ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 18, 2012

USISTADUU, UBRAZAMENI NA MAPENZI YA KICHINA -5

MDAU wa safu hii, leo naendelea na makala haya yahusuyo Usistaduu, Ubrazameni na Mapenzi ya Kichina ambayo naamini yatakuweka sawa kwa namna moja au nyingine. Tuwe pamoja...
Hapa nikupe angalizo kwamba ni bora uwe huaminiki au imani ya watu kwako iwe ya wastani. Endapo watu watakuwa na imani kubwa kwako, siku wakigundua una nyendo chafu za siri, heshima yako hupotea kabisa. Kama huaminiki, watu watasema ni kawaida yako. Waliokuamini wastani nao watanena hukuwa ukiaminika asilimia 100, hivyo halitakuwa gumzo.

Unapokuwa unaaminika kwa asilimia 100, maana yake hakuna shaka yoyote kwa watu juu yako. Hivyo basi, unapoboronga, heshima yako itashuka kwa kasi. Mitaani simulizi utakuwa wewe, kwani ni jambo geni na halikuwahi kutabiriwa kwako. Tafadhali, ishi maisha yako, usiishi maisha bandia. Utaumbuka.
Vivyo hivyo kwenye mapenzi. Mpenzi wako anayekupenda na kukuamini kupita kiasi, siku ukimtenda ndivyo sivyo, atakaa na maswali mengi kwa muda mrefu. Utageuka kinyaa mbele yake, kwa hiyo hata kukusamehe atapenda kufanya hivyo lakini atachelewa kwa sababu heshima yako kwake, imeondoka kabisa.
Pili; mapenzi yenu ni kama mnalazimisha. Hampendani kabisa au yeye hakutaki, kwa hiyo anaona hiyo ni fursa ya kukuadhibu. Utashangaa umemkosea jambo dogo lakini anavyolisimamia utadhani umeua mtu. Kama sura ya aina hiyo, inajiri kwenye uhusiano wake, jaribu kutazama mbele kwa matumaini. Hakupendi, atakupotezea muda.
Kila siku wauza magenge na maduka, wanaingilia ndoa za watu. Nafasi hizo wanazipata kwa sababu ya kutokuwepo ubize kwa wanawake hao. Asili yetu tunapenda utani, hivyo wakitaniana mara mbili, mwanamke anahama kihisia. Keshokutwa asubuhi mume akiondoka, huyu anakimbilia gengeni.
Huu ni mfano katikati ya mada yetu. Mtu wa aina hii akiwaona machangudoa barabarani, atawalaani kupita kiasi. Hata hivyo, mtindo wa maisha yake hauna tofauti na changudoa kutokana na ukweli kwamba mtu mwenye staha na heshima, hawezi kujilimbikizia vidumu. Mume usiku, mchana muuza bucha au houseboy, haijakaa vizuri.
Inabidi kutoa mfano wa aina hii kutokana na ukweli kwamba masistaduu wanaweza kukaa vibarazani na kusogoa kuwa mbona wake za watu wanaojionesha ni watu makini, nao wanacheza sana mechi za nje? Wanadanganywa nao wanadanganyika. Maisha yanaendelea, mke wa mtu anaitwa fuska pasipo yeye mwenyewe kujijua.
Dunia ilivyo ni kwamba huwezi kutoka kimapenzi na mtu halafu ikabaki kuwa siri. Iwe isiwe lazima itavuja. Japo maneno yanaweza yasifike kwa mumewe lakini kwa watu baki watamzodoa au kumsogoa kila anapopita. “Yule ni mke wa mtu lakini tabia zake chafu”
Wapo watakaozungumza: “Yule mwanamke hana kinyaa, ana mume lakini utadhani changudoa kwa jinsi anavyoisaliti ndoa yake.” Wewe hutayajua hayo unayosemwa, utajioni upo vizuri ukiamini unayofanya hayaonekani. Kwa kudhani nyendo zako za siri hazijulikani, utawalaani machangudoa wanaojiuza mitaani.
Hapa namaanisha kuwa wakati tunawaweka sawa masistaduu, inapendeza lile kundi la wanawake wanaojiona wapo makini wakawa mfano wa kuigwa.
Waache tabia za mafichoni, hadharani kujionesha ni watu wazuri kimaadili, wakati gizani wao ni wachafu kuliko hata hao wanaoonekana.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: