ANGALIA LIVE NEWS
Monday, June 4, 2012
Yaya Toure, Kalou wamvulia kofia Samata
Edo Kumwembe, Abidjan
NYOTA wa kimataifa wa Ivory Coast, Yaya Toure wa Manchester City na Solomon Kalou wa Chelsea wamekoshwa na kipaji cha mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samata baada ya kuichachafya vilivyo ngome ya Tembo hao juzi katika pambano la kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2014.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Yaya na Kalou walisema Samata ana kipaji cha hali ya juu cha kucheza katika timu yoyote kubwa barani Ulaya.
“Yule namba 10 (Mbwana Samata) ni hatari sana. Ana uwezo mkubwa sana, anacheza wapi yule? Kama tusipokuwa makini basi atafunga katika kipindi cha pili,” alisema Toure wakati wa mapumziko ya kwenye uwanja wa Felix Houphouet-Boigny.
Alipoulizwa uwezekano wa Samatta kucheza Ulaya, Toure alijibu, “ni juhudi zake tu, siwezi kusema lolote kwa sababu inabidi ufanye juhudi zaidi kucheza Ulaya, lakini ana kipaji kikubwa.”
Kama vile haitoshi, wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika chumba kimoja cha uwanja huo, Kalou aliyekuwa amefuatana na kocha wake, Sabri Lamouchi alionekana kushangazwa na uwezo wa Samata wakati alipoulizwa swali na mwandishi wa gazeti hili kuhusu mchezaji aliyemvutia zaidi uwanjani.
“Ni Yule mchezaji aliyevaa jezi namba 10. Uwezo wake ni mkubwa sana na kama akijiendeleza nadhani atafika mbali. Ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira ni hatari sana,” alisema Kalou.
Samata alipohojiwa kuhusu maoni ya nyota hao akiwa katika hoteli ya Ibis Plateau ilipofikia Stars jijini Abidjan, alijibu kwamba hakushangazwa na hali hiyo kwa sababu hata wakati akiwa uwanjani, mlinzi wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Eboue anayechezea Galatasaray ya Uturuki alimwambia hatashangaa kumuona Ulaya.
“Sishangai sana kwa sababu wakati tunacheza wakati fulani Eboue alinifuata na kuniambia hatashangaa siku akinikuta kiwanjani barani Ulaya,” alisema Samatta huku akicheka.
Katika pambano la juzi, achilia mbali Samata, wachezaji wa Stars walionyesha kiwango kizuri kwa ujumla tofauti na walipocheza katika pambano la kirafiki dhidi ya Malawi Mei 26 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
KUNDI C
P W D L F A Pts
Ivory Coast 1 1 0 0 2 0 3
Morocco 1 0 1 0 1 11
Gambia 1 0 10 1 1 1
Tanzania 1 0 0 1 0 2 0
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment