ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 30, 2012

Serikali yatangaza kiama kwa wafanyabiashara wa mbolea


Serikali imetangaza kiama kwa wafanyabiashara wa mbolea ambao wamekuwa wakichakachua mbolea kwa kuchainganya na saruji pamoja na chumvi na hivyo  kusababisha hasara kwa taifa na wakulima.

Kiama hicho kimetangazwa jana na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kuhusiana na changamoto hiyo.

Alisema tabia hiyo imezuka kwa wafanyabiashara ambao wanalenga katika kupata faida kubwa kwenye biashara wanazozifanya.

Malima alisema katika kuthibiti biashara hiyo chafu, Serikali imeanzisha Mamlaka ya Udhibiti  wa Ubora wa Mbolea ambacho kimeanza kazi mwaka huu.

Alisema chombo hicho, kitakuwa kikihusika na ukaguzi wa ghfla katika maghala, mawakala hata kwa wakulima ili kuwabaini wafanyabiashara hao na kisha kuchukua hatua za kisheria.

'‘Serikali imekuwa ikitoa ruzuku katika mbolea ambapo mkulima amekuwa akilipa nusu ya bei na lengo hapa ni kuongeza uzalishaji nchini  na kumuinua mkulima,”alisema Malima.

Alisema Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, hivi sasa yupo mkoani Ruvuma kukagua ubora wa mbolea.

Aliongeza kuwa serikali iko katika mchakato wa kuifanyia maboresho sheria ya mbolea bungeni ili kuifanyia marekebisho kwa kuongeza kiwango cha adhabu.

Marekebisho hayo yanayofanyika kwa kushirikisha maoni ya wadau yanatarajiwa kupelekwa bungeni Novemba mwaka huu.



Malima alisema tatizo la uchakachuaji linafanana sana na lile la mafuta, ambalo limekuwa likiwaingizia fedha nyingi wafanyabiashara wasio waaminifu na hivyo kutoa faini ya shilingi milioni tano kwao si tatizo.

Alisema wameshatoa mafunzo kwa wakaguzi 45 wa mbolea katika wilaya mbalimbali ambao watakuwa na kazi kubwa ya kukagua pembejeo hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: