ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 9, 2012

Ufisadi Machinga Complex balaa


Yapata hasara mil.14/- kila mwezi
Machinga Complex
Ufisadi uliojikita katika uendeshaji wa  kitega uchumi cha Jiji la Dar es Salaam cha Machinga Complex ni balaa kubwa kwani unalisababishia Jiji hilo  hasara ya Sh.milioni 14 kila mwezi.

Awali jengo hilo ambalo ni kituo cha biashara cha Wamachinga lilitarajiwa kukusanya mapato ya Sh milioni 313 kwa  mwezi, lakini ufisadi umesababisha lizalishe hasara sh milioni 14 kwa mwezi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Machinga Complex, Godwin Mmbaga, aliwaambia wanahabari jana jijini na kuongeza kuwa  kitega uchumi hicho kinakusanya mapato ya Sh milioni 5.2 kwa mwezi.


Hasara hiyo imetokana na ukiukwaji wa mipango ya uendeshaji wa jengo la Machinga Complex unadaiwa kufanywa uongozi wa  bodi ya mpito ya mradi huo, ambao ulisababisha Wamachinga waliokuwa wapangishwe kufanya biashara kukimbia na  kubakiwa na watu 50.

Kadhalika alisema licha ya hasara hiyo, mkopo wa ujenzi wa Machinga Complex uliokopwa kutoka Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulikuwa Sh bilioni 12.9  na sasa umefikia Sh. bilioni 31.5.

Hata hivyo, ilisema kuna utata katika suala la mkopo huo  na kwamba ameiagiza Halmashauri ya Jiji kukutana na NSSF kuzungumzia hoja hiyo.

Mwaka 2005 serikali ilipanga kujenga jengo hilo kwa gharama ya Sh bilioni 10 lakini kutokana na kupanda kwa gharama mradi huo ulitumia Sh bilion 12.9.

Mbaga alisema taarifa zinaonyesha kuwa NSSF inaidai Halmashauri ya Jiji Sh. bilioni 19.4 badala ya Sh bilioni 12.9 ambapo deni hilo likijumlishwa na  riba limekua na kufikia  bilioni 31.5.

”Jambo hilo lina utata katika deni hivyo Jiji wanatakiwa kukaa na NSSF na kulizungumza pia NSSF inatakiwa kukabidhi taarifa ya gharama ya mradi," alisema Mmbaga na kuongeza kuwa kilichofanyika ni  kukabidhi jengo kwa Jiji bila kuwasilisha mchanganuo wa  gharama.

Aliongeza kuwa jengo hilo halijakamilika na kwamba  linajaa maji wakati wa mvua na halina hewa na kuwasababisha wafanyabiashara kuishi katika mazingira magumu.

Akizungumzia ukiukwaji wa  taratibu za  uendeshaji mradi huo, alisema mambo yaliyotakiwa kufanyika hayakutekelezwa kwa mfano kushindwa kupata wapangaji 10,000 waliokuwa wamelengwa badala yake kupangisha watu 4,026.

Alisema idadi ilipungua kutokana na kuweka vizimba vya biashara hatua iliyoshusha idadi ya wafanyabiashara kutoka 10,000 hadi 4,026. Awali mradi ulilenga kujenga bila vizimba ili kutoa nafasi kwa wafanyabiashara wengi.

Ili kufidia hasara bodi iliongeza kodi kutoka Sh 30,000 hadi 60,000 kwa mwezi na kusababisha wafanyabiashara kulikimbia soko kutokana na kodi kubwa ambapo zaidi ya wafanyabiashara 2,000 walindoka na kurudi katika maeneo yasiyo rasmi.

"Walijikuta wakiondoka mmoja mmoja na kubakia wafanyabiashara 500 ambapo kati yao 450 wamekuwa wakifika, kufungua na kuondoka kwenda katika maeneo mengine kwa ajili ya kufanya biashara kwa sasa ndio hao wamebaki 50 ndio wanalipa kodi kwa wakati," alisema.

Alisema mradi huo ulikuwa na mpango wa kuwekwa maduka 128 ya  vivutio kwa wafanyabiashara lakini hayakuwekwa kutokana na kujenga vizimba.

Pamoja na kasoro hiyo Mmbaga alisema Bodi imebaini kuwa  nafasi ambazo zimetolewa kwa wafanyabiashara zilizidi licha ya kuwepo kwa idadi kamili ya vizimba.

"Jengo zima linatakiwa kuwa na watu 4,026 ila wapo wafanyabiashara 4,206 waliozidi ni 180 nadhani kuna baadhi ya vizimba vimegongana kuna wafanyabiashara wamepewa kizimba kimoja mara mbili," alisema.
Alisema tatizo jingine lililoibuliwa ni sehemu iliyotengwa kwa ajili ya maegesho ya magari ya kulipia  lenye uwezo wa kuhifadhi magari 100 limeporwa na kigogo wa Mamlaka ya Mapato (TRA) ambaye anaendesha mradi wa kuosha magari.

Alimtaja kigogo huyo kuwa ni A. Ngoda na kwamba hana mkataba wowote na  Manispaa ya Ilala pia halipii kodi kwa  Manispaa hiyo na kumtaka kuondoka kwani anaikosesha mapato serikali.

NIPASHE Jumamosi iliwasiliana na Ngoda kwa njia ya simu pamoja na kumtumia ujumbe mfupi lakini hakujibu wala kupokea simu.

Mbaga alisema changamoto inayoikabili bodi yake ni kukosa nguvu ya kuamua hatua zakuchukuliwa kutokana na sheria iliyopo na kwamba kazi yao ni kuishauri Halmashauri ya Jiji juu ya mradi huo.

Aliongeza kuwa wamelishauri Jiji kutafuta kampuni au taasisi binafsi  kusimamia mradi huo na pia kuangalia upya mikataba na  kurudisha mpango wa awali uliokusudiwa wa kuwaingiza wafanyabiashara 10,000 ili jengo  liweze kupata mapato badala ya  hasara.

Wakati huo huo, Mwenyekiti huyo alisema tayari ameagiza vizimba vilivyojengwa kwenye jengo hilo vianze kuondolewa ili kutoa nafasi kwa wafanyabiashara wengine.

 

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: