ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 9, 2012

Mapenzi ni fursa, iheshimu kwa maana haiji mara mbili-3

Na Luqman Maloto
Wiki iliyopita nilikueleza mfano wa Shadrack na Shania. Tuendelee nao kwa maana una mafundisho makubwa kwa watu wasioamini kwamba mapenzi ni fursa. Zingatia: Ukipata fursa ikamate inavyotakiwa, kinyume chake ni majuto.
Shania ni binti mrembo. Urembo wake ni wa hali ya juu mno. Amesifiwa na wengi kwamba mvuto wake unatosha kumshawishi kimapenzi mwanaume yeyote yule. Sifa zilipokuwa nyingi, kichwa kikamvimba, mabega akayapandisha. Akajiona yeye ndiye yeye, utamueleza nini?

Akiwa A-Level, alikutana na Shadrack, wakapendana. Kila mwanafunzi akajua uhusiano wao. Wenyewe wakapeana ahadi motomoto kuwa watafika mbali, huku wakila viapo vya kufunga ndoa na kudumisha mapenzi yao bila kuachana mpaka kifo kitakapowatenganisha.
Miezi sita ya uhusiano wao, Shadrack alimuona Shania na mwanaume lakini kutokana na namna anavyomuamini, wala hakumfikiria tofauti. Wakati Shadrack hakujali chochote, Shania kwa sababu lilikuwa tukio baya, alipokutana na mwenzi wake akaanza kujikanyagakanyaga.
“Unajua yule ni rafiki wa kaka yangu, hata nyumbani kwetu huwa anakuja,” Shania alishusha utetezi bila kuulizwa. Shadrack akauliza: “Unamuongelea nani?” Alipopewa majibu akashangaa. Akasema: “Hukuwa na haja ya kunifafanulia chochote, sijahisi chochote, wewe kaa na amani kabisa.”
Haikupita muda, Shadrack akagundua kwamba Shania anatoka kimapenzi na yule jamaa aliyemkuta naye. Ilimuuma sana, kwani walikuwa wamepeana ahadi nyingi mno. Mwisho akakubali yaishe kwa sababu maisha yanaendelea bila mapenzi. Akazingatia masomo yake.
Kumbe tabia ya Shania ni kuzingatia fedha kuliko utu. Hata alipoamua kujiweka kwa Shadrack ni kwa sababu alimuona ana unafuu wa kimaisha kuliko wanafunzi wengine wa kiume. Shadrack alikuwa anajiweza kiasi, vilevile darasani alikuwa vizuri, kwa hiyo kuwa naye akaona wanafunzi wenzake wa kike watamkoma.
Japokuwa anajiweza lakini Shadrack alikuwa mwanafunzi, kwa hiyo hakuwa na wigo mpana wa kipato kuweza kumhudumia Shania.
Hii ikasababisha Shania ampate huyo jamaa mbaye alikuwa mfanyakazi, ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Japo mshahara mdogo lakini aliweza kumudu kumpa huduma za hapa na pale.

Shadrack alipofika Chuo Kikuu, alipata ajira ya muda, hivyo akawa anapanga muda wa kazi na masomo. Asubuhi anakwenda kazini, jioni chuo. Kazini malipo yalikuwa si haba, hivyo kwa kipato, alimshinda yule mfanyakazi wa ofisi ya Mkuu Mkoa. Shania kuona hivyo akarudi tena kwa Shadrack.

Mapenzi yakendelea. Shadrack alijifanya kusahau yaliyopita lakini kila kitu kilikuwa akilini mwake. Alishajua kwamba Shania si mwanamke mwenye mapenzi ya kweli, ila humfuata pale anapoona mambo mazuri. Japo alikuwa na kinyongo, safari hii Shadrack alijitahidi kuonesha mapenzi makubwa kuliko mwanzo.

Alijitahidi kumjali zaidi, akahakikisha anatimiza kila hitaji la Shania. Siku za mwanzoni Shania alijitahidi kumuonesha Shadrack mapenzi ya kweli lakini kadiri muda ulivyosogea ndivyo ilivyothibitika kuwa mja asili hasahau asili yake. Shania alianza kumtesa kihisia mwenzake, Shadrack akawa mtu wa kulalamika.

Wakati Shadrack analalamika, Shania hakujirekebisha. Akikaa na marafiki zake wanacheka, anawasimulia jinsi wakiwa
chumbani Shadrack anavyomwaga machozi kwa ajili yake. Wenzake nao walishangilia, huku wakitamka waziwazi kwamba Shadrack ana tabia kama ya Bushoke. Eti ni mume bwege.
Kumbe Shania alikuwa na mwanaume mwingine anayeitwa Adili ambaye alimzuzua akili. Adili ni mfanyakazi wa kampuni moja ya bima, kwa hiyo kwa wakati huo alikuwa na kipato kikubwa kuliko Shadrack. Shania alisahau kila alichopanga na Shadrack, akaamua kumtesa.

Siku moja Shadrack alinasa ujumbe kutoka kwa Shania kwenda kwa Adili. Ujumbe huo ulikuwa ni malalamiko ya Shania akimlaumu Adili kwamba hamjali, anamtesa licha ya kwamba yeye anampenda sana. Ukiutazama ujumbe huo, kile anachokilalamikia Shania kwa Adili, hakitofautiani na malalamiko ya Shadrack kwa Shania.

Ukiutazama kwa makini ujumbe huo, ni kama Shania aliamua kuugeuza ujumbe wa Shadrack kwake, halafu akautuma kwa Adili. Shadrack aliumia kupita kiasi, akaona kumbe Shania hampendi ila anampenda Adili, kwani pamoja na kutendwa bado analalamika na anahitaji apewe nafasi.

Fuatilia Jumamosi ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: