ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 21, 2012

Moshi waonja machungu ya mgomo wa daladala




Huduma ya usafiri wa daladala katika Manispaa ya Moshi jana uliparaganyika na kusababisha adha kubwa kwa wakazi wa manispaa hiyo kwa saa nane baada ya madereva kugoma tangu alfajiri.

Madereva na makondakta wa daladala hizo waligoma kwa kile walichodai ni Manispaa hiyo kupandisha ushuru wa magari eneo la kituo kikuu cha mabasi kutoka Sh. 1,000 hadi 1,500.

Kutokana na hali hiyo, watu waliokuwa wanakwenda kazini na sehemu nyingine za biashara walialazimika kutumia usafiri wa teksi na bodaboda humu wengine wakitembea kwa miguu.


Mgomo huo ulikuwa neema kwa bodaboda na teksi kwani walikuwa wakisafirisha abiria kwa gharama ya Sh. 1,000 hadi 3,000 kulingana na eneo unalokwenda.

Kwa mfano, katika kituo cha daladala kilicho mbele ya Makao Makuu ya Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) magari aina ya Toyota Noah yalionekana yakipakia abiria kwa nauli ya Sh. 1,000 hadi eneo la Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa kila abiria.

Neema Michael na Elisante Massawe, walisema kuwa walilazimika kutumia usafiri wa bodaboda ili kufika mjini.

“Hapa nilipo sijui nitasafiri muda gani, kwa zaidi ya nusu saa nipo hapa kituoni, nimetoka Soweto, nimepanda bodaboda  kwa Sh. 1,500 badala ya Sh. 1,000 iliyozoeleka kila siku,” alisema na Neema kuongeza:

"Natakiwa kwenda kazini KCMC, lakini teksi na Noah wanasema bila Sh. 1,000 hawapakii,  kwa hiyo nitatumia Sh. 2,500 na kurudi ndiyo sijui.”

Wakizungumza na NIPASHE, baadhi ya madereva, Nickson Giliadi, Soka Sitena Michael Tadei, walisema manispaa hiyo imetangaza kuwa ifikapo Julai Mosi, mwaka huu, ushuru wa daladala utapanda hadi Sh. 1,500.

Walisema kwa mahesabu ya haraka msafirishaji anatakiwa kuilipa Manispaa hiyo zaidi ya Sh. 547,500 kwa mwaka huku wakidaiwa fedha ya stika ya Sh. 10,000 na kifaa cha kuzimia moto
kinachotolewa na Idara ya Zimamoto ya manispaa hiyo.

“Mara nyingine unapewa karatasi yaani stika baada ya kuwapa fedha yao, lakini kifaa hupewi, huu ni uhuni, ni kwa nini tozo la ushuru kwa Manispaa hii lipo juu zaidi kuliko miji mingine kama Arusha, Dar es Saalam na Mwanza, tunataka ipungue hadi Sh. 500,” alisema Giliadi.

Aidha, madereva hao walikusanyika katika eneo la Manyema huku wakifunga barabara, hatua iliyowalazimisha askari wa usalama barabarani kufika na kuwatuliza bila mafanikio hadi viongozi mbalimbali walipofika.

Baadhi ya viongozi hao ni mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani, Christoper Lyimo na Meya wa Manispaa hiyo, Michael Jaffary ambao walikubaliana kufanyika kikao cha dharura kujadili suala hilo.

Hata hivyo, madereva hao waligoma wakitaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bernadetta Kinabo, kufika eneo hilo ili awasikilize kwa kuwa amekuwa akitoa maamuzi ya kupanda kwa ushuru huo bila kuzingatia hali halisi.

Walidai kuwa kwenye eneo la Manyema wanapoegesha magari hakuna huduma ya choo na kumekuwa na majitaka yanayobubujika kwa wingi na kutoa harufu kali.

“Wanatutoza fedha na kila wakati wanazidisha, lakini hatuoni huduma nzuri, hapa hakuna choo na majitaka yanatiririka ovyo mtaani, fedha hizo zinaelekezwa wapi kama siyo kutoa huduma na kuboresha huduma kama za choo na nyinginezo kwenye vituo?” alihoji Tadei.

Walisema madiwani wa manispaa hiyo wamewasaliti kwani wamekubali ongezeko hilo bila kuwahusisha na kujali ongezeko la gharama nyingine za usafirishaji zikiwemo za vipuri.
Uongozi wa manispaa ulikutana na wamiliki na wadau wengine kusikiliza malalamiko yao.

Meya Faffary akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, alisema walikutana na wamiliki na wadau wengine wa usafiri na kujadili kwa kina na kuona madai mengine ni ya msingi na kuagiza menejimenti ya manispaa ikae na kutoa ufumbuzi.

Alisema suala la tozo la stika linafuatiliwa kwa kina kwa kuwa ni suala la kisheria zaidi, na kwamba majibu yatapatikana Juni 25, mwaka huu.

Mmoja wa wasafirishaji, Sanifa Nkya, alisema wamekubali kurudi kutoa huduma majira ya saa 8:00 mchana baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichowakutanisha wadau na manispaa, ambacho walielezea kero zao na kupokelewa na kwamba kikao kingine kitafanyika Jumatatu ijayo ili kupokea majibu ya manispaa.

Nkya ambaye pia ni Mwenyekiti wa njia ya Kiborloni, alisema upandaji wa gharama hizo haujazingatia wala kumjali msafirishaji kwani gharama za vipuri na mafuta zinazidi kupaa na huku manispaa ikiongeza ushuru mkubwa bila kuwajali.

Wakati wote wa mgomo, polisi walikuwa wakilinda doria katika maeneo mengi ya Manispaa kuhakikisha kuwa hazitokei vurugu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alithibitisha kuwepo kwa mgomo huo na kueleza kuwa jukumu lao ni kulinda amani na kwamba wanaopaswa kuutatua mgomo huo ni uongozi wa Manispaa.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: