Kila kona ni kilio dawa hakuna
Nafuu iko mkoa wa D�Salaam tu
Nafuu iko mkoa wa D�Salaam tu
Uchunguzi kwa NIPASHE ulifanywa katika mikoa minane, umethibitisha pasi na shaka yoyote kuwa wazee wameachwa njia panda katika kupatiwa matibabu ya uhakika bure kama serikali ilivyoelekeza.
NIPASHE imebaini changamoto kubwa kuliko zote wanazokabiliana nazo wazee katika kupata matibabu ya bure ni upatikanaji wa dawa.
Hali hiyo imejidhihirisha kwa baadhi ya wazee wagonjwa ambao wanafika katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, lakini baada ya kufanyiwa vipimo wamekosa dawa na kulazimika kuzinunua wenyewe nje ya hospitali.
Wakizungumza na NIPASHE, baadhi ya wazee hao walisema kuwa pamoja serikali kuweka sera hiyo, lakini imeshindwa kupeleka dawa za kutosha hospitalini na wao kujikuta wakikosa dawa za bure.
DODOMA: DAWA ZA WAZEE HABA
Ezekiel Sumbe (93) alisema kuwa huduma za vipimo na kumuona daktari ni bure, lakini baada ya kupeleka vipimo kwa daktari alimuandikia dawa.
“Hapa tatizo ni dawa kwani vipimo tayari, lakini nimeenda dirisha la dawa hamna hivyo inanibidi niende kununua nje ya hospitali ambako zinatakiwa fedha…sisi kama wazee tunashindwa kuielewa hii sera,” alisema.
Ramadhan Selemani (68), mkazi wa Hogoro wilayani Kongwa, alisema kuna baadhi ya dawa ambazo wazee wanatakiwa kuzitumia, lakini hazipatikani hospitalini hapo.
Aidha, alisema kuwa wazee hawajaelimishwa kwamba wanapaswa kutibiwa bure wanapofika mapokezi na kulazimika kugharamiwa matibabu na watoto wao.
“Uwekwe utaratibu ambao mzee akifika OPD (idara ya wagonjwa wa nje) aandikiwe moja kwa moja kutokana na umri wake tofauti na ilivyo sasa mpaka upewe kibali cha kutibiwa bure kutoka kwa mama msamaha (ofisi ya ustawi wa jamii katika hospitali hiyo),” alisema.
Johe Rajabu (85) alisema alikosa dawa hospitalini hapo na kulazimika kwenda kununua nje na kuulalamikia utaratibu huo kuwa ni kero kubwa kwao.
Pamoja na ukosefu wa dawa, lakini pia alisema wamekuwa wakitumia muda mrefu kusubiri huduma na kuchoka.
Katibu wa Afya katika Hospitali hiyo, Isaac Kaneno, alithibitisha kuwepo na tatizo la dawa kwa magonjwa ya wazee ambayo hutumia dawa za gharama kubwa.
Alisema hali hiyo inatokana na serikali kutotengwa fungu maalum kwa ajili ya kununua dawa za wazee.
Alisema wazee wanatibiwa katika kitengo cha Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuondoa usumbufu na mgongamano.
“Ni bora serikali iangalie sera vizuri na kutoa fungu la fedha kama ilivyo kwa ule Mfuko wa Afya ya Jamii,” alisema.
MBEYA: NI KIINI MACHO
Mkoani Mbeya, baadhi ya wazee wamedai kuwa sera hiyo ni sawa na kiini macho kwa wazee, kwani kila wanapofika kwenye hospitali za serikali hutakiwa kutoa fedha ili wapewe huduma.
Suha Nyerema (74), mkazi wa kijiji cha Ihyela Nyara wilaya ya Mbeya Vijijini, alisema wiki iliyopita alikwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya na kutakiwa kutoa Sh. 10,000 ili kumwona daktari.
Alisema baada ya kujitetea kuwa yeye ni mzee na anastahili kutibiwa bure, aliambiwa arudi kijijini ili apewe barua na afisa mtendaji wa kijiji ya kuthibitisha kuwa anastahili matibabu ya bure.
Alisema kwa kuwa hali yake kiafya ilikuwa mbaya na nyumbani kwake ni mbali, aliona ni usumbufu mkubwa kurudi nyumbani, hivyo akalazimika kutumia fedha ya nauli kulipia gharama za matibabu.
“Niliona gharama ya kurudi nyumbani kuchukua barua ya mtendaji ni kubwa zaidi, hivyo nikaamua kutumia fedha ya nauli kulipia matibabu na sasa nimewatuma watu nyumbani wakawaambie wanangu waniletee nauli niweze kurudi,” alisema Bibi Suha na kwamba licha ya kulipa Sh.10,000 baada ya kumwona daktari na kupata vipimo, aliambiwa kuwa dawa anazotakiwa kutumia hazipo hospitalini na hivyo akanunue kwenye maduka ya watu binafsi kwa fedha zake mwenyewe, hali ambayo aliona kuwa amedhulumiwa.
Jonas Zitatu (72) mkazi wa kijiji cha Inyara alisema alipelekwa hospitalini hapo na mwanaye, lakini wafanyakazi wa hospitali walimtaka mwanaye awapatie fedha ndipo atibiwe.
Alisema hajui kama kuna utaratibu wa wazee kutibiwa bure, kwani kila anapougua huenda hospitalini na kutoa fedha ndipo anapewa matibabu.
Hata hivyo, alisema kuwa aliwahi kuambiwa na mzee mwenzake ambaye aliwahi kutibiwa bure, lakini alijua kuwa mzee huyo alitibiwa kwa sababu watoto wake wamesoma na wanafanya kazi serikalini.
Katibu wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dorice Nzigilwa, alisema katika hospitali hiyo upo utaratibu wa kuwatibu wazee bure na kuwa wazee wanaohitaji huduma hiyo wametengewa chumba maalum na kupewa daktari wao kwa ajili ya kuwasikiliza.
“Hapa hospitalini tumetenga chumba namba saba kwa ajili ya kutolea huduma za bure kwa wazee wenye umri wa miaka zaidi ya 60 ili kutimiza maagizo ya wizara.
Ndani ya chumba hicho yumo daktari ambaye kazi yake ni kuwasikiliza wazee tu,” alisema Nzigilwa.
Akizungumzia namna ya kuwatambua wazee hao, Nzigilwa alisema kazi hiyo hufanywa na Afisa Ustawi ambaye pia anayo ofisi yake ndani ya majengo ya hospitali hiyo kwa ajili ya kuwapokea wazee na kuwaelekeza cha kufanya kabla ya kuanza kupewa matibabu ya bure.
Ofisa Ustawi wa Jamii hospitalini hapo, Grace Ngairo, alisema kuwa wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 wamekuwa wakipokewa na kupewa huduma bure, ingawa ikitokea dawa wanazozihitaji hazipatikani hospitalini hapo hutakiwa kuzinunua nje ya hospitali kama ilivyo kwa wagonjwa wengine.
Alisema kigezo kikubwa cha wazee kupewa matibabu ya bure ni umri unaozidi miaka 60 na ili kuthibitisha hilo wazee hao hutakiwa kufika hospitalini hapo na barua ya afisa mtendaji wa kijiji au mtaa anakoishi.
Alisema ikitokea mzee amekwenda hospitalini hapo bila kuwa na barua hiyo, hutakiwa kwenda ofisini kwake ambako hupewa fomu maalumu inayomuwezesha kupata huduma zote hospitalini hapo bila kulipia chochote.
Hata hivyo, Ngairo alikiri kuwa hakuna elimu wala hamasa inayotolewa kwa wazee kuwajulisha taratibu za wao kufuata ili waweze kutibiwa bure na badala yake alisema kuwa wazee wengi hupeana taarifa hizo wao kwa wao.
Akitoa takwimu za wazee waliowahi kupata huduma za matibabu ya bure hospitalini hapo mwaka huu, Ngairo alisema kuwa Januari wazee 128 walitibiwa bure, Februari walikuwa wazee 152, Machi walitibiwa wazee 123 na Aprili wazee waliotibiwa bure hospitalini hapo walikuwa 139.
Katika Hospitali ya Rufaa Mbeya uchunguzi wa NIPASHE umebaini kuwa hakuna dirisha wala chumba maalum inachoshughulikia matibabu ya bure kwa wazee na wote wanaokwenda kutibiwa hospitalini hapo hutakiwa kuchangia gharama za matibabu kama ilivyo kwa wagonjwa wengine.
Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Eliuter Samky, alithibitisha kutokuwepo kwa dirisha la wazee kwa madai kuwa hiyo ni hospitali ya rufaa inayopaswa kupokea wagonjwa kutoka katika hospitali za chini, ambako wazee hao wanapaswa kuanzia.
Alitoa mfano kuwa yeye ni daktari bingwa wa mkojo, hivyo asilimia kubwa ya wagonjwa anaowatibu ni wazee, hali ambayo inamfanya haoni umuhimu wa kuwa na dirisha la wazee pekee.
Uchunguzi wa NIPASHE umebaini kuwa kwa mgonjwa yeyote, wakiwemo wazee anayekwenda kutibiwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya hutakiwa kwanza kulipa mapokezi Sh. 15,000 ndipo apewe huduma nyingine ikiwemo kumwona daktari.
TANGA: HAWAIELEWI SERIKALI
Mkazi wa Kata ya Mwembesongo, mkoani Morogoro, Halifa Abdallah (71), mstaafu wa Shirika la Reli, alisema wanaendelea kununua dawa katika vituo vya afya na hospitali.
“Serikali ilitangaza sisi wazee tutengewe sehemu zetu katika kila hospitali na tupatiwe huduma bure ikiwemo dawa, lakini tunapokwenda hospitali unambiwa vipimo vingine unatakiwa kulipia na dawa unaambiwa hakuna hivyo inakubidi ukanunue kwenye maduka ya dawa, tunashindwa kuilewa serikali yetu,” alisema.
Mwanahamisi Ali (66), mkazi wa kata ya Kichangani, alisema tangu kutangazwa kwa mpango huo hakuna huduma zozote wanazopata bure katika hospitali zaidi ya kumuona mganga na kuishia kuandikiwa dawa huku wakitakiwa kwenda kununua.
“Alikuja Waziri Pinda siku ya wazee kitaifa, tulimpa malalamiko yetu kuhusu huduma za afya, akaagiza tupatiwe vipimo bure na dawa, lakini ukienda hospitali sanasana unambulia kuandikisha cheti na kumuona daktari, lakini dawa unambiwa hakuna,” alisema.
MOROGORO: KILIO NI DAWA
Mkurugenzi wa shirika kutoa huduma kwa Wazee katika Mkoa wa Morogoro (Moropeo), Samson Msemembo, alisema baadhi ya hospitali katika Mkoa wa Morogoro zimeitikia agizo hilo la Waziri Mkuu kutenga maeneo ya kuhudumia wazee, lakini kikwazo kimekuwa katika upatikanaji wa matibabu hasa dawa.
“Kuna hospitali zimetenga madirisha ya kuandikishia wazee na madaktari mfano ni hospitali ya mkoa na zile za wilaya, lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa dawa, wazee hawa wanambiwa waende kununua katika maduka ya dawa hakuna bajeti hiyo,” alisema Msemembo.
Alisema shirika hilo limekuwa likipokea malalamiko mengi kutoka kwa wazee kuwa wanapoenda kupata matibabu katika hospitali hizo wanaambiwa hakuna dawa na wanapaswa kwenda kujigharimia.
Aliitaka serikali kumaliza tatizo hilo kwa kuzisimamia halmashauri zake kuanzisha mfuko wa afya ya jamii na kuwaingiza wazee hao kupatiwa matibabu hayo kutokana na wengi kutokuwa na uwezo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Godfrey Mtei, alikiri kuwepo kwa ukosefu wa dawa katika sehemu zinazotengwa kwa ajili ya kuhudumia wazee kutokana na ufinyu wa bajeti na kuongeza kuwa wanakusudia kuwaingiza wazee hao katika NHIF na ule mfuko wa afya ya jamii.
IRINGA: URASIMU KERO
Baadhi ya wagonjwa wazee wanaopatiwa tiba katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa wameulalamikia utaratibu mzima wa matibabu kutokana na kukosa dawa na kuchukua muda mrefu hospitalini hapo.
Prosper Malangalile (68), alisema awali alikuwa akipata matibabu katika hospitali hiyo kwa kupitia Bima ya Afya, lakini amelazimika kuhamia katika hospitali nyingine ili kuepukana na urasimu.
Alisema hata mgonjwa akipata fursa ya kufika kwa muuguzi, anaambiwa kuwa hakuna dawa na kulazimika kwenda kutafuta njia nyingine ya kupata dawa hizo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Deogratias Manyama, alisema: “Kama kunatokea malalamiko ni vizuri wangeyaleta katika uongozi ili yapatiwe ufumbuzi.”
Alisema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wauguzi na kulazimika kutumia muuguzi mmoja katika idara nzima na kwamba uongozi utaomba kuongezewa watumishi ili kukabiliana na changamoto hiyo.
KILIMANJARO: HAKUNA DAWA
Ukosefu wa dawa pia unaelezwa na wazee wanaoitibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi ambao wanasema kuwa wamekuwa wakilazimika kwenda kuzininua katika maduka binafsi.
Neema Mushi (65) na Elirehema Msangi (70), walisema licha ya jitihada za serikali kuweka dirisha maalum kwa ajili ya kuhudumia wazee bure, lakini kikwazo ni kukosa dawa na kutakiwa kuzinunua.
“Tunaiomba serikali kuboresha huduam za afya kwenye hospitali za serikali, unakuja hospitalini unapata huduma za kumuona daktari, tunashukuru serikali kwa kuweka dirisha hili, ila tunaomba kuwe na dawa, sisi wazee hatuna uwezo wa kununua dawa,” alisema Mushi.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mawenzi, Dk. Saganda Kipalapala, alisema hospitali hiyo imetekeleza agizo la serikali la kuwa na dirisha maalum kwa ajili ya kuhudumia wazee ambalo lipo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, lakini changamoto wanazokumbana nazo ni kukosekana kwa dawa kutokana na bajeti ndogo na kushindwa kutosheleza makundi yote yenye msamaha wa kutolipia matibabu.
ARUSHA: WAPEWA BIMA
Katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, wagonjwa wazee wametengewa sehemu maalum inayotoa huduma kwa njia ya bima ili kuwaharakisha huduma.
Mganga Mkuu wa hospitali ya Mount Meru, Dk. Omar Chande, alisema: “Walitakiwa wawe na dirisha lao, lakini sisi tumeamua wazee hao wapokelewe kwenye sehemu inayotoa huduma ya matibabu kwa bima. Wakishapokewa hapo tumewatengea sehemu maalum pia ya kupokelea dawa.”
MUHIMBILI: HUDUMA BURE
Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wazee wanasema kuwa wanapata matibabu ya bure bila kuchangia chochote.
Hamis Ngirini (68) alisema kila akifika Muhimbili anapewa huduma bure ilimradi awe amefuata masharti waliyoweka.
Ngirini alisema alienda kwa mjumbe wa serikali za mitaa na kupewa barua ya utambulisho ambayo huwa anaitumia kuwaonyesha wahudumu pindi anapoenda kupata matibabu.
Afisa Uhusiano Msaidizi wa Muhimbili, Jezza Waziri, alisema huduma hiyo inatolewa kwa wazee baada ya kuangalia barua ya utambulisho kutoka ofisi ya serikali za mitaa.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE katika hospitali za Manispaa ya jiji la Dar es Salaam, umebaini kuwepo kwa unafuu huo ambapo wazee wanaendelea kupewa matibabu ya bure.
TEMEKE: UNAFUU MKUBWA
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Temeke, Zaitun Mgaza, alisema wazee wanapata huduma za bure kwa kufuata taratibu.
Alisema katika hospitali yake kuna mtu maalum wa kuhakikisha wanapata huduma nzuri na za bure.
AMANA, MWANANYAMALA POA
Kwa upande wa Hospitali ya Mwananyamala, mmoja wa wauguzi aliliambia NIPASHE kwamba wazee hawalipi wanapofika hapo kwa ajili ya kupata matibabu.
Alisema kuwa utaratibu huo unajulikana kwa kila mtoa huduma hospitalini hapo. Katika hospitali ya Amana, NIPASHE lilishuhudia baadhi ya wazee waliokuwa katika mstari wakisubiri kupatiwa huduma za afya na baada ya kuulizwa kama wanalizipia walisema hawalipii.
“Sisi hapa tunakuja kutibiwa kwa muda mrefu na hatulipi kitu chochote kwa hili tunashukuru serikali yetu kwa kutuondolewa gharama hizi ambazo kama zingekuwepo huenda tungeshindwa kuzimudu,” alisema Ayoub Yusuf (70).
Hata hivyo, alilalamikia kuchelewa kufanyiwa vipimo kama vya X-Ray na Ultrasound kutokana na urasimu wa watoa huduma.
KAULI YA WIZARA
Kutokana na malalamiko hayo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesisitiza kuwa imeziagiza hospitali zote za umma nchini kuzingatia huduma ya dirisha la matibabu kwa wazee, wajawazito, na watoto waliochini ya umri wa miaka mitano ili kwenda sambamba na sera ya taifa ya matibabu bure kwa makundi hayo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya katika vituo vya umma na binafsi, Dk. Edwin Mung’ong’o, ameliambia NIPASHE kuwa wahudumu wengi walioko katika hospitali za umma hawajafahamu kwa undani huduma ya bure ya matibabu kwa wazee na kinamama wajawazito, hali inayosababisha kuzorota kwa huduma hiyo katika hospitali hizo.
Alisema serikali ilianzisha huduma hiyo kutokana na hali mbaya ya kiuchumi hivyo kuona sababu ya kuondoa gharama za matibabu kwa wajawazito na wazee ili kupunguza idadi kubwa ya mama wajawazito kujifungulia majumbani.
Aliongeza kuwa katika kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufasaha, wizara imeweka mikakati ya kuzungukia hospitali hizo nyakati mbalimbali na utoaji ushauri kwa hospitali hizo ziwe na siku ya wadau katika kujadili matatizo yanayowakabili.
Aidha, alisema tatizo la dawa ni mojawapo ya changamoto inayoikabili serikali kutokana na ufinyu wa bajeti kunakopelekea hospitali hizo kukosa dawa na kuzua malalamiko kutoka kwa walengwa hao.
“Wengi wao wanapopata huduma ya vipimo, kuandikiwa matibabu pamoja na huduma nyingine hospitalini, lakini wanapoambiwa hakuna dawa hizo huanza kulalamika na kusema wanaonewa,” alisema Dk. Mung’ong’o.
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya hospitali hazina huduma ya matibabu ya bure kwa wazee na nyingine zinayo na kwamba kwa sasa serikali inapanga mikakati ya kuboresha huduma hiyo.
Kwa mujibu wa sera ya taifa ya mwaka 1990 pamoja na marekebisho ya mwaka 2007, wazee wote wenye umri wa miaka 60 ambao hawana uwezo, wanatakiwa kutibiwa bila gharama yoyote.
Makundi mengine ambayo yanatakiwa kupatiwa huduma za matibabu bure ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano, kina mama wajawazito na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wenye magonjwa sugu.
Imeandikwa na Agusta Njoji, Dodoma; Emmanuel Lengwa, Mbeya; John Ngunge, Arusha; Salome Kitomari, Moshi; Ashton Balaigwa, Morogoro; Gwamaka Alipipi, Richard Makore, Dar; Vick Macha, Iringa na Mwandishi Wetu, Tanga.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment