Advertisements

Saturday, June 9, 2012

Marufuku kuuza damu


Serikali imewatahadharisha na kuwakemea wahudumu wa afya wote wenye tabia ya kuuza damu kwa wagonjwa kuwa hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.

Aidha hospitali zote zimeagizwa kuweka mabango yanayoonyesha kuwa damu haiuzwi, na wananchi wametakiwa kutoa taarifa kwa viongozi pindi wanapoona wahudumu wanauza damu.

Tadhari hiyo ilitolewa jana na Waziri  Dk. Hussein Mwinyi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakati akitoa tamko la wizara hiyo kuhusu maadhimisho ya siku ya wachangia damu salama duniani ambayo huadhimishwa kila Juni 14 ambapo kitaifa hafla hiyo itafanyika mjini Moshi mkoani Arusha.

"...wizara yangu inakemea na kulaani kitendo cha kuuza damu kwa wagonjwa wakati inapatikana bure kwenye kanda zetu..." alisema na kueleza kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ni 'kila mchangia damu ni shujaa'.


Dk. Mwinyi alisema kuwa tangu kuanza kwa mpango wa damu salama nchini 2004, kumekuwa na mafanikio mbalimbali yakiwemo ya ongezeko la vituo vya kanda kutoka vinne mwaka 2006 hadi vinane mwaka 2007.

Mafanikio mengine ameyataja kuwa ni ongezeko la ukusanyaji wa damu kutoka chupa 52,000 mwaka 2005 hadi 140,000 mwaka jana ambapo mahitaji halisi kwa mwaka ni wastani wa kati ya chupa 350,000 na 400,000 ingawa malengo yaliyopo katika kipindi cha mwaka huu na mwaka ujao ni kati ya chupa 180,000 na 200,000.

Alisema mafanikio mengine ni kupungua kwa kiwango cha virusi vya Ukimwi kwenye damu inayokusanywa na vituo vya damu salama kutoka asilimia saba mwaka 2005 hadi asilimia moja mwaka jana na uanzishwaji wa mfumo mpya wa teknolojia ya habari na mawasiliano unaosimamia shughuli zote za upatikanaji wa damu salama.

Hata hivyo, alisema kumekuwepo na changamoto nyingi zikiwemo za mahitaji makubwa ya damu kuliko upatikanaji wake, uelewa mdogo wa jamii kuhusu suala la uchangiaji wa damu kwa hiari, uuzwaji damu usio halali, matumizi yasiyo sahihi ya damu katika hospitali na miundombinu hafifu hasa ya barabara.

Dk. Mwinyi aliziomba taasisi mbalimbali na viongozi wa serikali, siasa, dini na jamii kushirikiana na serikali katika jitihada hizi ili kunusuru maisha ya wahitaji wa damu.

Kuhusu maambukizi ya Ukimwi, alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia kati ya tano na 10 ya maambukizi hayo husababishwa na mgonjwa kuongezewa damu yenye virusi vya ugonjwa huo ingawa yapo magonjwa mengine kama vile virusi vya homa ya ini na kaswende.

Maadhimisho hayo ambayo kidunia yanaadhimishwa mjini Seoul, Jamhuri ya Korea, madhumuni yake hasa ni kuwashukuru na kuwashawishi wachangiaji damu kujiheshimu ili waendelee kufanya hivyo, kuwatia moyo wasiochangia kufanya hivyo na kuwahimiza wafanyakazi wa huduma za damu kuwatambua wachangiaji.
CHANZO: NIPASHE

No comments: