ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 4, 2012

NENO LA LEO: NCCR-MAGEUZI ACHENI KUPIGA MAYOWE, ACHENI UMMA UONE WENYEWE!


Ndugu zangu,
NCCR- Mageuzi wamewajia juu wapinzani wenzao, Chadema. Wanawashutumu Chadema kwa kuwaita NCCR- Mageuzi ' CCM 'B'!
Tumemsikia Mbunge Machali akionyesha machachali yake ya kisiasa. Naye amewaita Chadema ' mahayawani' Neno ' hayawani' lina maana ya ' mnyama'- mtu kuitwa hayawani ina maana ya mtu ' mshenzi'- usiyestaaribika kama alivyo mnyama. Nalo ni tusi, si ajabu nao Chadema wakaja na kauli ya kuwataka NCCR- Mageuzi wawaombe radhi kwa kuwatukana hadharani!
Lakini tuanze na aliyeanza; Machali wa NCCR- Mageuzi anasema; Chadema, ama wawaombe radhi hadharani vinginevyo NCCR - Mageuzi inaweza kuwapeleka mahakamani. Ndio, kiduku cha kisiasa kimechanganya . Naam, siasa ni burudani pia.

Nionavyo, NCCR- Mageuzi hawana sababu ya kutoka na kupiga mayowe hadharani. Walichopaswa ni kufanya kinyume chake, kuwaimbia wenzao; " Chadema , acheni kupiga mayowe, acha umma uone wenyewe!"
Ni kazi ya NCCR- Mageuzi sasa kuonyesha umma kuwa wao si ' CCM 'B''- Full stopp! Tumemwona David Kafulila leo magazetini - Kafulila kapambana vikali kuishutumu kamati ya Maadili ya Bunge juu ya sakata la mbunge wa CCM kupokea rushwa ya milioni moja. Ametishia kujitoa kwenye kamati hiyo.
Na jana kwenye runinga Kafulila kasema, ili kulinda heshima ya Bunge, itungwe sheria kwa mbunge anayepokea rushwa na kufikishwa mahakamani avuliwe ubunge na aende mahakamani kama raia wa kawaida.
Ndio, Kafulila ameonyesha, kuwa kama kuna wanaodhani NCCR- Mageuzi ni CCM' B', basi yeye hayumo kwenye timu hiyo. Wengine ndani ya NCCR- Mageuzi wafuate nyayo za Kafulila.
Chama cha upinzani kionyeshe wazi kuwa ni chama cha upinzani na si cha upinzani kwa wapinzani wenzake. Hilo la mwisho hata kama kisipoitwa ' CCM 'B' na wapinzani wenzake, kijue, kuwa Watanzania wa leo si wa jana. Wanatembea na ' mihuri' yao mifukoni. Wanatafakari kauli na misimamo ya wanasiasa na vyama vya siasa , kisha wanagonga 'mihuri' yao- kimyakimya wakisubiri 2015.
Naam, NCCR- Mageuzi kina uzoefu wa miaka mingi kwenye siasa za upinzani. Ichunge sasa, isije NCCR- Mageuzi ikawa NCCR- Manung'uniko! Hili la kuitwa ' CCM B' na Mbunge Wenje wa Chadema ni issue ndogo kisiasa .
Kwa NCCR- Mageuzi kuikuza vile kumezidi kuwafanya wapiga kura wahisi ina ukweli ndani yake. Maana, kwa wanasiasa na vyama kukebehiana majukwaani ni jambo la kawaida.
Kwenye uchaguzi uliopita tumesikia hata wapinzani wakiitwa ' fotokopi' ya CCM! Hakuna hata mpinzani mmoja aliyeonekana kwenye ofisi ya wakili kutaka kufungua mashtaka ya kudharauliwa kwa kuitwa ' fotokopi'.
Si tunaona leo, huyo aliyetamka wapinzani ni ' fotokopi' anakaa na kunywa chai na hao ' fotokopi' huku wakizungumza masuala ya Katiba!
Afrika 'origino' inaweza kuanzia na 'fotokopi'! Mwanasiasa usikonde kwa kuitwa ' fotokopi'. CCM 'B' yaweza kuwa na maana ya ' fotokopi' ya ' A'. Na katika siasa ' A' inaweza kuwa ' fotokopi' ya 'B'. Ni kujua tu namna ya kuchanga karata za kisiasa.
Ndio maana ya kusema, siasa ni burudani pia. Na kuna mwanasiasa ambaye anapaswa kupigiwa mfano. Mimi namkubali sana Nape Nnauye. Huyu jamaa hata atukanwe vipi. Atajikung'uta na kurudi tena kupambana jukwaani. Humsikii Nape kuzungumzia lugha ya kuwafikisha mahakamani wanaomkebehi yeye binafsi au chama chake.
Na jana Nape akiwa Songea kanifanya nicheke sana alipowaita wana- CCM wenzake wanaokwenda upinzani kuwa ni ' Oil chafu!' Sisi tunaoendesha magari mabovu mabovu tunajua haswa maana ya ' Oil chafu'.
Na katika hilo Nape anatuambia kuwa CCM inapopoteza wanachama wake ni sawa na chama hicho ' kumwaga Oil chafu'.
Na je, wanachama hao hao , wanapobadilika tena na kurudisha kadi za Chadema na kujiunga na CCM ina maana ni ' Oil chafu' iliyojisafisha yenyewe au kusafishwa na Chadema?!
Haki ya Mungu, siasa ni burudani pia!
Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765

No comments: