka wakili Twaha Taslima wa Chama cha Wananchi (CUF) katika kesi ya kupinga kufukuzwa uanachama Mbunge wa Wawi Zanzibar, Hamad Rashidi Mohamed na wenzake 10, kuwasihi wateja wake kuacha kuendelea kukiuka amri iliyotolewa na mahakama hiyo.
 

Amri hiyo ilitolewa jana na Jaji Agustine Shangwa anayesikiliza kesi hiyo baada ya Tamimu Ally Tamimu aliyewahi kupewa barua ya onyo na CUF katika sakata la kuwafukuza uanachama wao kudai kuwa amekuwa akifanyiwa vitendo vya fujo na viongozi wa chama hicho.

Tamimu ambaye ni mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Tandale kwa Mkunduge kwa tiketi ya chama hicho, alidai kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julias Mtatiro, akiwa katika mkutano wa hadhara mtaani hapo aliwatangazia wanachama wa CUF kuwa amefukuzwa uanachama.

Alidai kuwa Mtatiro aliendelea kuutangazia umma huo kuwa wamempa siku 30 afunge ofisi yake kama mwenyekiti la sivyo atatuma watu waifunge kwa nguvu. 

"Nilishawahi kuvamiwa na wanachama wa CUF ofisini kwangu na kunivunjia samani zilizokuwemo, hali hii ni kuendelea kukiuka amri ya mahakama kwani wanaweza kusababisha uvunjifu wa amani," alidai Tatimu. 

Wakili Taslima alikiri kuwa vitendo hivyo ni kosa kwa sababu Tamimu hakufukuzwa uanachama bali alipewa barua ya onyo na kama anafanyiwa vitendo vya uvunjifu wa amani aende polisi kutoa taarifa.

Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa jana lakini iliahirishwa kutokana na wakili Augustino Kusarika wa Hamad na wenzake kushindwa kufika mahakamani kwa kuwa na udhuru wa kikazi.

Kesi hiyo itasikilizwa Julai 12, mwaka huu maombi ya walalamikaji mbunge Hamad na wenzake wanaoiomba mahakama iwaamuru viongozi wa CUF waitwe mahakamani kujieleza kwa nini wasitiwe hatiani na kufungwa kwa kupuuza amri ya Mahakama.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: