ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 29, 2012

Fahamu nafasi ya uongo katika mapenzi!



KUONGOPA si jambo zuri katika maisha. Wakati mwingine unaweza kudanganya na kushindwa kuweka rekodi vizuri, matokeo yake baadaye unaingia kwenye aibu baada ya kugundulika kuwa ulidanganya.
Pamoja na ukweli huo, uongo una nafasi kubwa sana katika mapenzi. Najua unaweza kuchanganywa na maneno yangu, lakini ndiyo ukweli wenyewe. Uongo ni muhimu katika kuboresha penzi.
Inawezekana unajiuliza: “Huyu Shaluwa vipi tena? Yaani anafundisha watu wawe waongo. Wawadanganye wapenzi wao?”

Ni sahihi kujiuliza swali hilo, lakini nataka kukuhakikishia rafiki yangu, uongo kwenye uhusiano una nafasi yake ila inategemea unadanganya nini kwa sababu gani! Upo hapo rafiki?
Kwa kawaida uongo unakatazwa kuanzia kwenye mafundisho ya dini na hata katika jamii. Mtu muongo si mwaminifu. Hakubaliki.
Hata mwanasiasa ambaye ni muongo, wapiga kura wake hawamchagui tena atakaporudi mara ya pili; kwa nini? Kwa sababu aliwaongopea. Hiyo ni kweli kabisa, lakini hapa katika Let’s Talk About Love nataka kukupa kitu kipya kabisa ambacho hujawahi kukipata mahali popote; uongo mtamu!
DHANA YA KUONGOPA
Rafiki zangu, sitaki kueleweka vibaya katika hili lakini kama nilivyosema mwanzoni uongo si kitu kizuri kwenye jamii. Mtu anayedanganya hakubaliki. Kwa tafsiri ya haraka, muongo si mwaminifu.
Haaminiki kwa sababu ni rahisi kutunga mambo ambayo hayapo na akayatengenezea mazingira yakaonekana ni ya kweli. Huyu hafai hata kidogo. Lakini rafiki zangu, katika uhusiano upo uongo ambao unakubalika.
Nasema unakubalika maana una lengo la kutengeneza uhusiano, kuufanya uendelee kuwa na nguvu na si kuupoteza. Huo ndiyo uongo unaokubalika. Kabla sijaenda mbele zaidi hebu twende tukaone kwanza tofauti ya uongo unaokubalika na usiokubalika.
UONGO USIOKUBALIKA
Haikubaliki hata mara moja kumdanganya mpenzi wako kuhusu taarifa zako muhimu. Nasema hivyo kwa sababu utakuta mwingine anafanya kazi mahali fulani, lakini kwa sababu ya kutaka ukubwa anadanganya kwamba anafanya kwenye taasisi fulani kubwa.
Wapo wanaodanganya wanatoka katika familia zenye uwezo mkubwa kifedha, huku wengine wakijipachika majina ya koo maarufu ili waheshimiwe na wapenzi wao, huo ni utumwa, mbaya zaidi kuna siku ukweli unajulikana halafu unabaki na aibu zako. Kuwa mkweli.
UONGO UNAOKUBALIKA
Upo uongo unaokubalika rafiki zangu. Unajua kuna baadhi ya mambo ukiyasema kwa usahihi kama yalivyo yanaweza kuleta athari kwenye uhusiano, ndiyo maana nimesema kwamba upo uongo unaokubalika.
Inawezekana umefanya kitu ambacho hakimpendezi mpenzi wako, ama kwa kujua au kutokujua, lakini baada ya kuhisi labda amegundua na kukuuliza, unakataa. Ukikubali kwa kitu ambacho hakipendi inaweza kusababisha penzi kuvunjika.
Unabaki kuwa uongo mtamu kwa sababu kwanza una lengo la kulinda penzi, lakini pia hauna madhara kwa mpenzi wako. Huo ndiyo uongo mtamu ninaouzungumzia hapa.
Kutokana na nafasi yangu kuwa finyu, kwa leo naomba kuishia hapa, wiki ijayo nitafafanua zaidi kuhusu uongo unaokubalika kwa wapenzi.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia maagzeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is Your Valentine? vilivyopo mitaani.

No comments: